Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii ya kuzungumza mbele ya Bunge lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze moja kwa moja, nina miradi ya barabara ambayo iko kwenye Wilaya yetu ya Bukombe ambayo namuomba Mheshimiwa Waziri aiangalie kwa jicho la pili kwa sababu Wilaya ya Bukombe kwa ramani yake jinsi ilivyo, upande wa Kusini imepakana na hifadhi kwa hiyo hakuna namna ya kupita. Namna pekee ya kufungua Wilaya ya Bukombe ni kufungua barabara za upande wa Kaskazini. Kwa hiyo, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri utuangalie Wilaya ya Bukombe utuunganishe na Wilaya nyingine za Mkoa wa Geita na mikoa ya jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, iko barabara inayotokea Ushirombo inapita Katome, inapita Nyang‟orongo, inapita Nanda, inapita Bwelwa, inapita Iboya, inapita Bwendamwizo, inapita Ivumwa, inapita Wigo, inatokea Nyaruyeye Wilaya ya Geita, inakwenda Nyarugusu inatokea Buyagu hadi Geita Mjini. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inawasaidia wananchi wa Wilaya ya Bukombe kusafirisha mazao yao kuyapeleka Geita. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inawaunganisha wananchi wa Wilaya ya Bukombe pamoja na wananchi wa Wilaya ya Nyang‟hwale kwenda mkoani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia, Mheshimiwa Waziri aingalie barabara ambayo inatuunganisha Bukombe pamoja na Wilaya ya Chato. Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Geita, kwa wananchi wa Chato, pamoja na wananchi wa Bukombe. Barabara yenyewe ni hii inayopita Bulega, inatokea Kavoyoyo, inaenda Shisabi, inaenda Mwabasabi, inaenda Matabe, inatokea Bwanga kwa Dkt. Kalemani, tunaunganishwa na Daraja moja la Nyikonga. Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana hii barabara ni muhimu sana, uiweke na yenyewe iweze kutusaidia kwenye kukuza uchumi wa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Lunzewe Bwanga, leo ni miaka miwili imesimama haijengwi. Ni barabara ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami, kwa muda wote huu haijafanyiwa kazi, lakini mbali na hivyo wananchi wa Lunzewe pale hawajalipwa fidia kwa miaka yote hiyo. Hawawezi kuendeleza nyumba zao, hawawezi kufanya chochote kwa sababu wanasubiri fidia kutoka TANROADS. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri utusaidie barabara hii ijengwe, lakini vilevile wananchi wale waweze kupata fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vilevile, Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliwaahidi wananchi wa Bukombe; na hii ni sauti ya wananchi wa Bukombe inakulilia Mheshimiwa Waziri, kilometa tano za lami kwenye Mji wa Ushirombo tunaziomba. Sijaona mkakati wa aina yoyote wa kutekeleza ahadi hii, ninakuomba sana, wananchi wanaamini kwamba ahadi hii itatekelezwa na tuanze sasa hivi. Kilometa tano tu na sisi pale tupate lami Mheshimiwa Waziri, ili siku ukija na suti yako usitoke na vumbi, uje uko smart, utoke ukiwa smart kwa sababu utakuwa umetuleta barabara ya lami. Ninakuomba sana uzingatie hilo Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, uwanja wa ndege wa Geita. Mkoa wa Geita ndio mkoa unaotoa dhahabu na madini, Wizara ya Nishati na Madini mapato yake makubwa yanatokea Geita, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba pamoja na upya wake hatuna uwanja wa ndege. Uwanja wa ndege tuanaotumia ni ule wa Geita Gold Mine. Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri, umeonesha hapa kuwa ziko fedha ambazo zimepangwa kwa ajili ya uwanja wa Geita, tunaomba fedha hizo zitolewe, uwanja wa Geita ujengwe kwa haraka ili wananchi wetu waweze kupata maendeleo na usafiri wa anga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ninaomba vilevile nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, ile barabara inayotoka Katoro kuja Ushirombo, inapita Nyang‟hwale, barabara hii ni barabara kubwa inapitisha magari makubwa. Barabara hii tunaomba na yenyewe uiwekee lami kwa sababu, hii barabara ukiiwekea lami, utapunguza mizigo kwenye barabara ya Bwanga ambayo kwa vyovyote vile haiwezi kuhimili mizigo ya magari mengi yanayopita pale.
Mimi ninafahamu kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano mambo haya yanawezekana. Ninakutia moyo Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, ninakutia moyo nikiamini kwamba maneno haya niliyoyaomba na sauti ya Wanabukombe utaizingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Mungu akubariki sana. Naunga mkono hoja.