Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze na mimi kuchangia hotuba hii ya bajeti muhimu sana hii, bajeti ya Wizara ya Ujenzi.

Kwanza nikupongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wako kwa kazi mnazofanya, lakini kipekee niombe kushukuru kwa jambo moja kubwa ambalo limefanyika kuanza ujenzi wa barabara ya Laela – Mnokola kwa kiwango cha lami ambapo tayari pesa shilingi bilioni tatu zimefika na shughuli imeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niongelee kwa umuhimu wa pekee juu ya barabara hii; barabara hii target ni kujenga kilometa 66 ambazo zinaunganisha Jimbo la Kwela na nchi jirani ya Zambia kwa maana ya pale Mozi katika Province ya Mbala. Barabara hii ina umuhimu mkubwa, hiki kipande tulichoanza ni kidogo sana, maana yake hapo tunapofika pale Mnokola ni kilometa chache, sasa ili tuweze kuwa na impact na tukaona hii barabara itasaidia uchumi wa Jimbo la Kwela na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla, kuna haja sasa Serikali mje na mkakati wa kuendeleza hii barabara ili ikafike pale mpakani Zambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani, sababu yangu ni kubwa na ni ya muhimu kwamba tuna border yetu ya Tunduma ameiongelea dada yangu hapa Mheshimiwa Fiyao, ni border ambayo inapokea mizigo mingi na imefikia mahali imekuwa imezidiwa. Sasa kitendo cha kutengeneza barabara hii tutaweza kuongeza ile speed ya mizigo ile iliyo Tunduma tukaipitisha Laela, kupitia Jimbo la Kalambo na baadaye kupitia Zambia ikafika kwa urahisi. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, barabara hii ni ya kimkakati kabisa na barabara hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, namshukuru ameanza kuitekeleza kwa vitendo na hivi ninavyoongea wakandarasi wako site. Cha msingi focus yetu juu ya barabara hii tuhakikishe inafika kwenye nchi jirani ya Zambia, tutakuwa hapo tumefanya ufanisi mkubwa ambao utakuwa na tija kwenye uchumi wa Mkoa wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, nataka niongelee Barabara ya Muze – Ntendo. Tayari ilitangazwa tender tangu mwezi wa saba, ninavyoongea hivi ni mwaka mzima na katika swali langu la nyongeza juzi, nilikuuliza Waziri kwamba kwa nini huyu mkandarasi mwaka mzima hajaripoti site? Na tayari mkataba kuanzia mwezi wa tisa mwaka jana alikuwa ameshasaini mkataba wa kuanza hiyo barabara? Maana yake mwaka mzima mtu ana mkataba mezani, lakini kazi hajaanza kufanya, madhara yake ni yapi Mheshimiwa Waziri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, itasababisha huyu mkandarasi siku anafika site mkataba umesha-expire na baadae tunaanza kupigwa interest ambazo hazikukusudiwa kwenye mradi huu. Nikuombe sana barabara hii ni muhimu sana na ndio inachagiza mapato kwenye Halmashauri yetu ya Sumbawanga DC. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri mkandarasi aende kuripoti site, lakini kwenye barabara hiyo hicho ni kipande tu cha kufika Muze kilometa 37. Hii ni jumuisho la barabara ya jumla ya kilometa 200 mpaka Kilyamatundu, barabara hii ndio barabara inayobeba uchumi wa Bonde lote la Ziwa Rukwa na Jimbo lote la Kwela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii barabara kuna kipande kimekuwa na huyu consultant aliyepewa kufanya upembuzi yakinifu mwaka wa tatu sasa no plan. Hiyo report haijakamilika na barabara hiyo ya Kilyamatundu – Muze – Ntendo mpaka Majimoto inaunganisha mikoa mitatu kwa pamoja, Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Songwe na Katavi n akule tayari kuna shughuli nyingi za uchumi zinaendelea pale. Tuna hawa watu wa gesi ya helium