Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. IDD K. IDD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza kabisa, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia leo kupata nafasi ya kuchangia bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kaka yangu Mwigulu Nchemba kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya pamoja na Naibu wake Waziri naye ameendelea kufanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka kujikita kwenye mambo machache sana. Moja, niendelee kuipongeza sana Serikali kwa bajeti hii ambayo imeileta hapa mezani. Ni bajeti nzuri, ni ambayo kama itaenda kutekelezeka kwa asilimia mia moja, basi italeta matunda makubwa sana kwenye maeneo yetu. Nimeona Wizara ya Nishati imeweza kuweka nguvu kubwa katika kuhakikisha kwamba inapeleka umeme kwenye maeneo yetu. Sasa niombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kutoa support kubwa sana kuhakikisha kwamba anapeleka fedha kuwalipa wakandarasi ili waweze sasa kuona namna gani wanaweza kuendelea na kazi ili ifanyike haraka sana ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya vijiji vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifanyike hivyo hivyo kwenye barabara na niombe sana Waziri wa Ujenzi, Jimbo la Msalala lina barabara moja ambayo tayari inafadhiliwa na Mgodi wa Barrick na niwapongeze sana Barrick kwa kuendelea kuonyesha jitihada za kuhakikisha kwamba wanatoa ushirikiano kwa Serikali ili kuona namna ya kujenga barabara hiyo. Niombe sana kwa Waziri wa Ujenzi, waone namna gani ambayo wanaweza wakapeleka mchakato huu haraka ili ikiwezekana basi mwezi unaokuja barabara hii ianze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii imekuwa ni barabara ambayo ina kero kubwa sana. Watu wanapata ajali nyingi, magari yanadondoka na hasa magari yanayobeba mizigo mikubwa. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Waziri wa Ujenzi waweze kuharakisha mchakato huu ili barabara hii ianze kujengwa, kwa sababu fedha zipo kila kitu kipo tunasubiri tu mchakato ukamilike ili barabara ianze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo kwenye barabara zingine ambazo zimetajwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, basi ni vyema pia Mheshimiwa Waziri baada ya hapo kwenye bajeti ya mwaka unaoanza akapeleka fedha mapema ili barabara hizi ziweze kujengwa, zirahisishe kujenga uchumi wa maeneo yetu hasa katika Jimbo la Msalala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie mambo mawili. Jambo la kwanza nataka nizungumzie habari ya oil ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kwenye nchi yetu hii ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu Mheshimiwa Waziri wa Nishati, kaka yangu January Makamba amekuwa akizungumzia sana habari ya mafuta na pia akaacha kuzungumzia habari ya oil ambayo pia inatumika katika maeneo mengi sana. Sisi tunatumia kwa ajili ya magari na vyombo vya moto vyote. Sasa kumekuwa na changamoto, nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Waziri kwamba makubaliano ambayo huwa wanaaingia pamoja na Nchi za Afrika Mashariki katika kuweka ushuru wa malighafi ya oil kuingiza nchini kwa kiwango cha asilimia 10. Hata hivyo, niendelee kuomba sana, makubaliano ambayo huwa wanaingia huko kwenye Nchi za Afrika, wenzetu wanakuja kurekebisha kodi mbalimbali za ndani kuhakikisha kwamba wanajenga mazingira ya uwekezaji mzuri kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye suala zima la oil, aende akafanye mabadiliko, afute VAT na apunguze kodi mbalimbali zitakazowezesha wananchi kuingiza malighafi ya oil ili waweze kuwekeza viwanda vingi na tuweze kuzalisha oil hapa hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwani utaona kabisa kwamba kwa sasa hali ilivyo ni rahisi kununua oil katika nchi zingine, nchi za Jirani kwa sababu oil ni bei rahisi kuliko kununua oil hapa nchini hii. Hii inasababishwa na kuweka kodi mbalimbali kwenye malighafi ambayo inakuja hapa kwenye viwanda vyetu ambayo itazalisha oil hiyo. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, aende akakae, aangalie kama inawezekana wapunguze hiyo gharama ya kuingiza/kutoza malighafi ambazo zinakuja kuzalisha oil kwenye viwanda vyetu hivi vya ndani. Hii itasaidia kuhakikisha kwamba wananchi sasa wanaenda kuwekeza kwenye sekta ya kutengeneza oil.