Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa bajeti nzuri sana iliyolenga kuwakomboa Watanzania yenye mahela mengi, yenye ma-bi na ma-bi na ma-tri. Kwa hiyo tunampongeza sana Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tumpongeze Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mwigulu, kwa bajeti aliyoiwasilisha nzuri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Naibu Waziri na timu yako, pamoja na Katibu Mkuu na wataalamu wako; tunakupongeza sana kwa kazi nzuri ambayo unaifanya ndani ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ya kuchangia katika bajeti hii. Kwanza nitoe shukrani kwa fidia ambayo tumekuwa tukizungumzia pale Makambako inayohusiana na polisi; tunakushukuru sana kwa kutupa fidia ile, wananchi wale sasa wameweza kufaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ziko fidia mbili ambazo bado, fidia ya kwanza ni watu wa umeme wa upepe; watu hawa wamesumbuka zaidi ya miaka 20, hatimaye hatujui nani mwekezaji anayewekeza, maeneo yao yamezuiliwa kwa muda mrefu. Tunaiomba Serikali kama haiwezekani basi wananchi hawa waweze kuendelea na maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ya pili inahusu Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo walishalipa fidia, kuna baadhi ya watu 18 ambao bado uhakiki wao ulikuwa haujakamilika. Tuombe wakakamilishe uhakiki wao ili waweze kulipwa fidia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mapendekezo au masuala yaliyokuwa yanawahusu wafanyabiashara. Tunaishukuru Serikali kwa bajeti hii imewajibu mengi mazuri. Lakini nizungumzie mambo mawili; moja ni hili la VAT ambalo lilikuwa linapendekezwa za VAT kutoka shilingi milioni 100 Serikali imejibu sasa itakwenda milioni 200. Ombi langu; fedha milioni 200 kwa sasa ni ndogo, twende mpaka milioni 300 tutakuwa tumekusanya wafanyabiashara wengi ili waweze kujiunga na suala la VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili linahusiana na faini; faini ilikuwa shilingi milioni nne na ushee. Tunaishukuru Serikali imekubali kupunguza maombi ya wafanyabiashara ambayo sasa faini yake wameiweka shilingi milioni tatu. Bado idadi kubwa ya wafanyabiashara hawa, zaidi ya asilimia themanini na kitu, hawana elimu; ombi langu, faini hii ya shilingi milioni tatu bado ni kubwa, siyo suluhisho. Tunaomba angalau sasa iwe milioni moja. Ikiwa milioni moja angalau kwa sababu milioni tatu hela hizi ni nyingi sana kwa faini ya mfanyabiashara ambaye ni mlipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya vitu vinafanyika bila mfanyabiashara kujua kwamba hili amelifanya ni kosa. Kwa sababu kama nilivyosema, wafanyabiashara walio wengi hawana elimu lakini ndiyo idadi kubwa ya wafanyabiashara ambao wako katika nchi yetu. Kwa hiyo, tunaomba bei hii iweze kupunguzwa kutoka amount iliyowekwa sasa iende shilingi milioni moja, ikiwezekana ishuke zaidi, kwa sababu nia ya Serikali siyo kukusanya faini, ni kukusanya kwenye uhalisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni wakulima wa zao la ngano; bajeti hapa anaelezea Mheshimiwa Waziri alipokuwa anawasilisha HS Code 1001.99.10 na 1001.99.90. Sisi kule Njombe Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Mtaka, amehimiza wananchi juu ya kulima ngano, Wilaya za Wanging’ombe na Ludewa ni wakulima wa ngano wakubwa ambao wameitikia, na kwa sababu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe, alihimiza sana kwamba ngano sasa inatakiwa ipatikane kupitia nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukienda Arusha wenzetu wa Arusha nao wameitikia wanalima ngano; ukienda Manyara vilevile wanalima ngano. Sasa kwa kupunguza kodi ngano inayotoka nje kutoka 35 kwenda 10 unawafanya hawa wakulima wa ndani sasa waone hauna umuhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani hii bei 35,000 ya kutoka nje ibaki palepale ili kusudi hawa watu wa viwanda wanunue ngano inayozalishwa hapa, tutakuwa tumewatendea haki wakulima wetu sana. Kwa hiyo, ninaomba sana kwamba Serikali, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, ulione sana jambo hili. (Makofi)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Deo Sanga, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Festo Sanga.

TAARIFA

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Hiki anachokizungumza mzee wangu, Mheshimiwa Sanga, ni jambo sahihi kabisa kwa sababu Mheshimiwa Rais, mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Wilaya ya Makete tu ametoa ngano bure kwa wakulima iweze kulimwa kwa ajili ya kusambaza viwandani. Kwa hiyo, kitendo cha kushusha kodi kinakwenda kusababisha kwamba wakulima wetu wawe stranded kwa maana ngano wanayolima sasa itakwenda kukosa soko. Kwa hiyo, hili lazima Wizara ya Fedha iangalie kwa sababu tayari Mheshimiwa Rais ameshachukua hatua ya kushusha na kusambaza ngano bure kwa wakulima nchini, ikiwemo Makete.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Deo Sanga, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili kwa sababu nia ya Serikali ni nzuri, kwamba tuhimize watu wetu ngano izalishwe kwa wingi kupitia Nchini Tanzania, na wakulima wameitikia, na sisi kule Njombe kupitia Mkuu wetu wa Mkoa amehimiza jambo hili, na hata Iringa nao wanalima ngano sana sasa, wameitikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba kwamba Serikali, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, jambo hili liangalie mara mbili, na utakapokuja kwenye majumuisho lazima utupe majibu ili wananchi nchini waweze kujua Serikali imechukuaje hatua juu ya jambo hili ambalo wanategemea kuuza ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho; niishukuru Serikali kupitia Waziri mwenye Dhamana ya Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Ashatu, kwa kuweza kulipa fidia ya Liganga na Mchuchuma kule Njombe; tunaishukuru sana Serikali sisi kule Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu kwamba sasa fidia imeshalipwa na ni hela nyingi, ombi letu kwamba sasa mradi huu ni lazima Serikali muhakikishe unaanza ambavyo wananchi wa Mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla wategemee kwamba Liganga na Mchuchuma sasa inakwenda kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho; tumepitisha bajeti hapa za kisekta, Wizara mbalimbali; ombi langu kwamba tuhakikishe sasa fedha hizi zinakwenda kwa wakati ili zikaweze kufanya kazi iliyokusudiwa ya maji, barabara, elimu, afya n.k. Kwa hiyo, naomba sana sasa fedha zianze kwenda ili mradi kule wananchi wanategemea sana, na sisi tutakapokwenda kwenye ziara mara baada ya mwisho wa bajeti hii sasa Wabunge nina imani tunakwenda kufanya ziara kwenda kuwaeleza wananchi tulichopitisha hapa fedha za ma-B nama-B na ma-T. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)