Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kusema na kwa sababu katika Bunge hili ni mara yangu ya kwanza kuzungumza. Nataka niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Newala Mjini kwa kunirejesha tena katika jengo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mengi ya kusema kabla sijaenda mbali. Nikiwa ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Klabu ya Yanga nataka kuipongeza klabu yangu ya Yanga kwa kuchukua ubingwa. Vijana wetu tunawapongeza, mmefanya yale tuliyowatuma mfanye, tunataka mfanye hivyo na nchi za nje pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mimi nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza maraisi waliotokana na Chama changu kwa kushinda uchaguzi. Tupo awamu ya tano ya maraisi, na faraja niliyonayo kwamba wote waliopokezana vijiti wametoka Chama cha Mapinduzi.
Nampongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kushinda, nampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, naipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais, Mabaraza ya Mawaziri yote ya Muungano na lile la Baraza la Mapinduzi Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna kazi moja tu ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi, pamoja na Waheshimiwa Mawaziri chapeni kazi. Ukimsikia mtu anakuambia mnakwenda kasi muulize nilipoapishwa niliambiwa niende speed gani? Kwa hiyo, mimi nataka kupongeza sana. Lakini wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. (Makofi)
Ndugu zangu uongozi wa nchi ni kupokezana. Kabla ya Magufuli tulikuwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kafanya mambo mengi nchi hii. Mimi nataka niwape mfano ambao ni my personal experience.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimaliza shule form four mwaka1967 wengi mlikuwa hamjazaliwa. Shule inaitwa St. Joseph College Chidya, nikapelekwa kwenda Ilboru, kwa sababu ya matatizo ya mawasiliano ya Mtwara na Arusha mimi nilikuwa natembea wiki nzima kwa gari katika barabara ya vumbi kutoka Newala, Nachingwea, Tunduru, Songea, Njombe, Iringa, Morogoro nikifika Chalinze napanda basi kwenda Arusha; wiki nzima niko njiani, hatukuwa na barabara ya lami. Akaja Mzee Mwinyi akatuanzishia daraja, Mzee Mkapa akatujengea daraja, Jakaya akatuwekea lami. Leo unatoka Newala kwa gari saa nane mchana na saa mbili jioni upo Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya kazi nzuri, ametuwekea sekondari kila kata, amejenga barabara za lami nchi hii, kama ilikuwa ni kushindana ndiye anayeongoza kwa kujenga barabara za lami nyingi kuliko waliomtangulia. Kigoma mlikuwa mnalalamika tupo gizani, ameondoa tatizo la umeme, amewawekea daraja mto Malagarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwanza tunampongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ameiongoza nchi salama miaka kumi amemaliza, kijiti amemkabidhi Mheshimiwa John Pombe Magufuli, sasa sikilizeni kazi ya Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya miezi sita tu vijana wanasoma bure toka fstandard one mpaka form four, ndani ya miezi tu. Ndani ya miezi sita amesema ile Mahakama ya Ufisadi mliyokuwa mnaidai tarehe 01 mwezi Julai inaanza. Miezi sita bado…
(Hapa baadhi Wabunge walizungumza bila kutumia vipaza sauti)
Mtu mzima naongea mambo ya kuzomea zomea wakati hujaruhusiwa, mtu mzima anaongea. Mimi nilidhani mnawafanyia vijana wenzenu hata mimi size ya mzee wenu? (Makofi)
MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hii disturbance iliyotokea utaniongezea muda. (Makofi/Kicheko)