wako kule site, lakini barabara ni mbovu na ubovu wa barabara hii Engineer Kasekenya tulienda na wewe mwaka jana, ina madaraja ambayo kila mwaka lazima yabebwe na mvua na yale madaraja yanagharimu takribani shilingi bilioni tisa mpaka shilingi bilioni 10 kila mwaka na huwa hakuna option, lazima yatengenezwe kwa sababu, yakishaondoka hakuna mawasiliano popote. Kwa hiyo, solution ni barabara hiyo ya lami iweze kujengwa kwa wakati, kama alivyosema ndugu yangu Mheshimiwa Mwenisongole, barabara yake yenyewe inaishia Kamsamba ambako ni Kilyamatundu, unatoka hapo unaunganisha na Jimbo la ndugu yangu Mheshimiwa Geofrey Pinda, kule Kavuu. Tayari mtakuwa mmefanya connection ya mikoa mitatu at per kwa maana ya Songwe, Katavi na Rukwa na impact ya uchumi kwa sababu bonde lile unajua jinsi lilivyokuwa na ardhi yenye rutuba, kilimo kizuri cha mpunga, lakini Ziwa Rukwa linazalisha samaki wengi, mtakuwa mmeinua uchumi wetu kwa namna ya pekee kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine la tatu ambalo nataka niongelee na limeongelewa na Wabunge karibu wote waliosimama wa Mkoa wa Kigoma, Rukwa na wa Songwe wanaongelea habari ya uwepo wa hizo meli katika Lake Tanganyika. Ameongea ndugu yangu Mheshimiwa Assa kwa data ambazo zimetoa picha halisi juu ya umuhimu wa kuwa na meli ndani ya Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, meli ya Liemba iliondoka kwenda kwenye matengenezo, lakini Mwongozo, mpaka leo hii hatujui zitarudi lini, basi tuombe meli mpya, sisi tunafanya shughuli za kilimo, soko kubwa kama alivyosema ni DRC. Hata mapato ya bandari tunayojinasibu kwamba bandari kwa mwaka huu itaweza kuandika faida ya kuingiza trilioni moja kwa mara ya kwanza ni kwa sababu ya DRC peke yake kama nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, DRC ina sehemu kuu kubwa ambazo ukienda eastern part kuna sehemu ambayo unapitia bandari ya Kigoma, lakini kwenye upande mwingine wa Katanga lazima upite kupitia Mkoa wa Rukwa kwa maana ya Kasanga, upite Kabwe na Kalema kwa upande wa Katavi. Kwa hiyo, hii sio option, tumejenga zile bandari, lakini tuhakikishe kwamba sasa meli inakuja ili bandari zile tulizoweka mabilioni ya fedha ziweze kuwa na tija ya kuinua uchumi wa mikoa hii mitatu kwa wakati mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, niongelee jambo ambalo lilifanyika wakati wa zamani sana miaka zaidi ya 20 iliyopita. Kulikuwa na mpango wa kuunganisha reli ya TAZARA na Mkoa wa Rukwa kwa maana ya mpaka kufika kwenye bandari ya Kasanga na bandari ya Kabwe kwa maana ya kujenga reli inayounganisha reli ya TAZARA. Itapita katika Jimbo langu la Kwela, Laela, itapita Kaengesa itaenda Matai kule Kalambo kwa ndugu yangu Mheshimiwa Kandege na baadaye tutaunganisha bandari ya Kasanga, hii reli ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ile document iliyofanyiwa kazi na NDC mkaifufue upya muanze kufikiria kwa sababu tusipofanya hivyo tutawafukuza watumiaji wa bandari yetu ya Kasanga ambao ni wa DRC wataenda kwenye bandari nyingine za Namibia, wataenda bandari za Msumbiji na South Africa kwa sababu speed yetu inacheleweshwa kwa sababu miundombinu yetu bado sio rafiki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe pia ndugu yangu Mheshimiwa Engineer Kasekenya utakuwa na kumbukumbu ulipofanya ziara ndani ya Jimbo langu la Kwela, kuna ahadi za kujenga barabara kiwango cha lami kwenda Seminari ya Kaengesa, kilometa tatu mmezichukua ninyi TANROADS. Nikuombe sana hii ahadi mkaitimize kwa sababu ile ahadi ni ya Mheshimiwa Rais mwenyewe Mama Samia Suluhu Hassan, lakini pia wewe mwenyewe