Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha bajeti yao hapa Bungeni. Yapo mambo ambayo nilikuwa napenda kupata ufafanuzi wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya ndege; ukisoma kitabu cha hotuba ya Waziri, ukurasa wa 90 – 91 unaeleza kuwa kupitia TCAA Serikali itaendelea kusimamia uboreshaji wa viwanja vya ndege na kiwanja cha ndege cha Nduli kikiwa kimojawapo. Lakini ukiangalia hali halisi ya kiwanja cha ndege cha Nduli kipo katika hali mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanja kina matatizo makubwa sana katika njia ya kurukia na kutua ndege (runways), kiwanja hakina fence, kila siku mifugo inapita katikati ya kiwanja. Kutokana na mafuriko yalijitokeza mwaka huu kiwanja kimeharibiwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2015 safari za ndege zilikuwa 2,300. Idadi ya abiria kwa mwaka 2015 walikuwa 8,300 hivyo ni ongezeko la asilimia 198 kwa safari za ndege katika kipindi cha miaka mitano. Kuna ongezeko la wasafiri wanaosafiri kwa ndege, ni asilimia 90 kwa kipindi cha miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mbuga ya wanyama ya Ruaha; kama kiwanja hiki kitakamilika kwanza tutaongeza utalii na pia tutakuza uchumi wa Mkoa na Taifa zima. Naomba kujua kama kiwanja hiki kitajengwa kwa sababu katika mpango kipo, lakini muda ndiyo leo Waziri atupe jibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara za kiuchumi mkoa wa Iringa. Serikali ya Awamu hii ya Tano, sera yake ni ujenzi wa viwanda ili kukuza kwa uchumi wa nchi na kutengeneza ajira kwa wananchi. Katika mkoa wetu wa Iringa barabara nyingi za kiuchumi bado hazijaweza kujengwa kwa kiwango cha lami pamoja na kwamba katika hotuba yake kuna baadhi zimetengewa fungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kilolo; barabara ya Ipogolo - Kilolo, makao makuu, hii barabara inaunganisha Mkoa na Wilaya kilometa 37, lakini iliyojengwa kwa lami ni kilometa saba tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mufindi; kuna kiwanda cha karatasi, viwanda vya chai, msitu mkubwa; barabara zake ni Mafinga - Mgololo - Changalawe kupitia vijiji vya Sao Hill, Mtila - Matana kutokea Nyororo, Nyororo – Kibao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu reli ya kati; ili kuponya barabara zetu ni vema Serikali ikaijenga. Ushauri wangu ni kuwe na TANRAIL ambayo itafanya kazi kama TANROADS kuweza kusimamia masuala ya reli nchini, mfano reli ya kati, reli ya TAZARA, reli mpya kwenda DRC, hii ya Tanga - Uganda, Tanga - Kigali; itasaidia kubeba mizigo mingi, itasaidia kulinda barabara zetu, itasaidia kupunguza gharama, itasaidia kufungua fursa ya ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya TAZARA; muda mrefu Serikali inazungumzia kupitia upya mkataba wa Sheria za TAZARA, je, Serikali imefikia wapi? Ni kwa nini kwa upande wetu tusitumie reli ya TAZARA kwa usafirishaji wa ndani ya nchi, tuliambiwa upande wa Zambia wanafanya hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mishahara ya wafanyakazi wa TAZARA imefikia wapi, hakuna tena mgogoro? Naomba kupata majibu ya Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.