Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Assa Nelson Makanika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana Wizara hii ambayo hakika ni Wizara yenye kuchochea uchumi kwa Taifa lolote lile ambalo lina mpango wa kujiendeleza. Awali ya yote kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pili nimshukuru Mheshimiwa Rais, nimshukuru na Mheshimiwa Waziri kwa jitihada kubwa sana anazozifanya na ndipo niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa umejikita katika maeneo matatu; eneo la kwanza ni miundombinu yenyewe kwa ujumla wake ambao imebeba bandari, miundombinu ya barabara, reli na hatimaye usafiri wa anga. Hivi leo tunajadili Wizara hii na Mheshimiwa Waziri unisikilize vizuri. Wizara yako ndio iliyotufikisha mahali hapa tulipo na kama Wizara yako ingeweza kutazama na kuwa na fungamanisho na Wizara zingine hivi sasa uchumi wetu ungekuwa umekwisha ku-take off kutoka hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni kweli Kigoma na tunaishukuru Wizara yako Mheshimiwa Waziri, Kigoma kwa upande wa barabara tunachokiomba kwenye Wizara yako, ni kutia mkazo na kuharakisha barabara hizi za kuunganisha Mkoa wa Kigoma ziweze kukamilika kwa wakati. Lakini tuna barabara ambayo ni changamoto sana, barabara hii nimekufikisha barabara ya kuanzia Mwandiga inakwenda mpaka Kata ya Kagunga. Barabara hii inapita katika kata tatu ambazo kata hizo zinajumuisha wananchi karibu 70,000 Kata ya Kagunga, Kata ya Ziwani na Kata ya Mwangongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umesikia watu wanaomba barabara kwamba iwekewe lami, pale hatuombi barabara kwamba iwekewe lami tu, ni kwamba hakuna barabara kabisa. Hivi sasa sijui unaweza ukawaambia nini wananchi wa kata hizo, wananchi wa kata hizo wanakwenda kupata matibabu nchi jirani ya Burundi, wananchi wa kata hizo wanakwenda kutafuta huduma zote ambazo ni stahiki katika nchi jirani ya Burundi. Lakini wananchi hao wanatoa kodi katika nchi yetu ya Tanzania, kesh/kesho kutwa utawaambia nini kwamba waone fahari ya wewe kukupa kodi ikiwa kodi wanakupa wewe lakini miundombinu kama hii ya msingi wewe hauwapatii? Upande wa Burundi wameweka mpaka lami, wakitaka kufika sehemu ya Tanzania wanapita nchi ya Burundi ndipo waweze kuingia Tanzania, kwa hili tunahatarisha hali ya usalama wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni ya kiusalama huko tuna Kambi ya Jeshi ukienda Kagunga, lakini hata ukiachilia usalama barabara hii ni barabara ya kiuchumi. Huko tuna Hifadhi ya Gombe, mtalii kufika Gombe ni lazima apite njia ya maji, asipopita njia ya maji hawezi kufika Gombe. Kwa nini tusipeleke miundombinu hii ili iweze kuchochea uchumi wa kitalii? Mheshimiwa Waziri litazame hilo sana ili uweze kuwasaidia wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa kata hizo tatu. Lakini kutoka bajeti iliyopita mpaka hii ya sasa tumepoteza zaidi ya wananchi 102 mpaka dakika ya sasa kwa sababu ya kukosekana barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamama wajawazito wanahitaji kujifungua ili wafike Maweni, Kigoma Mjini wanapita njia ya maji wengi wanafia ziwani. Mheshimiwa Waziri uweze kutazama hivi vifo mimi ninaamini Wizara yako haiungi mkono tuweze kupoteza Watanzania wenzetu. Uweze kukaa chini, utazame, ufikirie na hawa ni Watanzania wenzetu, uweze kuokoa maisha yao na wao ili waweze kuona fahari hata hata hao wanaobaki ya kwamba waache kupoteza mama zetu ambao wanaiaga dunia kila kukicha. Natambua ya kwamba kumekuwa na jitihada nyingi sana kuhusu hii barabara naomba sana Mheshimiwa Waziri uweze kuongeza nguvu sana ili hii barabara iweze kutoboka haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni jambo la bandari; bandari ni mojawapo ya kitu ambacho kinaingiza mapato katika nchi hii, lakini katika nchi hii tuna bandari mjumuisho, bandari ambazo zimerasimishwa na ambazo zisizo rasmi zaidi ya 600 na kitu. Lakini ndani ya hizo bandari 600 na kitu bandari mbili tu katika nchi nzima ndizo zinazojiongoza kwa faida. Moja ni bandari ya Dar es Salaam; mbili ni bandari ya Kigoma, bandari zingine zote ambazo mnapeleka miundombinu zinajiongoza kwa hasara. Leo hii shilingi 100 inayozalishwa katika bandari ya Dar es Salaam na shilingi 100 inayozalishwa katika bandari ya Kigoma inaweza ikatumika shilingi 80, shilingi 20 ikaenda kwenye Mfuko wa Hazina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini shilingi 100 inayopatikana katika bandari ya Mwanza inatumika yote na tunakopa shilingi 20 tunakwenda kuwalipa wafanyakazi katika bandari zingine. