Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nichangie katika mjadala huu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara nyeti, Wizara ambayo ndiyo moyo wa uchumi wa nchi yoyote duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako naomba nisome tu Ilani ya Chama chetu Chama cha Mapinduzi, kipande kidogo tu, paragraph moja. “Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, 2015, kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wabunge wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani, imeandaliwa ikiwa ni mkataba kati ya CCM na wananchi.” Niishie hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma ilani hii kuweka msisitizo jinsi tulivyoji-commit tukiwemo sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwa wananchi wetu waliotuamini hususan katika suala hili la miundombinu. Katika ilani hii, ukurasa wa 57 umetaja kwa msisitizo mkubwa sana, barabara ya kutoka Mkiwa, Itigi, Rungwa hadi Makongorosi, kilomita 413 ikiamini na kuwatilia uzito wananchi waamini kwamba wakichagua Chama cha Mapinduzi, barabara hii itajengwa katika kipindi cha ilani hii cha miaka mitano; yaani 2015 - 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii imekuwa ikizungumziwa na Wabunge wanaotoka katika Jimbo ninalotoka mimi sasa na Wabunge hawa wakitokana na hiki Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Ismail Iwvata lakini Mheshimiwa John Paul Lwanji ambaye nimempokea kijiti. Inawezekana ikawa sababu ya yeye kutokurudi humu barabara hii ikawa na mchango mkubwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu sasa kidogo inaonekana Serikali hii sikivu ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais ambaye alikuwa ametokana na Wizara hii, Waziri aliyempokea ameonesha alama ndogo kuonesha kwamba sasa barabara hii itajengwa kwa kilomita 35 kutoka Mkiwa hadi Itigi na kupita kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ilani hii, miaka mitano imesema kwamba barabara hii itakuwa imejengwa kwa kiwango cha lami. Kilomita 413, Jimbo langu peke yake kuna kilomita 200. Barabara hii imekuwa ikijengwa miaka ya nyuma kutokea Mkoa wa Mbeya, kuna kilomita 36 zimejengwa kilomita 36 tena na mwaka huu zinajengwa kilomita 43. Upande wa Mkoa wa Singida ambapo Jimbo langu limo, ndiyo kwanza wameanza na kilomita 35. Nakushukuru sana Profesa Mbarawa kwa kuanza hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hesabu ndogo tu ambayo haihitaji sana kwenda kwenye vyuo kusomea hesabu hii kwamba 200 ukigawa kwa 35 unapata ngapi? Kwa maana kwa mpango huu wa 35, barabara hii itajengwa kwa zaidi ya miaka saba na kama kila mwaka watajenga kilomita 35, ilani hii itakuwa imeleta shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuona na kuanza kujenga barabara hii lakini niombe sasa; kama tuna dhamira ya kweli ya kutekeleleza ilani tuliyoiahidi, Mheshimiwa Rais wetu wakati akiwa katika ziara yake ya kutafuta kura katika Jimbo langu, moja ya sehemu ya hotuba yake ambapo wananchi walipiga makofi ni pale alipozungumzia kwamba sasa anajenga barabara hii katika kipindi chake cha miaka mitano ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilomita 35 mara tano maana yake, hataweza kufika hata nusu ya hii barabara. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri, aoneshe msisitizo kwamba ile ahadi ya Mheshimiwa Rais, basi anaitimiza, aongeze japo 35 nyingine, ikifika mara tano at least tutakuwa tumesogea kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni ndefu na inapita katika Vijiji vya Gurungu, Sanjaranda, Songambele, Majengo, Itigi Mjini, Doroto, Lulanga, Itagata, Ukimbwi, Chabutwa, Mtakuja, Mitundu na Kalangali. Katika Wilaya ya Sikonge kuna Vijiji vya Kiyombo, Kirumbi na Mwamaluku; wakati inakuja tena katika Jimbo langu, Vijiji vya Mwamagembe, Kintanula na Rungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri atuongezee, awape thamani wananchi ambao wamekuwa wakikichagua chama hiki toka uhuru, hawana mpango wa kubadilisha mawazo, tusiwape fikra mbaya wananchi waaminifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naombe sasa niongelee barabara nyingine ambayo tumejengewa pale kutoka Manyoni, kupita Itigi, hadi Chaya. Naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kujenga barabara hii ya kilomita 89.3; imekwisha lakini kuna shida pembeni mitaro ya kupitisha maji ya mvua haiko vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema ikamaliziwa barabara hii kutoka Chaya kwenda Nyahuwa ili tuwaunganishe wananchi wa Mkoa wa Singida na Mkoa wa Tabora. Tukiijenga barabara hii itakuwa na tija sana kiuchumi kwa wananchi wa Mikoa ya Kati lakini Mkoa wa Tabora kusafirisha mazao yao kuleta katika masoko ya Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la shida kidogo ya mitandao katika baadhi ya maeneo yangu katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi; katika vijiji vichache tu, Mheshimiwa Waziri akitusaidia watu wa mitandao wakatufikia katika Kijiji cha Idodiyandole na Kijiji cha Mbugani na Ipanga Masasi, tutakuwa tumemaliza tatizo hili la mawasiliano na wananchi wangu watakuwa katika dunia ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna shida kidogo ya usikivu wa redio katika masafa ya FM katika maeneo yale. Hawa watu wa mawasiliano kila nikiwasiliana nao wanasukumiana; huyu wa Habari, huyu wa Mawasiliano. Serikali ni moja naomba tusaidiwe kama ni busta, pale kuna redio yetu ya Wamisionari ya St. Gaspar pale wanaitwa Redio Mwangaza wameweka busta yao, sasa redio kubwa kama ya Taifa bado haisikiki. Tunaomba Serikali itusaidie hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la service levy pia za minara zimekuwa ni shida zimekuwa kidogo kidogo sana; minara hii ambayo inajengwa hasa na hallotel. Makampuni yale mengine wanatulipa vizuri, kuna shida tu katika jinsi ya kupata malipo, lakini ukipata malipo yao yanatosheleza. Naomba sasa Serikali itusaidie, vijiji ambavyo minara ya Hallotel imewekwa na tunatumia simu zao na tumekuwa ni wateja wakubwa, basi nao walipe levy vizuri, vijiji vyetu navyo vinufaike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kupigiwa kengele, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, basi Waheshimiwa Mawaziri watuangalie, ahsante sana.