Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu kwa niaba ya wananchi wa Vunjo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara ya kwanza nachangia kwenye Mkutano huu wa Bunge, nipende tu kusema kwamba haki ya kuwa na fikra tofauti na mwenzio ni haki ya msingi, ni haki ya kuzaliwa, ni haki ya Kikatiba na tusijengeane chuki binafsi kwa sababu hizi ni kazi za Watanzania tu tunazifanya. Masuala ya chuki binafsi hayana nafasi hapa tunapita tu na Tanzania ina umri mrefu kuliko sisi binadamu. Kwa hiyo, kujengeana chuki binafsi hapa siyo jambo la kheri wala halitatujengea mambo yote ya udugu wetu na mambo ya msingi kwa maslahi binafsi ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wajibu wa Bunge letu ni kuisimamia na kuishauri Serikali. Wajibu wa Bunge letu kwa niaba ya wananchi kwa kuwa wananchi ndiyo walipa kodi na rasilimali za Taifa zinazotumika na Serikali, tunasimamia Serikali kwa niaba ya wananchi na kuna kanuni inayosema hakuna haja ya kulipa kodi kama hakuna uwakilishi (no taxation, no representation). Sisi Wabunge tukiwa ndani ya Bunge hili, tukiwa tunasema mambo hata kama hayapendezi lakini mgongano wa fikra unaleta tija. Hata mwanasayansi mmoja Isaac Newton katika kanuni yake ya tatu anasema katika kila kani mkabala kuna kani iliyo mrejeo sawa na kinyume. Tukiwa na mawazo mapana Serikali hii ya Awamu ya Tano itafanya kazi yake vizuri ya kuhudumia Watanzania kwa maslahi mapana ya wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na usafirishaji, hii Tanzania ni kubwa. Afrika Mashariki kabla haijaingia Sudan ya Kusini, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi ni asilimia 48 tu ya eneo lote la Afrika Mashariki, Tanzania ina eneo la kijiografia zaidi ya asilimia 52. Katika hali hiyo tufanyeje? Lazima tukubali kwenye vipaumbele tuanze kuwekeza kutokana na kasi ya mabadiliko ya sayansi ya teknolojia duniani na suala la kuunganisha bandari zetu na reli na hasa reli ya kati ambayo ndiyo lango kuu la uchumi na kuwa na reli ya kisasa (standard gauge), hili sio suala tena la kupiga danadana. Suala la Serikali kutumia resource zake kwenye bajeti hii shilingi trilioni moja kujenga standard gauge labda ungesema ni upembuzi yakinifu na mambo mengine. Dunia ya leo nenda hata Marekani, nenda Ulaya, Mheshimiwa Waziri ametembea na anaijua dunia na ningependekeza hata Kamati mbalimbali za Bunge ziende nje ya Tanzania wakapate exposure ili waweze kuishauri vizuri Serikali, tuone wenzetu duniani wanafanyaje, wakiwekeza kwenye akili ya mwanadamu mambo mengine yote yanaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri suala la reli ya kati Serikali ikope na hii kazi ifanyike ndani ya mwaka mmoja, miaka miwili au mitatu suala hili tuachane nalo tufanye mambo mengine makubwa zaidi. Tukisema tunatafuta resource zetu wenyewe hatuwezi tukajenga hii reli ya kati. Angalia wenzetu wa Kenya wameshaanza kuanzia Mombasa, wameshafika Nakuru, Naivasha sasa wanakimbilia Nairobi wakiwa na lane hii moja ya reli sisi bado tunapiga danadana ya maneno tu, mara ratili kumi, mara ratili pound ngapi hapana hatuwezi tukafika huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, bandari zetu tulizonazo, jana kwenye maoni ya Upinzani nilizungumzia kuhusu Bandari ya Mtwara nayo ikapewa kipaumbele chake ukilinganisha na Bandari ya Dar es Salaam.
