Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, kwanza natoa shukrani za dhati kwa kunipa nafasi. Namshukuru sana Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kumteua Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Dkt. Medard Matogolo Kalemani kuwa Naibu Waziri na Makatibu Wakuu wote.
Ndugu zangu, hili Bunge tusifanye vichekesho au viigezo, tukumbuke Bunge la Tisa, sikuwa Mbunge, nilikuwa naangalia kwenye TV. Hapa Bungeni alikuwa rafiki yangu, kipenzi wangu, Waziri Mkuu anaitwa Edward Ngoyai Lowassa. Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa alijiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, hapa Bungeni. Cha ajabu jamaa wa pili hao hao wamemchukua kumpa tiketi agombee Urais awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, wanaona ajabu wakati si kweli kama Mheshimiwa Sospeter Muhongo alihusika na Escrow Account ila alisingiziwa kwa ufisadi wenu ninyi baadhi ya Wabunge, tunalijua hilo, lakini Mheshimiwa Edward Lowassa hapa alitolewa, alijiuzulu, lakini ninyi mkamkumbatia mkatembeza nchi nzima, je angekuwa Rais nchi hii ingekuaje? Ndugu zangu mnasahau matapishi yenu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sipendi kuwakashifu ninyi rafiki zangu, lakini mnashika pabaya lazima tuwaambie ukweli, mnakuwa na akili ya kusahau kama vile kuku wa kizungu au samaki anakwenda kunasa kwenye nyavu. Leo siku hata tano haijapita unasahau unataka ripoti ya kumkashifu Mheshimiwa Sospeter Muhongo na Magufuli kumchagua kuwa Waziri wa Nishati na Madini, akupe wewe kuwa Waziri, wakati ninyi hapa mmemtembeza Lowassa nchi nzima na Bunge hilihili, nchi nzima walifahamu kwamba amejiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, sasa si ajabu hii? Mnasahau…
TAARIFA...
MHE. ALLY K. MOHAMED: Hiyo ya Rais Mwinyi usizungumze, Rais Mwinyi alikuwa amelala nyumbani kwake…
…kule Magereza Shinyanga ni tofauti kabisa, wala hakuwa fisadi kama unavyofikiria wewe. Unamsingizia, Mwinyi hakuwa fisadi, Mwinyi alijiuzulu kutokana na kashfa ya Magereza Shinyanga, tofauti kabisa na rafiki yangu. Achana na ninyi, mlimtembeza mtu mnamjua kabisa mtu kajiuzulu kwa sababu ya rushwa, mkamtembeza nchi nzima, mtacheka wenyewe. Nimeshawapasha! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Wizara ya Nishati na Madini, hasa REA, imesaidia kabisa katika vijiji vyetu kupata umeme. Ninachoiomba Serikali, iwapatie pesa ya miaka mitatu ya nyuma, REA walikuwa hawajapata pesa, wanadai karibu bilioni 272 maana yake Wakandarasi wako vijijini wanadai hizo pesa mpaka sasa. Haiwezekani hizi hela za mwaka huu, bajeti ya mwaka huu, bilioni zaidi ya 500 waanze kuzimegua ili kuwalipa Wakandarasi ambao wapo kazini, lazima tuhakikishe kabisa kwamba wanapewa hela zao za miaka mitatu ya nyuma, bilioni 272 Wakandarasi wakalipwe ili awamu ya pili ikamilike bila matatizo yoyote na hizi Milioni 540 zifanye kazi kwa vijiji vyote katika nchi hii kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nataka kuzungumzia alipoishia jirani yangu Mheshimiwa Silinde, kuhusu vinasaba. Vinasaba vimepitwa na wakati, vinasaba tumezungumza mara nyingi hapa, tuliruhusu vinasaba kwa sababu ya tofauti ya bei ya mafuta. Leo bei ya mafuta inalingana nchi nzima, nani atachakachua? Tuliamua hapa mafuta ya taa yapande bei ili wasiwe wanachakachua na mafuta ya taa kweli yameteremka hayaagizwi tena nchini kutokana na kwamba walikuwa wanachakachua kwa sababu bei ya mafuta ya taa, bei ya diesel vinalinganalingana.
Mheshimiwa Spika, tunaona uchungu, yule wa vinasaba kutokana na mafuta yanayoingia nchini kwa mwaka mzima zaidi ya lita bilioni mbili, anachukua zaidi ya bilioni tisa kwenye gharama ya vinasaba. Huyu wa vinasaba faida yake ni bilioni 14. Usimamizi wa EWURA unachukua zaidi ya bilioni 13.9, wakati ukaguzi wa mafuta TBS yenyewe inachukua bilioni 2.8 kwa ajili ya kudhibiti mafuta kama yana ubora. Sasa vinasaba vina faida gani?