ulivyokuja jimboni kwangu ulijionea umuhimu wa barabara hii. Nikuombe sasa katika bajeti hii tunayoenda kutekeleza muone namna ambayo mnaweza mkakamilisha barabara hii ya Kaengesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, sio mwisho kwa umuhimu, naomba niwaombe Mheshimiwa Waziri na Naibu tunahangaika sana na Mheshimiwa Rais anahangaika sana kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Pengine unaweza kupata financing kutoka kwenye Britain Institutions kama World Bank na taasisi nyingine African Development Bank, naomba kwenye usimamizi wa fedha hii inapofika mkandarasi amefanya ile kazi tumlipe malipo yake kwa wakati. Kuweka hizi pesa na ninajua sio jambo la kawaida, haiwezekani karibia kila miradi mingi lazima kuwe na ucheleweshaji ambao tunasababisha kulipa interest kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kawaangalieni wanaofanya approval kwenye level ya Wizara au Wizara ya Fedha, yawezekana kuna ujanja fulani unafanyika ili malipo yacheleweshwe kwa makusudi baadae itokee interest, jambo hili halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anapambana kwa namna ya pekee kutafuta fedha. Nimekupa mfano, leo hii nilikuwa naangalia kuna fedha hapa interest tulipigwa kwa ajili ya kuchelewesha malipo nina figure nyingi hapa sitaki kuzitaja sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu ya muda nitakuletea uone impact ya tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakuwa tunapata mkopo wa kujenga, lakini tunacheleweshwa makusudi, aidha iwe katika Wizara yenu hiyo ya Ujenzi au Wizara ya Fedha. Kaeni mjitathmini kati ya Wizara hizo mbili ni namna gani mnaigharimu Serikali kwa kulipa interest kwa wakandarasi ambazo hazina sababu yoyote ile kwa sababu tuna room, mkataba unatupa, section ina-provide siku 56 anapo-submit invoice mkandarasi tuwe tunafanya tathmini. Sasa mpaka zinapita siku 56, zinafika siku 100 mpaka 160 interest ina-accrue, badae tunalipa fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nimuombe Waziri, nilikuwa nataka nije kushika shilingi kwa sababu ya jambo hili, niombe tu kalifanyie analysis ya kutosha uone ni hasara ngapi Serikali imepata, kama kulikuwa watu wamefanya uzembe, kachukue hatua ya haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii system ya defund system ina approval nyingi. Lengo la approval ni kufanya control kwa maana mmeweka level 16, lakini kama hiyo control inaenda kutusababishia hasara ya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nendeni mkatafute level chache tu ambazo watakuwepo watu makini, wanafanya scrutiny ya documents zetu wana-approve malipo yanafanyika, ili tuepukane na interest hizi tunazolipa pasipokuwa na sababu yoyote ile, nikuombe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho sasa, sio mwisho kwa umuhimu, watu wameongea sana Mkoa wa Rukwa sisi pekee ndio hatuna uwanja wa ndege. Tuna vivutio vikubwa vya utalii kama Kalambo Falls na Uwanda wa Ziwa Rukwa kule tuna Nyanda za Lyamba Lyamfipa nzuri kabisa, lakini uwanja wa ndege ambao unaweza uka-promote utalii katika eneo hili hatuna, mwaka wa tatu uwanja wa Sumbawanga unaongelewa katika bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Waziri, tumechoka na tumekubaliana, niko na wenzangu, kwenye hili sasa tutashika shilingi tujue uwanja wa ndege wa Sumbawanga mnajenga lini ili na Mkoa wetu wa Rukwa uweze kuinuka sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahangaika mpaka tuende Songwe uwanja ambao walikuwa wanagombaniana jina. Sisi hata wa kugombania jina haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)