Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa maneno ambayo aliyatamka Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha hotuba yake, alisema; Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu Samia Suluhu Hassan, apewe maua yake. Na mimi narudia hivyo; apewe maua yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais tangu aingie madarakani amefanya maamuzi makubwa yenye manufaa makubwa kwa nchi hii. Kwanza alikuja na kauli inayosema kazi iendelee; maana yake nini, alikuwa anamaanisha kwamba miradi mikubwa ambayo ameirithi kutoka kwa mtangulizi wake ambayo ni ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii; Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Mradi wa SGR na miradi mingine ya aina hiyo, kwamba iendelee kutekelezwa. Ameendelea kuisimamia, inaendelea kutekelezwa. Hakuna mradi hata mmoja ambao umesimama; apewe maua yake kwa kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameongeza jambo moja kubwa vilevile, wakati ule tulikuwa tunatekeleza miradi mingi tu ya huduma za jamii, yeye ameiongezea fedha miradi ya sekta za elimu, afya, barabara vijijini, yote hiyo ameiongezea fedha kwa nia ya maendeleo ya wananchi wa Tanzania; apewe maua yake kwa sababu hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo ambayo yanazungumzwa sana katika nchi hii, ningependa kutoa ushauri; Watanzania wote hata kama tuna maoni mazuri namna gani tulenge katika kuitunza na kuilinda amani ya nchi yetu, amani ya nchi yetu ni lulu. Ndiyo maana unaona kwamba kuna wanafunzi kutoka Sudan wamekuja kusoma Tanzania kwa sababu nchini kwao imekosekana amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana viongozi wa vyama vya upinzani, viongozi wa dini, kama wana jambo lolote kwa umoja wao wanaweza wakaandaa mkutano wakaomba kukutana na Mheshimiwa Rais, kama kuna ufafanuzi wowote Mheshimiwa Rais hatakataa kuonana nao, ataonana nao, watazungumza na wataelewana ili manufaa ya Taifa letu yaendelee kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze sana vipaumbele vya bajeti ya mwaka huu, 2023/2024, vizuri kabisa. Cha kwanza kabisa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi kwenye uwekezaji na biashara. Hili neno uwekezaji limelihesabu katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amelitaja mara 57, uwekezaji. Maana yake ameonesha msisitizo kwenye kipaumbele hiki. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote, lakini haya najua amefanya kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais; apewe tena maua yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele kikubwa cha pili; kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ili kukusanya mapato mengi zaidi, ikiwemo kutoka kwenye masoko ya fedha ya kimataifa kwa nia moja kwamba tukipata mapato mengi zaidi tuyapeleke kwenye miradi ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii; apewe maua yake Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaumbele hivi viwili vinategemeana; ili sekta binafsi iwekeze inategemea sana uwekezaji wa sekta ya Umma. Ili sekta binafsi iwekeze inategemea sana Serikali iwekeze kwenye maeneo ambayo yanatoa huduma kuihudumia sekta binafsi. Nilisema siku ile ya mradi wa bandari nilivyochangia; nilisema kwamba ili sekta binafsi iwekeze inahitaji gharama nafuu za umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Serikali inaelekeza fedha nyingi zaidi kwenye kulipa kwa ajili ya kuwekeza kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, lakini kwa ajili ya kuwekeza kwenye gesi, na kwa ajili ya kuwekeza kwenye vyanzo vingine vya umme na nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kule kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere wako Wamisri; kule kwenye LNG kuna mataifa mengine tunayoingia nayo mkataba; kule kwenye vyanzo vingine kuna mataifa mengine tunaingia nayo mkataba. Sasa kama kila mtu ataanza kuhoji kwa nini tunaingia mkataba na nchi nyingine, kwa nini tusiboreshe ujuzi wa watu wetu; ni mpaka lini tutaboresha ujuzi wa watu wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka twende kwa haraka ndiyo maana tutakutana na mataifa mengine kwa ajili ya kushirikiana nao. Wenzetu wamesha-advance, ili watusaidie na sisi tuweze kukimbia badala ya kutembea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji gharama nafuu za usafiri na usafirishaji, ndiyo maana tunawekeza kwenye SGR, tunawekeza kwenye viwanja vya ndege, tunawekeza kwenye barabara za lami na madaraja makubwa, tunawekeza kwenye vivuko, tunawekeza kwenye miradi mingine kama hiyo ya bandari. Tunahitaji kukimbia badala ya kutembea ili tuweze kuwafikia wenzetu ambako wamefikia tunahitaji linkages. