Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Fedha.

Kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa namna alivyoweza kutupatia fedha nyingi. Pia, kusema kweli kwangu Musoma Mjini kwenye upande wa huduma za jamii sina lawama na Serikali kwa sababu imenipa fedha zaidi ya asilimia 90. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu ukiangalia kwenye upande wa elimu tumepata fedha za kutosha na hata kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa vipo vya kutosha. Vilevile kwa mwaka huu yale makali ya uchangiaji kwa wananchi yamepungua kwa maana hawakuweza kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa afya namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maana ya kwamba tulitoa ombi la sisi kama Manispaa kupewa ile iliyokuwa hospitali ya mkoa na Serikali imekubali. Hata hivyo, kama hiyo haitoshi tulipata fedha milioni 500 tukaomba kwamba walau itumike kujengea uzio wa hospitali hiyo tuliyopewa, Serikali imekubali. Vile vile, tuliendelea kuomba kupata eneo kwenye ile Hospitali ya Rufaa kama hekari 20 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu Serikali imekubali. Kwa upande wa maji Musoma Mjini tuna zaidi ya asilimia 100. Hilo ni pongezi kubwa ambayo tunaendelea kuipa Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, hata kwenye upande wa umeme Serikali imekubali kunipa umeme wa REA katika zile kata za pembezoni. Kwa hiyo, ndio maana leo nasema, leo naendelea kuipongeza sana Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo imeendelea kutupatia fedha kwa ajili ya huduma za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hizo huduma nzuri ambazo tumeendelea kuzipata, bado nina maombi machache. Leo ukizungumza tatizo kubwa kwa wananchi wa Jimbo la Musoma ni uchumi kwa maana ya kwamba mzunguko wa fedha ni mdogo sana. Kwa sababu mzunguko wa fedha ni mdogo sana yako mambo ambayo Serikali imeyafanya lakini bado hayajawasaidia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Serikali imetengeneza Sera nzuri za kuhakikisha kwamba mikopo ya gharama nafuu inawafakiwa wananchi. Pia, mikopo hiyo inatolewa na Benki kama NMB, CRDB, TADB pamoja na TIB. Kwa mfano, Serikali ilisema kwamba fedha hizo zilenge kwenye uvuvi, ufugaji, kilimo pamoja na biashara ndogondogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida iliyopo ni kwamba zile benki au taasisi hizo za fedha sio rafiki kwa ajili ya wale wajasiriamali wadogo. Bado masharti yanayofuatawa ni yale yale ambapo yule mjasiriamali mdogo anahitaji atoe security kwa maana ya hati ya nyumba. Kwa kweli hili sasa linawapa wakati mgumu sana wale wananchi ambao wana uwezo mdogo ambao wanahitaji kuendelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeishauri Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri, waone namna gani tunaweza kuwasaidia wale wananchi wa wadogo, wale Machinga ambao wanahitaji fedha ili waweze kufanya biashara zao. Pia, kwa bahati mbaya sana ushirika mpaka sasa umeshindwa kufanya vizuri na hiyo ndio iliyokuwa njia pekee ambayo ingeweza kuwasaidia wale wafanyabiashara wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu kwa sasa ambalo Serikali ingeendelea kulifanya; kwanza, wamesimamisha hata zile fedha ambazo zilikuwa ni asilimia 10 kwa ajili ya akinamama, vijana pamoja na watu wenye ulemavu ambazo walikuwa wanapata kidogo na sasa Serikali imesimamisha na haijulikani ni lini itaweka utaratibu madhubuti ili wananchi hawa waweze kukopa na fedha hizo ziwasaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, kama hivyo ndivyo, ombi langu ni kwamba, hivi ni kwa nini Mheshimiwa Waziri asitoe fedha tukapeleka kwenye maeneo ya masoko. Kwa mfano pale Musoma, wale watu wangu wa Mwigobero, Soko Kuu, Nyasho na Soko la Saa Nane pamoja na masoko mengine wangeweza kupewa fedha wakaunda aina fulani hivi ya ushirika ambao wangeendelea kuwakopesha wale watu wao ambao ni wafanyabiashara wanaowafahamu na wanazo biashara kwenye yale maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo ingeweza kuwasaidia sana ili na wao wakaendeleza maisha yao kuliko hivi sasa tunasema Serikali imemwaga fedha, imepeleka fedha lakini wale wananchi wenye uwezo wa chini hizo fedha hawazioni. Kwa hiyo, kwenye upande huo bado kwetu kuna tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine, tunaishukuru Serikali kwa kuingia makubaliano na Serikali ya Dubai hasa kwenye maeneo ya Bandari. Ombi langu hapo ni moja tu kwamba, Mheshimiwa Waziri baada ya ile awamu ya kwanza ambayo inahusu Bandari ya Dar es Salaam, basi kwenye awamu ya pili na ile bandari yetu ya Musoma nayo iwekewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumezungumza hata katika ilani kwamba tutajenga reli ya kutoka Arusha kwenda Bandari ya Musoma. Ni matumaini yangu kwamba ukizungumza Musoma iko Karibu sana na Uganda ambako iko mizigo mingi ingependa kwenda Uganda. Kwa sababu ile Bandari ya Musoma imekufa basi na yenyewe tukiwapa hawa wawekezaji na hiyo reli ikijengwa itasaidia sana kuchangamsha uchumi wa Musoma na watu wetu wataendelea kupata ajira. Kwa hiyo, nadhani na hilo nalo mkumbuke kwenye hiyo awamu ya pili itakayofuata, basi na sisi tuweze kuwemo humo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naipongeza Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwenye huu Mradi wa BBT. Mradi huu ni mzuri ambao unawagusa vijana katika kuinua uchumi wao. Hata hivyo, ombi langu hapo, Serikali ingefanya kitu kimoja, pamoja na Wizara kuendelea na Mpango huo ili uende kwa speed kubwa, ni vizuri fedha hizo vile vile zingetolewa kwa kila mkoa. Yaani sisi pale Mara tungepewa kama ni bilioni mbili, maeneo tunayo yangetengwa na vijana wetu wengi wangepata mafunzo pale pale na wakaweza kujenga uchumi wao kupitia kilimo. Tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo ingewasaidia vijana wetu wengi kupata ajira na maisha yao yakaenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo liko tatizo ambalo watu wetu linawasumbua. Serikali iliweka mpango mzuri wa zille fedha za TASAF. Zile Fedha za TASAF ni fedha ambazo zinawasaidia wale watu ambao uwezo wao ni mdogo (kaya maskini), lakini leo hii ninavyoongea sijui kwa mikoa mingine lakini kwa Musoma imeleta kero kubwa. Leo huwezi kuamini tangu mwezi wa Kwanza mpaka sasa wameendelea kusubiri na wapo watu bado hawajalipwa fedha za TASAF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na hali hiyo kwa kweli imekuwa ni kero na tuone namna ya kumaliza hilo tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)