Tumezungumzia masuala ya malori zaidi ya 5,000 mpaka 6,000 kwa mwezi pale Kurasini ni suala la kufanya maamuzi tu Bandari ya Kavu ya Soga ipo pale fanya maamuzi, mwekezaji yupo tunasonga mbele lakini ni danadana mwakani tunarudia kwenye maneno hayo hayo hatuna nafasi ya kufanya mambo ya namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara zetu, sisi Wabunge wakati tunatoka Dar es Salaam tunaona eneo la Chalinze lilivyoharibika, ni matuta matupu. Eneo lile anatoka Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na amejenga barabara nyingi tu ndani ya Taifa hili tunasemea vitu gani vya ajabu hapa? Angalia barabara za Gairo hapo, tupo kwenye hali gani na tunapita sote pale tunaona. Kwa nini barabara hizi zinaharibika kiasi hicho? Ni kwamba zaidi ya asilimia 99.43 ya usafirishaji wetu wa mizigo unatumia barabara. Sasa tunafanya mambo ya vicious cycle of poverty, unazunguka pale pale barabara, barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wengine wanasema bandua lami weka lami, kuna suala la classification theory! Labda niwaombe watu wa TANROADS na Wahandisi na ikupendeze Mheshimiwa Waziri Wabunge tupewe semina kuhusu ujenzi wa barabara unakuwaje ili tuwe na fikra pana za kuweza kutoa michango yetu iweze ikasaidia vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ijikite kwenye kutoa huduma za elimu, afya, maji, haki, mahakama na nyinginezo lakini masuala ya ujenzi wa barabara, ujenzi wa reli na bandari duniani leo ni suala la kutafuta wawekezaji, ni sekta binafsi inapewa kipaumbele katika maeneo haya. Serikali tena mnaanza kurudi kule ambapo tumeshatoka tutakuwa tunapiga danadana tu.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge tunamchanganya hata Waziri. Jana hapa Mbunge mmoja alitoa mchango kuhusu reli akashangiliwa sana, mwingine akasema kuhusu viwanja vya ndege akashangiliwa sana, sasa Waziri achukue lipi, awekeze kwenye reli au awekeze kwenye viwanja vya ndege au basi tu tunafanya kama ngoma za kuigiza hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri TANROADS kwamba maji ni adui mkubwa wa barabara. Tulivyofundishwa masuala ya asphalt na bitumen kwenye ujenzi wa barabara maji ni adui mkubwa wa barabara. Sasa Serikali kuu inashirikianaje na Serikali za mitaa ili TANROADS kwa kushirikiana na Halmashauri kuona namna gani tunaishirikisha jamii ili tuweze kufungua mitaro yetu vizuri, kuwa na kilimo cha matuta, kilimo cha kingamaji, hasa maeneo ya miinuko ili iweze ikawa ni shirikishi kwa wote, la si hivyo hili tunalofanya hapa barabara zetu zinaharibika kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee nimpongeze Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kazi nzuri anayoifanya na unyenyekevu na upole wake na tarehe 13 tulishiriki naye kwenye kongamano la pamoja la namna ya kujikinga na maafa (risk management) katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Wataalamu wetu wakati mwingine tunawalaumu kutokana na mashinikizo tunayowapa sisi viongozi wa kisiasa halafu wanashindwa kufanya kazi zao vizuri. TANROADS kusema ukweli wanafanya kazi nzuri kuna wachache hawafanyi kazi vizuri, sasa wale wachache wasifanye wale wengi wakalaumiwa bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mawasilianio, kodi zisizotabirika, sisi ni wa pili baada ya Gabon kwa kodi nyingi na zisizotabirika kwenye sekta ya mawasiliano hasa kwenye sekta ya simu. Tuwe na mifumo endelevu na mipana ya miaka zaidi ya 100 ijayo ili tuweze kuhakikisha kwamba Tanzania tunayoihitaji ya miaka 150 ijayo inakuwaje, tuweze kushindana na wenzetu duniani. Tusipofanya hivyo tutakuwa hata kwenye ukanda wa Afrika Mashariki tutakuwa nyuma. Kwa mfano Bandari ya Dar es Salaam ndiyo inashika mkia katika ukanda wa Afrika Mashariki, tusijilinganishe na tunachopata sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naomba zile barabara za ahadi za Rais ziweze kupewa kipaumbele, ahsante sana.