Mheshimiwa Spika, halafu cha ajabu, EWURA hao hao wako chini ya Idara ya Maji wakati vipato vyao vyote vinachukuliwa katika Wizara ya Nishati na Madini. Wenyewe ukiwauliza hawahusiki kabisa moja kwa moja na Wizara ya Nishati na Madini, lakini mapato yao, kila kitu wanachukua kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, nilizungumza Bunge lililopita kabla halijaahirishwa. Mpaka hawa jamaa wakawa wanatumia pesa kwenda gym, wanalipa kila mfanyakazi wa EWURA Dola 400, akienda gym asiende gym. Wanajipangia mishahara wanavyotaka, wananyanyasa watu wanavyotaka. Hivi vinasaba vimepitwa na wakati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu TRA kukagua magari ya mafuta, TRA wana vituo njiani (checkpoints) tatu au nne, lazima magari yapite, TRA ikague mafuta kama yameteremshwa njiani au hayajateremshwa njiani. Kama watumishi wa TRA ni wabovu wanagongesha mihuri, je hao EWURA ndiyo watakuwa waaminifu kama malaika? Ni kuongeza mzigo kwa walipakodi kupandisha bei ya mafuta bila sababu. Nashauri hizi pesa za EWURA ziende REA moja kwa moja kutatua matatizo ya umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka mzima pamoja na usimamizi, EWURA wanachukua shilingi 18 na senti 85 kutoka kwenye gharama za vinasaba, halafu wanachukua shilingi sita kwa ajili ya usimamizi, jumla bilioni 42 . Hizi pesa zikienda REA kule zitasaidia kutatua matatizo ya umeme vijijini, kuwalipa Wakandarasi. Kwa hiyo, naomba Serikali irudie upya hivi vinasaba, iangalie kama vina umuhimu ama havina umuhimu. TRA ndio wasimamizi wa mafuta kama yanavuka mipaka au hayavuki mipaka.
Ndugu zangu na uchakachuaji ulipitwa na wakati, tulikuwa tunachakachua kwa sababu mafuta ya taa yalikuwa chini kabisa, mia tano, mia sita, tumeongeza ile bei ili wananchi wapate umeme vijijini, sasa nashangaa bado wanaendelea na vinasaba ili kuumiza wananchi wetu na havina faida wakati huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, hawa jamaa wa REA tuwape pesa kama inavyotakiwa. Hizi pesa ziende moja kwa moja REA zisipitie Hazina. Zikipitia Hazina zinakuwa na vigezo, miaka mitatu mfululizo, REA hawakupata hela kama inavyopangwa, miaka mitatu nimepiga hesabu hapa ni milioni 272, REA hawajapata hela. Wakandarasi wanadai kule vijijini, wanadai tozo kule vijijini, lakini sababu pesa ziko Hazina, hizi pesa zimeshatoka kabisa sasa kwa nini zisiende moja kwa moja REA ili REA wafanye kazi na tuwawajibishe kama hela hawajawapa wakandarasi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile naishauri Serikali, kwanza naishukuru sana kupunguza tozo ya umeme ili wananchi wetu wapate, lakini vilevile ndugu zangu wa mijini wamekaa wanaiba umeme, tatizo kubwa. Ni tatizo kubwa, haiwezekani mtu ana AC tatu, ana kiwanda hawafuatilii, Serikali kama wanashindwa REA peke yake kufuatilia TANESCO watafute JKT wapite nyumba kwa nyumba hasa mijini. Watu wa mijini wamekuwa wezi wakubwa wa umeme, wanaiba umeme mchana kutwa, Manzese wanasaga usiku wanaiba umeme, viwanda vidogovidogo wanaiba umeme, wanaoumia ni watu wa kijijini ambao hawana utaalam wa kuiba umeme.
Mheshimiwa Spika, mpaka baadhi ya watu wakubwa Serikalini wanaiba umeme, mashule makubwa makubwa yanaiba umeme, mahoteli yanaiba umeme. Ndugu zangu hatuwezi kufika, tuibe umeme, tuibe na maji, halafu hapa tunakuja tunalalamika tunataka kila kitu wakati sisi wote tunasaidia wizi.
Mheshimiwa Spika, unakuta Mbunge anamwona mtu anaiba umeme, hatoi ripoti, bado anamsaidia, tuna kazi ya kuilaumu Serikali, hatuipigi vita kwa njia ya namna hiyo, tumsaidie Rais Magufuli kutumbua majipu hata katika wizi wa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mkurugenzi wa TANESCO, Mkurugenzi wa REA, wanafanya kazi, inabidi tuwaunge mkono. Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo usisikie maneno ya majungu, mimi nilikuwa kwenye Kamati ya Public Account Committee, ni uzushi yule James Rugemalila alikuwa anadaiwa kodi, ndipo tuliamua alipe kodi; hana kashfa yoyote, kashfa kama mnayo nyie kwa majungu yenu hatoki na anakaa pale kwa niaba ya Serikali ya CCM. Ataendelea kufanya kazi na katika Mawaziri wachapakazi hakuna kama Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, hana siasa. Mnataka kwenda kwa vigezo vya rushwa, huyu hali rushwa, wala kashfa ya ESCROW Account hamkumwona hata kapewa kiroba cha hela waliopewa hela walitajwa humu yeye hahusiki.
Mnamsakama bure hamfanyi lolote, aliyemchagua Rais Magufuli kwa niaba ya Serikali ya CCM, kwa hiyo hawezi kubanduka atachapa kazi. Ngojeni na ninyi wananchi watawachagua na kutokana na uongo wenu wameshawagundua hamuwezi. Mmeshapigika huko nje mnaleta fitina za uongo hapa, hamkubaliki kwa speed ya Magufuli inayokwenda kama umeme. Kwa hiyo, Rais Magufuli speed yake hamuipati, shemeji zangu nawaambia ukweli, mliboronga kuchagua mtu aliyekataliwa na Bunge, akajiuzulu, mkamtembeza nchi nzima, sasa safari hii ndugu zangu kaeni chonjo mtapungua siku hadi siku. Ahsanteni sana. (Makofi)
SPIKA: Mlichokoza wenyewe jamani, jamani taratibu tufike au siyo. Haya, ahsante sana Mheshimiwa Ally Keissy hayo ndiyo mawazo yake, msimlaumu wala msimshutumu. Mheshimiwa Ahmed Shabiby mchangiaji anayefuata na Mheshimiwa Stephen Masele ajiandae.