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye suala zima la Jimboni ambalo wananchi wa Msalala wamenituma na hasa kwenye Sekta ya Madini. Mheshimiwa Waziri hapa naomba anisikilize vizuri sana, kuna jambo linaendelea la asilimia mbili kwa wachimbaji wadogo wadogo. Niombe sana, asilimia mbili hii nimehudhuria semina mbalimbali za watu wa Waziri wa TRA, wakitoa ufafanuzi juu ya asilimia mbili kwa wachimbaji. Mheshimiwa Waziri ameweka asilimia mbili kuanzia mchimbaji yeyote yule mwenye mapato ya kuanzia zero mpaka milioni mia ndiyo atayehusika na kulipa asilimia mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, kama hataweka mfumo mzuri, wachimbaji wadogo wadogo mitaji yao inaanzia milioni mia na kuendelea juu. Sasa niombe kama tutaenda kupitisha hii asilimia mbili kwa wachimbaji wadogo wadogo, basi tuongeze kutoka kipato cha asilimia zero kwenda mpaka bilioni tano kwa sababu uchimbaji wa madini si kama biashara nyingine. Uchimbaji unaanzia kwenye mtaji mdogo sana, ni milioni mia moja kwenda juu. Kwa hiyo Waziri akisema kwamba mtu atakayechajiwa asilimia mbili ni kuanzia zero mpaka mia moja, maana analenga wale wachimbaji wadogo wadogo akinamama ambao wanaenda kuokota mifuko michache na kwenda kuchoma kupata gramu mbili, tatu kwa ajili ya kuendesha maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, hii asilimia mbili haiendi kumsaidia mchimbaji mdogo mdogo isipokuwa waje na mfumo, waweke utaratibu mzuri wa kwenda kuona ni namna gani wanaweza kuwajengea mfumo mzuri wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kutunza hesabu zao na waweke mfumo mzuri kuona namna gani wanaweza kukubaliana na matumizi ambayo yanafanyika kwenye maeneo yale, kwa sababu kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo ni nadra sana kumkuta mama ambaye anauza maji ana risiti, ni nadra sana kumkuta mtu ambaye anauza matimba ya kufunga mle ndani ana risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashauri TRA na Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakae na timu yake waangalie ni namna gani sasa wanaweza kuweka mfumo mzuri utakaomwezesha mchimbaji mdogo anapokuja kufunga hesabu zake kwa mwaka, baadhi ya matumizi wayakubali. Kwa hiyo wafanye research, waje na utaratibu huo, lakini wakisema kwamba mchimbaji mdogo mdogo alipe asilimia mbili, hii asilimia mbili haiendi kumgusa mchimbaji mdogo mdogo, isipokuwa inaenda kumgusa mama mnyonge kabisa ambaye anaenda kufanya sisi tunaita ukwale, mifuko miwili, mitatu, anaenda kusaga, anapata pointi mbili, gramu mbili ndiyo hii sheria ambayo wameileta ya asilimia mbili inaenda kum–favor, lakini kwa mchimbaji mwingine yeyote yule ile asilimia mbili haiendi kum–favor kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawataweka utaratibu wa namna gani wanaweza kukubaliana na matumizi ili mchimbaji huyu aweze kuweka gharama zake vizuri, itakuwa ni changamoto sana. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, hii asilimia mbili ikiwezekana waende kuipitia upya, waiache kwanza, tukae vizuri kuona namna gani tunajadiliana, ni yupi atakayeweza kunufaika na hii asilimia mbili. Kama mapato yatakuwa ni asilimia zero mpaka bilioni tano tunakubaliana na hii asilimia mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ailete na sisi tutaipitisha, lakini kama ni mapato kuanzia asilimia zero mpaka milioni mia moja, biashara ya dhahabu siyo biashara ya vitumbua. Biashara ya dhahabu mtaji wake duara moja tu gharama yake ni milioni mia tano mpaka bilioni moja. Sasa Waziri akisema asilimia asilimia zero mpaka mia moja, maana yake bado ni changamoto na wachimbaji watakuwa hawajaelewa chochote kile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nizungumzie habari ya leseni. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Doto Biteko, anafanya kazi kubwa sana. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, leo hii utaona wachimbaji walikuwa kupata leseni ni kazi sana, lakini ukisoma Ripoti ya Wizara ya Madini, utaona kabisa wamegawa leseni nyingi kwa wachimbaji. Leo hii tuna uhuru wa kumiliki leseni kwenye maeneo yetu, lakini bado kuna changamoto hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika baadhi ya maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo, kumekuwa na wawekezaji ambao wanatoka nje kuja kuchukua leseni hizi kubwa kwa maana ya prospecting license na leseni hizi hawaziendelezi. Wanapokuja kuchukua maeneo haya, wanatoka hapo baada ya kupatiwa leseni ya prospecting license wanaenda na documents zetu kwenda nje kutafuta mikopo na mikopo ile hairudi kuja kuendeleza leseni zile. Matokeo yake wanachukua zile fedha wanaenda kufanya mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, kuna wachimbaji ambao tayari wapo kwenye maeneo yale, kwangu ukiangalia kuna maeneo ya Nyangalata, kuna maeneo ya Segese na maeneo mengine yote, kuna wachimba wengi ambao wanahitaji kuchimba na wamewekeza kwenye leseni zile za prospecting license, lakini bado hawajapatiwa leseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri aje na mfumo kuhakikisha kwamba wale ambao wanapatiwa leseni za prospecting license hawazifanyii kazi, utaratibu ufanyike ikiwezekana kuwafuta ili wapewe wachimbaji wadogo wadogo waweze kufanya kazi, kwani wachimbaji wadogo wadogo kwa sasa ndiyo wanaochangia mapato makubwa kwenye Sekta hii ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Biteko anapokuja ku-wind up hapa aje na kauli atueleze je, ni vipi sisi wachimbaji wadogo wadogo ambao tuko kwenye maeneo ambayo yameshikiliwa na leseni kubwa na leseni kubwa hizo hazifanyi kazi, namna gani anaenda kuzifuta ili wachimbaji wadogo wadogo tuweze kunufaika na maeneo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)