Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uzima na afya njema hata tumepata kufika kuiona siku ya leo. Nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kumwongoza vema Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na leo hii anafanya kazi iliyotukuka katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru Mungu pia kwa jinsi Mawaziri wanavyofanya kazi vizuri, Mawaziri wote, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wengine. Lakini kipekee sana niwashukuru baadhi ya Mawaziri ambao walifika Jimboni kwangu, nikianzia na kaka Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, ulinyeshewa sana na mvua kipindi kile! Pia Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, pamoja na Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, tunawashukuru sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nichangie kama ifuatavyo:-
Nikianza na suala la uwanja wa ndege wa Songwe, uwanja huu umejengwa zaidi ya miaka 14 sasa, tangu ambapo ulipendekezwa, tunashukuru Serikali ilipofikia, lakini bado unahitaji kuboreshwa zaidi! Uwanja huu ni muhimu sana kwa sababu unaunganisha Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini iwe Mbeya, Njombe, Katavi, Rukwa na Ruvuma, tunautumia uwanja huu wa Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja huu wa Songwe, nilikuwa nasoma kwenye vitabu umetengewa shilingi bilioni 10, lakini bilioni 10 hii naamini kwa suala la kujenga taa pamoja na kujenga ujenzi kwa maana ya fence, hakika Mheshimiwa Waziri hazitatosha kwa bajeti ambayo imetengwa pale! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini uwanja huu utakapojengwa, utafungua fursa nyingi sana za kiuchumi Nyanda za Juu Kusini. Wawekezaji wengi sana ambao wamekuja ili wawekeze, lakini wanasema hatuwezi kusafirisha mizigo kutoka Mbeya, ama kutoka Songwe, ama kutoka Njombe mpaka kwenda Dar es Salaam halafu ndipo iende Ulaya, wanataka ndege Emirates zitoke huko ziende moja kwa moja Mkoani Mbeya kwa ajili ya kuchukua hizo raw products na pia ziweze kuwa processed. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia uwanja huu ni muhimu kwa sababu kuna baadhi ya viwanda ambavyo vilikwishaanzishwa pale, vinashindwa kuendelea kwa sababu hakuna njia madhubuti; ukiangalia TAZARA, nayo haifanyi vizuri. Kwa hiyo, tunaomba uwanja huu uweze kukamilika kwa wakati ili uweze kufungua fursa nyingi za kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika suala la barabara, suala la barabara kwa Jimbo langu la Busokelo ni changamoto kubwa sana. Nakumbuka kuna barabara ambayo iliahidiwa ni zaidi ya miaka 12 sasa inasemwa itajengwa kwa kiwango cha lami. Nikichukua kitabu cha Ilani ya Chama chetu ukurasa wa 49, hii ni Ilani ya Chama mwaka 2015 imeandikwa ile barabara pale kwamba Katumba – Mbambo - Tukuyu, kilomita 80 kwa kiwango cha lami, lakini kwa miaka yote hiyo hata hivi ninavyoongea, nakumbuka nilishawahi kuleta swali na Mheshimiwa Naibu Waziri, alilijibu kwamba ifikapo mwaka huu mwezi Septemba ama Oktoba itakuwa imekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tukija katika bajeti ukifungua ule ukurasa wa 243, imeandikwa upgrading to DSD of Katumba-Lwangwa- Mbambo- Tukuyu road kilometa 83, lakini hapa inaonyesha ni kilometa moja tu! Tunamwomba sana, Mheshimiwa Waziri, barabara hii ni ya enzi na enzi, alikuja Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa aliahidi, lakini alikuja Mzee, Mheshimiwa Dkt. Kikwete aliahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 28 Agosti, 2015 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, saa sita na dakika thelathini mchana aliahidi barabara hii na wananchi walipiga sana makofi wakiamini kwamba itajengwa. Hakika tunawaombeni sana, kwa sababu barabara hii, kule tuna vitu vingi kwanza kuna gesi asilia. Hii gesi asilia, kuna viwanda viwili ambavyo vinafanya extraction na exploration za minerals, lakini zinaharibika kwa sababu barabara haziko imara!
