Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nami nashukuru kwa kupata wasaa huu wa kuweza kuchangia kwenye bajeti ya Serikali. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mambo ambayo anayafanya na maono ambayo ameyaweka mbele ya kugusa kila sekta. Niendelee kumtia moyo na kumwambia asitoke kwenye ujasiri wake kwa kila anachokiamini kwamba kinaenda kuliendeleza Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na Menejimenti nzima ya Wizara ya Fedha kwa jinsi walivyokuja na bajeti ambayo ni nzuri, inayogusa wananchi wa Tanzania. Pia nampongeza sana Waziri wa Fedha, siyo rahisi mtu kupunguza mipaka yako ya utawala, lakini umekubali kubeba maono ya Mheshimiwa Rais, kujipunguzia mipaka ya utawala, kukubali ile Idara ya Mipango basi irudi kuwa Tume ya Mipango. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa kufurahi kwa sababu ile idara, ile rasilimali iliyo pale na rasilimali watu ya wafanyakzi waliokuwa pale walikuwa hawatumiki ipasavyo. Ni kama walikuwa dormant fulani. Sasa nina hakika wataalamu wataenda kutumika vizuri na kuongeza uchumi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwa mliyofanya kwa watumishi wa Tanzania. Nawapongeza sana, pale Ukurasa wa 36 mmeorodhesha vitu mlivyofanya, lakini naomba niende kushauri sehemu ya madeni au malipo ya watumishi ambayo siyo ya kimshahara. Mmesema mmelipa, lakini naomba mwongeze juhudi, hasa kulipa likizo za walimu, watumishi wa afya walio kwenye Halmashauri zetu Tanzania. Nawapongeza kwa sababu sasa mmeamua stahiki za Wakuu wa Idara zilipwe na Serikali kupitia TAMISEMI. Hilo litaleta heshima iliyo bora kwa wale watumishi na kuongeza hadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti iliyopita Mheshimiwa Waziri alisimama hapa tukamshangilia sana. Wakaweka posho ya shilingi 100,000 kwa Watendaji wetu wa Kata, lakini posho hii badala ya kujenga, imeenda kubomoa. Watumishi hawa hawalipwi posho hizi ipasavyo. Wengine wanadai mwaka, wengine wanadai miezi mitano; humu nina message nyingi sana, wanasema, Mbunge wetu leo hilo lisemee. Naiomba Serikali, mje na utaratibu mzuri wa kulipa hizo stahili zao ambazo mlikaa hapa zikapotishwa kwenye bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wastaafu wetu. Kila Mbunge amesimama hapa amesema, kabla mtumishi hajastaafu hupewa barua ya miezi sita kwamba unaenda kustaafu. Sasa kwa nini Serikali msichukue jukumu la kuangalia ni nini kinachodaiwa kwenye mifuko mkakipeleka, kuliko huyu mstaafu sasa? Ameshastaafu na anaanza kuhangaika kufuatilia makato yake, kufuatilia malipo yake kwenye mifuko na wakati ule hana wanaomjua tena Serikalini. Hilo tuliangalie kwa ufasaha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni upande wa elimu. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa bajeti aliyokujanayo iliyoangalia mtoto wa mkulima ambapo sasa vyuo vya ufundi wanaenda kusoma bila ada na vyuo vya kati wanaenda kupata mkopo. Hongereni sana. Pia nashukuru kilichofanyika jana, tumeona kwenye mitandao. Tumeruhusu wanafunzi wa Sudani kuja kumalizia masomo Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu kabisa nitumie nafasi hii kuiomba Wizara ya Elimu na Serikali, tuna watoto wetu ambao walirudi kwa ajili ya vita kutoka Ukraine. Mpaka sasa hivi hatujafanya utaratibu warudi kwenye vyuo. Leo tumeleta hawa wa nje, hivi hawa wa hapa wanajisikiaje? Naiomba sana Serikali, na Waziri wa Elimu waangalie wazazi waliokuwa na watoto Ukraine ambao wengine ni madaktari, walikuwa wanakuja kuisaidia nchi, wengine ni wahandisi, wengine wanasomea taaluma nyingine mbalimbali, basi nao warudishwe kwenye vyuo wakaendelee na masomo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi sasa kwenye utendaji wa Serikali. Nawapongeza sana, kwani kumekuwa na ushirikiano wa kutosha kwa Mawaziri wetu, mmekuwa wanyenyekevu, tunapowafuata kuuliza tunavyotaka kuuliza, tunapata majibu. Wengine hata tukiwapigia simu saa nane usiku mnapokea. Nawaomba mwendelee na ushurikiano wa aina hiyo, mwendelee kumsaidia Mama, mwendelee kuyakuza maono ambayo yeye ameyaweka mbele, bila kuogopa inasema nini, bila kuogopa miluzi inayopigwa, lakini msimame kwa maslahi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi tena kwenye afya. Vituo vya afya vimejengwa, lakini nashauri kwamba hakiwezi kuwa kituo cha afya bila wafanyakazi na vitendea kazi. Tunashukuru juhudi za Serikali wameendelea kuajiri, lakini naomba tuwe na mkakati basi kwamba, wakati huu tujikite kuajiri wataalamu wa afya ili vile vituo visije vikageuka magofu. Naomba sana vituo vingi havina wataalam, vituo vingi havina vifaa tiba, basi tuweke nguvu yetu kule tuweze kuendeleza maono ya Mama Samia Suluhu Hassan ambayo ameyaweka mbele maslahi ya Watanzania, ambaye amejitoa usiku kucha akitupigania Watanzania. Basi na sisi tumuunge mkono kwa kuweza kufanya yale maono yake yaonekane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono. (Makofi)