Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MH. DKT. RAFAEL M. CHENGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi hii, na mimi niungane na wenzangu wote ambao tumeingia kwenye uchaguzi huu baada ya kuwa tumeshashinda kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Tanzania ya leo imempata Rais ambaye Watanzania wote wanamuhitaji na lazima tuwe na mahali pa kuendelea. Serikali si kwamba inakatika ni mwendelezo. Mheshimiwa Kikwete alifanya kazi kubwa sana kwa Watanzania na Mheshimiwa Magufuli amekuja kuendeleza pale Kikwete alipoishia na kuongeza zaidi kasi. Ni rahisi kuwa msemaji mzuri wa kupinga kila kitu, lakini naomba Waheshimiwa Wabunge sisi ni watu wazima tufike mahali tuwe more objective katika mazungumzo yetu. Watanzania wanatuangalia kutupima kwa jinsi tunavyoongea na uwakilishi wetu humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunazungumzia Mpango, tunazungumzia Mpango wetu wa Taifa. Bunge hili ningefurahi sana tukijikita kuzungumza tutoke hapa twende wapi, hivi vijembe na hadithi hazisaidii kwa sasa hivi, bali Watanzania tusema sasa tunataka tu-achieve kitu gani, yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache ya kuongea, jambo la kwanza naomba ni-acknowledge kwamba tumeanza Awamu ya Tano ikiwa na deni la shilingi trilioni 1.8, ukiangalia siyo hela ndogo ni hela kubwa sana. Watanzania lazima tufunge mikanda na ndiyo maana Mheshimiwa Rais amekuja na kauli mbiu ya kwamba hapa ni kazi tu. Maana yake ni nini? Kila mmoja awajibike kwa nafasi yake.
Mheshimiwa Waziri Mpango kama ilivyo jina lake Mpango ameleta mpango mzuri sana, ninaomba Watanzania tuu-support. Mpango huu utakuwa mzuri tu ikiwa tutakubaliana sisi kama Bunge twende na Mpango huu kipamoja na siyo tumegawanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia makusanyo ya kodi tumeona kwa kipindi kifupi baada ya kudhibiti mianya ya kodi yamepanda sana. Sasa hivi the tax and revenue effect ni asilimia 12 ya GDP. Kitu ambacho bado ni chini inapaswa iongezeke. Itaongezeka tu kama tutaweza kuweka miundombinu ya kuongeza uchumi wetu.
Hapa naomba niungane na wasemaji wote, huwezi ukazungumzia uchumi bila kuwa na miundombinu ya uchumi. Lazima swala la miundombinu ya barabara na reli iwekewe kipaumbele kikubwa sana. Reli ya Kati, reli ya TAZARA lazima iwekewe kipaumbele kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunaposema viwanda, kweli tunataka nchi ya viwanda lazima tuweke miundombinu ambayo itawezesha viwanda hivi viweze kweli kufanya kazi yake kikamilifu. Ukiangalia leo hii hata kwenye viwanda vya nguo malighafi inayotoka nje au inakuwa rahisi zaidi kuliko mali inayozalishwa hapa nchini.