Kwa hiyo nasema nchi ipo salama. Ametoka Rais wa CCM amemkabidhi kijiti Rais wa CCM, ilani ya uchaguzi iliyokuwa inatekelezwa sasa Mheshimiwa John Pombe Magufuli amechukua pale alipoacha Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ndiyo maana nchi ipo shwari, haijashikwa na watu wababaishaji, imeshikwa na watu makini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kusema hayo niseme mengine. Kwanza nataka niombe sana Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ana nia nzuri na nchi hii, Mawaziri wake wana nia nzuri na nchi hii, hebu tuwape ushirikiano ili Tanzania pawe mahala pazuri pa kuishi. Mbona kila nchi nje huko wanatupongeza? Wanawashangaeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kusema hayo nataka kwenda kwenye barabara. Nataka niishukuru Serikali yangu ya CCM Serikali sikivu, watu wa Mtwara tumeomba barabara ya lami kutoka Mtwara – Tandahimba – Newala – Masasi. Hotuba ya Waziri inasema bajeti ya mwaka huu kuanzia tarehe 1 Julai, 2016 barabara inajengwa. Naomba watu wa Tandahimba, Newala, Masasi, Mtwara, kazi mliyotutuma tumeifanya majibu ya Serikali ndio hayo, barabara itajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili barabara ya mkoa. Mheshimiwa Waziri Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mtwara tumeomba barabara ya mkoa kutoka Newala – Nyambe – Ndanda ichukuliwe na mkoa kwa sababu, watu wa Tandahimba na Newala Hospitali yetu ya Rufaa ni Ndanda. Tunaomba ombi hilo lichukuliwe barabara iwe ya mkoa ili iweze kutengenezwa vizuri kwa sababu, Halmashauri zetu uwezo umekuwa mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Newala tulikuwa na uwanja wa ndege ambao umetumika sana wakati wa vita vya Msumbiji. Bahati mbaya nyumba zimejengwa karibu sana mpaka uwanja wa ndege ule umefutwa, lakini Halmashauri imeomba ipewe barua rasmi ya kuufuta uwanja wa ndege wa Newala, hilo jambo halijafanyika, tunaomba lifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, Wilaya tumetafuta eneo la kuweka uwanja wa ndege, Waziri uliwatuma wataalam kuja kuona, wametuambia shughuli gani tufanye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba suala la ujenzi wa uwanja wa ndege Newala, utakapokuwa unajibu, watu waliozoea kuwa na uwanja wa ndege tangu enzi ya mkoloni sasa inapokuwa hatuna uwanja wa ndege tumerudi nyuma. Tutapenda kusikia kauli ya Serikali kuhusu lini mnaanza kujenga uwanja wa ndege wa Newala, lakini kwa hatua za awali tunaomba wale watu wafidiwe eneo lile mlichukue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Newala tuko mpakani na Mto Ruvuma; nimeona hapa hotuba kivuko hapa, kivuko hapa, sisi tuna mawasiliano ya karibu sana na Msumbiji. Kuna daraja kule la Umoja, kuna daraja la Kilambo, lakini Tandahimba na Newala pale tuna vivuko vingi na nafikiri ndio tunaingiliana zaidi na watu wa Msumbiji kwa sababu ya kupakana, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri, Wizara iangalie uwezekano wa kutuwekea kivuko katika Mto Ruvuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko barabara inaitwa barabara ya Ulinzi, hii ni barabara inatoka Mtwara inaambaa ambaa kandokando ya Mto Ruvuma mpaka Tunduru mpaka mkoa wa Ruvuma. Barabara hii haijatengenezwa miaka yote na Serikali kuu, muda mrefu mmeaicha kuitengeneza, tunapata tabu kusomba korosho kwa sababu ya hali ya barabara na korosho za Mtwara nyingi zinatoka katika bonde la Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nilikuletea barua, bado uko mgeni Wizarani kwamba, vijiji vya bonde la Ruvuma Wilaya yangu ya Newala, hawana mawasiliano ya simu. Walikuwa wanatumia simu za Msumbiji ambazo dakika moja tu shilingi 1,000, lakini haraka haraka ulituma watu wako, watu wa Halotel wakaja, bonde la Ruvuma leo Halotel ni Halotel kweli kweli. Tatizo lile la watu wa Newala, watu wa Tandahimba kutumia simu za Msumbiji umetuondolea tuko ndani ya Halotel ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Waziri, mimi nataka nikushukuru sana kwa uharaka wako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nakushukuru, lakini kwa kumalizia uwanja wa ndege wa Mtwara uwe uwanja wa Kimataifa wa Mtwara. Ninakushukuru.