Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi hii, lakini naomba sana nimshukuru Mwenyezi Mungu kwamba ametufikisha leo siku ambayo tunaenda kuijenga nchi yetu kwa kuitengenezea uchumi thabiti. Uchumi thabiti wa nchi hii unategemea sana miundombinu ambayo leo ndio tunaijadili kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, ili Tanzania iendelee na ili uchumi wa Kyela ukue kuna vitu ambavyo tunavihitaji; kitu cha kwanza ni kuhakikisha barabara yetu ya kutoka Ibanda kuelekea Itungi ports inakamilika kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hii najua imetangazwa lakini naomba sana Serikali ihakikishe inafanya haraka kwasababu tayari bandari yetu na meli zetu zimekamilika na zipo tayari kwa ajili ya kufanya kazi pale Itungi port. Hii barabara isipokamilika zile meli hazitafanya kazi.

Mheshimiwa Spika, uchumi wa Kyela pia unategemea sana Bandari ya Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam ndio inayopeleka mizigo yote inayokwenda Malawi na pia kuelekea hadi Zimbabwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bandari yetu vyovyote vile ninajua sisi hapa tulipo tulikuwa tunajitahidi kuona ni jinsi gani ambavyo nchi yetu inajikwamua kiuchumi kupita bandari, tunajua nchi nyingi Malaysia wamekuwa matajiri wanaenda kwa sababu ya bandari, sasa nataka tu niwahakikishie Watanzania na niseme mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu nataka nilihakikishie Bunge; katika kipindi ambacho watanzania na Bunge hili linatakiwa kujivunia ni kipindi hiki, bandari yetu inakoelekea ndugu zangu tunakwenda mahali pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu ndiye msema kweli, leo mzigo wa pale bandarini umeongezeka kwa asilimia 21 sio kitu cha mchezo, na katika hili tusipoipongeza Serikali na katika hili tusipompongeza Rais kwa kumuona Erick na kumfanya awe ni DG pale tutakuwa tunafanya makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna wakati tunafanya vikao kwenye Kamati unaambiwa DG wa bandari hayupo, ukiuliza yupo wapi wanakwambia yupo Rwanda, yupo Congo, DG anajibeba kwenda ku-negotiated, kutafuta masoko hiki kitu hakikuwahi kutokea huko nyuma, leo hii tusipompa nguvu huyu Erick, tusipomsifia, tusipompa nguvu na kumpa ari, nafikiri tutakuwa tunafanya makosa makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema bandari hii ndio kioo chetu na ndio sehemu yetu ya uchumi magari yote yanayotoka bandarini yanapita barabara ya TANZAM kuelekea Malawi. Nataka tu nisisitize ninaomba sana pale Inyara nafikiri ni Mbeya, lakini nataka niseme pale Inyara ni lazima tujenge bandari ya nchi kavu, Wamalawi, Wazambia na nchi zote za SADC ni lazima zije zichukue pale mzigo ndipo tutakapokuwa tumerahisisha kazi na tutakuwa tumejenga uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee TRC kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa; ni kweli wananchi nataka niseme ndugu zangu sisi Bunge hili tulikuwa tunategewa sana mwaka 2025 tuchekwe, watu walijiandaa watucheke, lakini nataka nishukuru kwamba safari hii vicheko vinarudi kwetu, kilio kinarudi kwao, kwa sababu mambo yanayoendelea kwenye reli yetu, kwenye SGR ni mambo ambayo wengi hawakuyategemea, walidhani yatasimama, lakini sasa yanasonga mbele na katika hili nataka nimpongeze sana Mtendaji Mkuu wa TCR na nafikiri kupongeza ni sahihi, lakini tumpongeze pale ambapo amefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo ambalo huwa wakati mwingine tunaliangalia kijuu juu, leo hii ujenzi wa reli Tanzania ni ujenzi ambao ni the cheapest duniani, tunajenga kilometa moja kwa wastani yaani ukichanganya zote halafu ukapata wastani kwa dola milioni 3.8 hii ni kiwango ambacho kipo chini ukilinganisha mpaka na nchi zetu jirani ambao wamejenga SGR lakini siyo ya umeme. Wenzetu wengi wamefika kwenye sita wanaenda mpaka nane. Mimi nataka niseme Tanzania ni lazima tutembee kifua mbele kujivunia kwamba tuna watendaji wazuri ambao wapo wa kizalendo kwa ajili ya kuisaidia nchi yao. Yanaweza yakazungumzwa maneno mengi kwamba mara wanafanya hivi wanafanya hivi. Ndugu zangu palipo na mambo mema ni lazima pawe na maneno mabaya ili kutukatisha tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ninawaomba tusikatishwe tamaa na maneno, tukianza kukatishwa tamaa na maneno hatutafika mbali. Mimi nawaomba watendaji waendelee na kazi wafanye kazi na tupo na Mheshimiwa Kakoso Mwenyekiti wa Kamati yetu anajua kutupanga na kutuambia mambo yote ambayo yanafanyika, tunataka tukushukuru sana Mheshimiwa Kakoso kwa kuhakikisha unawalinda hata hawa ndugu zetu wanaofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu nishauri kwenye SGR, kuna kipande pale cha Kilosa kwenda Mikumi kile kipande naomba kiunganishwe, lakini kwa nini naomba kiunganishwe? Kwa sababu pale ndipo ambapo SGR ina uwezo wa kuungana na TAZARA na TAZARA ikiungana na SGR mizigo ni rahisi kupelekwa kila sehemu mzigo unaotoka TAZARA ukaja SGR na unaotoka SGR ukaingia TAZARA sasa nataka niseme pamoja na hayo niombe tu barabara yetu ya kutoka pale Iringa ilivyojengwa imeshaanza kuharibika na kama inaharibika najua tatizo liko wapi.

Mheshimiwa Spika, tatizo lipo kwa wasimamizi wetu, sasa naomba tunapojenga kuanzia Igawa kuelekea Mbeya hadi Songwe isiwe hivyo tena, tujenge barabara ya maana ambayo itakuwa imestahimili na inaweza pia kupitisha mzigo mkubwa.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba tu niseme tumefika hatua ambayo tunahitaji kuijenga nchi yetu kizalendo na kuipigania, tukiacha kuipigania nchi yetu hakuna mtu mwingine ambaye atasimama kuipigania nchi hii, nchi hii ni yetu sisi sote na Tanzania ni yetu wote na Rais ni wetu wote. Tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, tumefikia hatua pia ya kuhakikisha kwamba Mbeya yetu inakwenda kuwa ya kisasa. Tunaenda kujenga barabara ya njia mbili pale mjini sasa nikuhakikishie tu kama tulikuwa tuna wasiwasi tayari imeshawekwa kwenye bajeti ya mwaka kuu na inakwenda kujengwa na tayari Waziri ameshathibitisha hawezi kutuangusha, ninakuombea Waziri wetu na ninataka niseme mimi nitalinda shilingi yako mpaka tuhakikishe barabara zile zinajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii Mungu akubariki sana na naunga nkono hoja. (Makofi)