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wafanyabiashara wawekeze kwenye sekta binafsi wanahitaji Serikali iwekeze kwenye uzalishaji wa malighafi. Ndiyo maana hii miradi ambayo inakuja kupitia sekta ya kilimo nayo ni muhimu sana ili waweze kupata malighafi kwenye viwanda, viweze kufanya kazi kwa mwaka mzima ambapo vitatoa ajira kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali inawekeza kwenye kuzalisha ujuzi. Wafanyakazi wenye ujuzi watapatikana kwenye vyuo vyetu vya kati na vyuo vya ufundi. Hapo napo lazima Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan apewe maua yake kwa uamuzi wake wa kuondoa adha kwenye vyuo vya ufundi, lakini vilevile kuondoa adha kwenye vyuo vya kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuendelea bila kupata nguvu kazi yenye ujuzi. Uwekezaji huo ambao unawekwa na Serikali ni jambo la muhimu sana la kuunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi kwenye majimbo yetu. Kwenye majimbo yetu iko miradi muhimu ambayo inaendelea kutekelezwa kwa muda mrefu. Ninaiomba na kuishauri Serikali, ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kule kwenye Baraza la Mawaziri kuna miradi ambayo inaendelea kutekelezwa hapa nchini kwa muda mrefu, naomba ipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ile barabara namba T8 ambayo inatoka Mwanza – Shinyanga – Nzega – Tabora – Ipole – Rungwa mpaka Mbeya kupitia Chunya, hiyo barabara ikikamilika ni linkage kubwa sana katika ku-supply vitu mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha Ipole – Rungwa hakina mkandarasi; kipande cha Rungwa – Itigi hakina mkandarasi; kipande cha Rungwa – Makongorosi hakina mkandarasi. Ni jambo muhimu sana kuweka kipaumbele kwenye barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara namba T9 ambayo inatoka Biharamulo inapita Nyakanazi nakwenda Kasulu, ikifika Kanyani mpaka Uvinza haina Mkandarasi na kutoka Uvinza mpaka katikati pale kabla hujafika Mpanda hakuna Mkandarasi; inakwenda mpaka Tunduma, hiyo nayo ni muhimu sana ipate kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya maji ambayo nayo haijakamilika kwa muda mrefu. Kule kwangu kuna mradi wa Bwawa la Igumila kwa ajili ya kusambaza maji kwenye kata za Kitunda na Kireli lakini kuna extension ya mradi wa maji wa Ziwa Victoria nao bado haujafika kwetu, naomba speed ikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya REA ambayo inatakiwa ikamilike by mwezi Disemba mwaka huu. Nayo Serikali iendelee kuweka kipaumbele ili ikamilike kama ratiba ilivyotangazwa kwa wananchi. Tusicheleweshe kabisa miradi ya umeme ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi hii. Baada ya hapo kipaumbele kiendelee kuwekwa kwa ajili ya umeme kwenye vitongoji ambao mwaka huu unaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kwenye sekta ya kilimo; siku ya bajeti ya kilimo nilitaja hapa madeni ambayo wakulima wangu wa Sikonge bado wanadai mpaka leo, kwa muda wa miaka miwili, mitatu. Nilipendekeza siku ile kwamba Serikali illipe hayo madeni halafu yenyewe ndio iendelee kubanana na hizo kampuni. Lakini baadaye nikasikia Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ametoa maelekezo kwenye hii Kampuni ya TCJE ambayo iko badala ya Apex ya ushirika. Kwamba hii kampuni ya TCJE walipe hayo madeni kwa kukata kwenye utaratibu wa pembejeo na nini. Mimi namuunga mkono Mheshimiwa Waziri, lakini nilikuomba naomba sasa…

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kakunda kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Cherehani.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nampa taarifa mzungumzaji, naomba tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha aondoe kodi kwenye duty twine, hessian cross ili kampuni hii ya TCJE iweze kupata faida kubwa na iende kumalizia madeni ya wakulima wa Tumbaku ambao hawajalipwa kwenye Mikoa yetu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kakunda taarifa unaipokea?

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa na ninamini Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo wameisikia hiyo taarifa, na wataifanyia kazi ili wakulima wetu waweze kulipwa madeni ambayo wanadai kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hoja hiyo kwa mara ya mwisho, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa jinsi ambavyo ameandaa bajeti vizuri na akawasilisha vizuri. Zile mwembe alizokuwa anatupa hapa vilikuwa ni vionjo ambavyo vimewafanya Watanzania wamwelewe vizuri na waielewe bajeti yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)