Mheshimiwa Naibu Spika, si gesi asilia tu, kuna suala zima la geothermal, karibu tutaanza kuchimba, umeme wa kutumia joto ardhi pia unatoka kule! Nakumbuka alipokuja Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo yeye mwenyewe alijionea ile barabara hadi akauliza Mheshimiwa Mbunge hapa vipi, nikasema na mimi nitalia kilio kwa Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu ili aweze kutuwezesha kwa barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hivyo tu, hivi ninavyoongea Mheshimiwa Waziri, barabara ile nilipita mwezi wa nne hakika ilikuwa ni worse, worse, worse, nusura nipate ajali! Watano walikufa kwa sababu ya mvua ambazo zimenyesha sana kipindi hiki. Kwa hiyo, tunaomba mtukumbuke, mtukumbuke kwa maana ya kwamba, sehemu ambapo ilitakiwa tusafiri umbali wa kilometa pengine 20 inatulazimu tuzunguke sana. Kama mnakumbuka kipindi ambacho kumetokea mafuriko ya kule Kyela, watu wa Kyela wanalazimika kupita Ipinda, waje Mbambo, waje Masoko, waje Tukuyu wanatumia barabara hii na ndiyo kiunganishi pekee cha Halmashauri zote tatu, maana yake Halmashauri ya Rungwe, Wilaya ya Rungwe, Busokelo na Kyela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaombeni sana na si hivyo tu, ni zaidi ya tani 20 kama si 30 zimeharibika wiki mbili zimepita kwa sababu ya barabara kutopitika, kwa maana ya kwamba malori yameweza kuzuia njia na hakuna abiria anayeweza kupita pale na utelezi ni mkali sana. Kwa hiyo, wananchi ambao wanalima wanashindwa kwenda kupeleka mazao yao kwenda mjini kwa sababu hakuna magari yanayokwenda kule kuchukua bidhaa zao, kwa hiyo tunawaombeni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini siyo hivyo tu, kuna suala zima la madaraja. Madaraja ni changamoto kubwa, ni changamoto kubwa kwa sababu sasa mvua zilivyonyesha zimesababisha baadhi ya madaraja hayo kuondoka, kwa maana ya kwamba wananchi wanatumia tunaita madaraja utepe. Sasa baadhi ya wanafunzi hawawezi kwenda ng‟ambo ya pili ya mto kwenda kusoma kwa sababu hawawezi kuning‟inia kwenye zile nyaya ama zile kamba ambazo zimewekwa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kama kuna emergency plan yoyote iweze kutusaidia ili haya madaraja yaweze kujengwa hasahasa daraja la Nsanga. Halafu kuna daraja ambalo lipo Kata ya Kisiba ambalo linaitwa Kibundugulu, hii Kibundugulu imesababisha hata kwenye mitandao, ambao mna WhatsApp, baadhi ya akinamama wanatembea juu ya kamba, inasikitisha sana! Kwa mfano, kama huyo mama ni mjamzito kwa vyovyote vile hawezi kuvuka pale kwa sababu inahitaji apite mmoja baada ya mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaombeni sana Wizara hii kupitia Wizara ya Miundombinu mtusaidie kutengeneza hata emergency, wakati bado tunaendelea kusubiri hiyo long plan kwa ajili ya kutusaidia kujenga madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hayo, pia kuna suala hili la mitandao ya simu; mitandao ya simu ina-diverge sana kulipa kodi na kwa bahati mbaya sana pengine sijui tuna mtambo ama hatuna mtambo, lakini ni muhimu kupitia TCRA wawe na mtambo ambao unaweza uka-filter ama ukajua ni kiwango gani cha course ambazo kila siku zinaingia na kiwango gani cha mapato hata kama ni hizi M-pesa, Tigo pesa ili Serikali ipate mrabaha wake sawasawa, iwezekanavyo. Kwa maana hiyo basi, ni muhimu kuanzisha mitambo kama nchi zingine ambapo inarahisisha sana kutokuwa katika quarrels na Serikali kwa maana ya kufuatilia masuala ya kodi, mara hapa, mara pale, wewe unaingia tu kwenye system unajua bwana wewe umefanya hivi na hivi then lipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsanteni sana!