Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Mary Deo Muro

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na ninayo machache ya kuchangia kwenye Wizara hii. Kwanza namshukuru Mungu kuwa na afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuchangia eneo la mwanamke na nishati; nimeamua kuchangia eneo hili kwa sababu nimeona ni jinsi gani mwanamke anahangaika na nishati kuanzia asubuhi mpaka jioni na saa nyingine ashindwe hata kutayarisha chakula kwa kukosa nishati. Nafahamu kabisa kwamba, ndani ya jengo hili wanaume wengi wanakuta chakula kiko mezani, hawajui mwanamke amehangaika kiasi gani mpaka akifikishe mezani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia safu ya uongozi kwenye nishati naona ni wanaume wawili wamekaa pale, lakini hakuna mwanamke ambaye angesimama kwa niaba ya wanawake wa Tanzania ambao wanahangaika siku nzima kutafuta kuni ili waweze kutayarisha chakula kwa ajili ya familia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za katikati hapo nyuma, kulikuwa na mradi unaitwa biofuel ambao tulitarajia kabisa ungeweza kutumia gharama ndogo ya kumfikia kila mwanamke alipo, akapata moto poa, ambao ungeweza kumrahisishia kupika na kufanya kazi za upishi kwa urahisi, lakini mpaka sasa hivi hatuoni dalili zozote za ule mradi wa mibono ambao ungeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kueneza vijiji vingi nishati mbadala. Tunaona kuna biogas na zimetengewa pesa hapa bilioni 3.2, lakini ukiangalia kwa Tanzania ilivyo kubwa, mpaka akafikiwe mwanamke aliyeko kule kijijini pembezoni, akapate biogas itakuwa ni karne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mwanamke ataendelea kulia machozi jikoni huku akichochea vyungu, akichochea sufuria, ili mwanaume akae ale mezani, ambaye haingii jikoni na mwanaume hapati uchungu kwa sababu siye anayepika! Mwanamke ndiye anayehangaika, apike, atafute wapi kuni, atatafuta mkaa, atatafuta chochote kile, lakini chakula kiive! Namwomba Waziri anapokuja angalau atuambie amemuangaliaje mwanamke wa Kitanzania? Jinsi gani anaweza akasaidika na bajeti hii ambayo ameileta mezani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, atakapokuja kujibu, naomba Waziri aje na majibu sahihi, sana sana atuambie labda ule mradi wa biofuel umeishia wapi? Watu walishaanza kulima na mibono ilishaletwa mpaka majiko, umeishia wapi? Leo ukija kwenye bajeti hii ya 3.2 billion kwa Tanzania nzima wakati unaweza ukatumia biofuel ikaenda kwa haraka na kwa nafuu zaidi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Mkoa wangu wa Pwani. Mkoa wangu wa Pwani, Wilaya ya Kibaha, kuna mradi ambao ulikuwa unaendelea wa TANESCO wa Gridi ya Taifa, walitathminiwa wakaambiwa kwamba watalipwa. Ni Vijiji vya Kiluvya, Mwanalugali na Mikongeni, lakini tangu wametathminiwa kwenye mpango wa miaka mitano ilielezwa kwamba, wamelipwa lakini mpaka sasa hivi hawajalipwa na kinachoendelea hatuelewi! Wananipigia simu kila siku wanasema utakaposimama, tuulizie kwa Waziri, Je, hela zetu tutalipwa? Kama hatulipwi, tuendeleze maeneo yetu? Kwa hiyo, Waziri atakapokuja kujibu, ningependa kupata majibu ya maswali ya Wanakibaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuchangia yafuatayo. Kwa mfano, tunaona TANESCO imebeba mzigo mzito sana, inazalisha umeme, inasambaza, inauza! Hivi kweli, hili shirika binafsi litaweza kufanya kazi zote hizo? Kwa nini Serikali isije na mpango mwingine ambao uta-faster maendeleo ya Tanzania tunapoelekea kwenye Tanzania ya viwanda? Nadhani kungekuwa na mpango wa ziada wa kuisaidia TANESCO isifanye kazi zote peke yake; kuzalisha, kusambaza, kuuza, ndiyo maana unakuta saa nyingine…
MWENYEKITI: Ahsante.