Kwa hiyo, lazima upande wa nishati tuboreshe nishati ipatikane kwa bei ya ambayo itawezesha uzalishaji wetu uweze kupambana na bidhaa za kutoka nje. Mheshimiwa Muhongo amethibitisha, ni Waziri ambaye amejitoa mhanga, kazi yake ni sahihi na naomba tumuunge mkono jitihada zake hizi (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kwenda mbali na suala zima alilosema Mheshimiwa Mdee suala la kilimo, lazima kilimo vilevile tukipe kipaumbele, hapa siyo kusema ushabiki kwa sababu asilimia kubwa ya Watanzania wanashughulika na kilimo, kilimo hiki kiweze kuwapatia Watanzania ajira na kuongeza pato la Taifa. Bila kufanya hivyo hatutasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia juzi hapa kwamba Msajili wa Hazina ameamua fedha yote kwenye taasisi za Serikali wafungue akaunti Benki Kuu. Ni uamuzi sahihi na nauunga mkono, kwa sababu leo hii kama Serikali iweze kujua kwamba hizi public enterprises zote zinazalisha kiasi gani na mwenye mali ambayo ni sisi Watanzania tujue kinachozalishwa na kinatumikaje. Bila kujua vile inakuwa ni tatizo na ofisi ya Msajili kwa sasa naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tumuunge mkono sana Msajili aliyepo sasa hivi Ndugu Mafuru, kwa sababu huko nyuma ofisi ya Msajili haikuwa inafanya kazi inavyotakiwa hata haikujua haya Mashirika yanafanya nini yanazalisha nini wanaleta kiasi gani Serikalini, lakini kwa muundo huu mpya itasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna benki hapa zitalalamika lakini Mheshimiwa Mwenyekiti niseme hivi, hela ya serilkali ambayo ipo kwenye mabenki ni trilioni 1.1, katika hela hiyo bilioni 335 iko kwenye current account, haizai faida yoyote ile hawa jamaa wanatumia kuzalisha wenyewe, matokeo yake hata riba zinakuwa ziko juu. Sasa tuweke uwiano sawa ili benki zi-compete vizuri kwamba hakuna pesa ya bure. (Makofi)
Serikali hii ina hela hela zake kwenye current account na inakopa tena kwa riba kubwa zaidi, sielewi ni uchumi wa aina gani huu na sijui wanapokuwa wanafanya wanafikiria kitu gani. wewe hela za kwako uende kukopa tena kwa riba ya juu unafanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika hili niunge mkono kabisa kwamba Serikali kupitia Msajili wa Hazina waandae utaratibu ambao hautaleta matatizo ili pesa inayozalishwa ichangie kwenye bajeti ya Serikali, ichangie kwenye mapato ya Serikali na kuondoa ufujivu wa fedha ya Serikali. Kuna mashirika hapa walikuwa wanajigawia fedha wanavyotaka wenyewe, Bodi ikiamua imeamua. Tuachane na utaratibu huo, sasa hapa ni kazi tu. Dada yangu Halima Mdee hapa ni kazi tu, lazima pesa ipatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wabunge tunalalamika pengine baadhi ya vitu vyetu havijakaa sawa, ndiyo Serikali haina pesa itatoa wapi na sisi tuhangaike kutoa mchango utaokasaidia Serikali iweze kukusanya mapato ya kutosha na iweze kutoa huduma kwa Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna benki hapa Tanzania 54, lakini mabenki tisa tu ndiyo yamekuwa yakichezea hela ya Serikali mengine hapana! Sidhani kama kutakuwa na ulalamishi wowote ule kwa nini walalamike, isipokuwa tuongeze mapato ya Serikali
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia; huko Busega, asubuhi nilisema hapa, kuna tatizo kubwa na hili siyo la Busega peke yake, ni maeneo yote ambayo yanapakana na hifadhi za Taifa. Naiomba Serikali kupitia Wizara husika na kuwashirikisha Mawaziri wanaohusika na wadau wote, tuwe na mkakati wa pamoja. Tunahitaji tulinde hifadhi zetu za Taifa, tu-promote utalii, lakini wakati huo huo tujali maisha ya wananchi na mifugo yao ili kuweza kujenga usalama na mahusiano ya karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa agizo la Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii alilolitoa hapa, limefanya kazi. Mifugo ile nimeambiwa bado kuna hapa na hapa lakini baadhi ya mingine imeanza kuachiwa. Naomba Mheshimiwa Waziri ufuatilie tena ili vijana wako wa Game Reserves waheshimu wakulima na wafugaji walio kandokando ya hifadhi hizi. Kwa maana hiyo, tusiwe na uhasama ambao hauna tija yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze Waziri Mkuu. Waziri Mkuu ameanza kazi vizuri, endelea kuchapa kazi, Serikali yako na wanachama wote, Watanzania wote, pamoja na Rais watawaunga mkono, ahsanteni sana.