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumueleza mchangiaji kwamba Mwanza kwa sababu ya kukosa miundombinu ya treni ndio imeonekana haizalishi bandari yake, lakini bandari ya Mwanza ni bandari ya pili kwa ukubwa na ni bandari ya pili kwa uchumi katika nchi hii, asilete hadithi. Ahsante sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Assa unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siipokei, nina data kamili hapa ninaweza nikamsaidia kaka yangu hapa aweze kuelewa nina chanzo cha hali ya uchumi wa Taifa mwaka 2020, kimetoa hii takwimu, nitakupa nikusaidie tu kidogo maarifa madogo haya, ya kwamba nchi ya DRC Congo ndio soko ambalo tunaelekea mpaka dakika ya sasa. Asilimia 34 ya mizigo ambayo inaingia katika bandari ya Dar es Salaam inaelekea Congo na ikieelekea Congo maana yake ni Kigoma njia pekee. Asilimia 23 ya mizigo ambayo inapitia bandari ya Dar es Salaam inaelekea Rwanda, asilimia tisa inakwenda Zambia jumla ya asilimia 63 ya mizigo yote inayoingia nchini inaelekea ukanda wa Kigoma haiwezekani Mwanza ikawa ndio bandari ambayo inaingiza uchumi mkubwa, hiyo haiwezekani hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee na mchango wangu na itoshe tu kukuambia ya kwamba hali ya takwimu hizi zinazoonesha, hali ya uchumi wenyewe inatuambia miaka mitatu mfuatano inaonesha hali ya uchumi ya kwamba bandari ya Kigoma na ya Dar es Salaam ndizo zinajiongoza kwa faida na sio bandari nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natarajia kwamba Wizara iweze kutazama mambo haya nadhani jambo ambalo linakosa katika uchumi wetu ni linkage pekee, uchumi wetu hauna linkage leo hii tunaweza tukaona the growing market ya bandari ambayo inaelekea mpaka sasa ni Congo, lakini sisi tunaweza tukatoa reli tukapeleka kwingine wakati tunaliacha soko linakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Congo imeingia sasa hivi East Africa, Congo sasa hivi imeingia kwenye soko la East Africa, imekuja kuwa sehemu ya Jumuiya tumejipangaje kuliteka hili soko la Congo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuliteka soko hili ukiitenga Kigoma unaumiza Taifa, ukiitenga Kigoma katika kuteka soko hili unaliumiza Taifa zima, hauiumizi Kigoma pekee. Hivyo mimi ninashangaa reli mpaka dakika ya sasa mara tu baada ya Congo kusema kwamba anaingia kwenye Jumuiya hii tungeelekeza nguvu kubwa kuelekea Kigoma ili tuweze ku-save hii mizigo, asilimia 63 ya mizigo yote tunayotoa na kuingiza inapita hapa. Kwa nini tusielekeze Congo ili tuweze kuteka huu uchumi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika hivyo hivyo nashangaa sana hata meli, hakuna hata meli moja mpaka sasa hivi ambayo ina-operate katika Lake Tanganyika haipo. Leo hii Kigoma haina hata meli moja, MV Liemba chali haifanyi kazi, Mwongozo chali haifanyi kazi, mnataka uchumi gani wa Congo muuteke? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa tu nilizonazo ambazo ni za uhakika hata meli ambayo imejengwa ya Mwanza haifai na wanasema hakuna bandari ya kuweza kuipokea ile meli ni kubwa, unaelekeza kule kwa nini tusielekee Kigoma. Hii sio kwamba nachukia sehemu zingine, ninajaribu kuonesha ya kwamba soko pekee tupende tusipende kama tunahitaji mapato mengi sharti tuelekee Kigoma. Hivi sasa juzi Mheshimiwa Bashe ametuambia kwamba anakwenda kusaidia hii crisis ya mafuta, I can tell you two years or three years we are going to fail, crisis ya mafuta itarejea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote nina mifano ya kutosha na Kigoma msichukulie hata mchikichi, nilitaka nimuambie Mheshimiwa Bashe mchikichi sio long plan ya kufanya sasa hivi, kwa sababu michikichi inalimwa Kigoma miaka na miaka pelekeni teknolojia kuna mafuta mengi yanapotea kule Kigoma. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Assa, muda wako umemalizika.

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nitachangia kwenye Wizara zingine mbele. (Makofi)