Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna ya pekee sana alivyoendelea kushusha fedha kwenye majimbo yetu, lakini pia kuendeleza miradi mingi ya kimkakati ambayo imekuwa na bajeti kubwa lakini tumeona haijaweza kusimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana pia Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anazofanya katika Wizara ya Fedha pamoja na Naibu Waziri kwa kazi wanazofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo machache ambayo nataka kuchangia leo; jambo la kwanza nataka kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuondoa ada kwenye Vyuo vya Elimu ya Kati. Hili jambo limepigiwa kelele muda mrefu sana, lakini leo sasa kwa bajeti hii wamekuja na muafaka wa wananchi wengi ambao walikuwa wakipiga kelele eneo hili. Tuwapongeze kwa sababu wamekuja na source ya kutafuta fedha kwa namna ya pekee ambavyo sasa wanaenda kuyakabili haya ambayo wameyaleta kwenye bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona eneo ambalo wamekuja nalo katika mwaka huu wa fedha unaofuata kwa ajili ya bajeti ya mwaka unaofuata, wamekuja na kuongeza shilingi mia kwenye mafuta. Jambo hili ni jambo zuri na tuna imani kabisa kwamba sasa tunaenda kuona matokeo na shilingi mia itakavyoongezwa kwenye mafuta. Kwa mfano, Busega tuna barabara inayotoka pale Nyashimo kuelekea Dutwa kwa Mheshimiwa Kundo kule. Tunaomba hii barabara itengenezwe kupitia fedha hizi ambazo tumeziweka ili wananchi wa Jimbo la Busega waone matokeo ya shilingi mia kwenye mafuta na barabara hii ni barabara muhimu sana kwenye uchumi wa wilaya hizi mbili kwa maana ya Wilaya ya Bariadi pamoja na Wilaya ya Busega. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumza, sijui kama wameishafanya research ya kutosha kwa nini watu wanakwepa kutoa risiti na kwa nini watu hawadai risiti? Jambo hili ni jambo la kutiliwa maanani sana. Tuendelee kutoa elimu kwa walipa kodi, tuendelee kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili waendelea kutoa risiti na hawa wananchi ambao wananunua vifaa na wenyewe waendelee kuomba risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nimekuwa nikifikiria, sijui kama mmeishafanya cost benefit analysis kwamba kiasi kinachopotea kwa kutokutoa risiti kwa maana ya mwananchi kutokudai risiti kile kiasi kinachopotea ukilinganisha na kiasi ambacho tunaweza kumpa mtu anapodai risiti kama token kwa yeye kudai risiti. Nilikuwa najaribu kufikiria, wanaweza kuunganisha mfumo wa risiti za EFD wakaunganisha na namba za simu za wananchi kwa sababu kila mwananchi ana namba ya simu, anapoenda kununua anataja namba yake ya simu, halafu kunakuwa na mfumo TRA na mwananchi anapokuwa amenunua na kupata risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile risiti anapokuwa ameipata kwa mwezi mzima wanajua kabisa kwamba namba hii ya simu imepewa risiti kadhaa zenye thamani kadhaa wanam-credit bonus kwenye simu yake. Kwa sababu ameomba risiti hili jambo linaweza likawa zuri, hili jambo linaweza likawa na tija kwa mwananchi kuomba risiti. Kwa sababu mwananchi akiomba risiti ndipo atakuwa amechangia mapato katika nchi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie wananchi wa Tanzania kutokuomba risiti siyo kwamba wewe ndiyo unayenufaika, ananufaika yule muuzaji, kwa sababu ile kodi umemwachia, ile kodi anakula yule muuzaji kwa sababu hataipeleka TRA, kwa sababu hakuikatia risiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaweza kufanya hata mambo mengine kwamba, ile pesa wanaweza waka-credit kwenye kadi yake ya bima, wanaweza waka-credit kwa mwananchi ambaye hana, hapati mshahara kwamba anakatwa bima kupitia mshahara wake wakam-credit kwenye simu yake ikatumika kulipa matibabu yake. Hii itamwongeza mwananchi kujua kwamba ana haki ya kuomba risiti lakini mwananchi huyu huyu atajua kwamba nikiomba risiti mwisho wa mwezi nitapata credit ya manunuzi ambayo nimefanya. (Makofi)

Mhesjhimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mtu amefanya manunuzi ya shilingi milioni tatu, mwisho wa mwezi akapata credit ya shilingi elfu hamsini, anajua kabisa kwamba ninapoomba risiti mwisho wa mwezi nitapata credit kwenye simu yangu ya shilingi elfu hamsini. Naamini mapato ambayo tunayapoteza kwa wananchi kutokudai risiti ni makubwa kuliko mapato ambayo tutatumia kumpa mwananchi kama bonus kwa yule atakayekuwa ameomba risiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sasa Wizara ikae itafakari ione kama inafaa, basi tuwe na mfumo wa makampuni ya simu, mfumo TRA na mfumo wa hizi risiti tunazotoa ili ziweze kuwa na credit kwa mtu anapokuwa amenunua apate credit mwisho wa mwezi ili aone thamani ya kuomba risiti. Kwa sababu sasa hivi muda mwingine hawaoni thamani ya kuomba risiti ameenda kwa mfanyabiashara anaambiwa hii bidhaa nitakuuzia laki tisa, lakini bila risiti nitakuuzia shilingi laki nane na sabini ana-opt kutokuchukua risiti, lakini akijua kwamba nimefanya manunuzi ya kiasi fulani na mwisho mwezi nipata credit kutoa kwenye Serikali yangu, naamini kila mwananchi sasa atakuwa na morali ya kuomba risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasoma Ripoti ya CAG majuzi nikaona hata Serikalini. Serikali Kuu hawakuomba risiti yenye thamani ya bilioni 15, Mashirika ya Umma hawakuomba risiti za EFD milioni mia tano hamsini na siti, Serikali za Mitaa bilioni 10.08, jumla bilioni 25 hawakuomba risiti na ni watumishi wa Serikali. Hawa hawatufai, ni wahujumu uchumi kama wahujumu uchumi wengine, ni lazima sasa tuanze na Serikalini na wao wawe sehemu mojawapo ya kuhakikisha kwamba wanaomba risiti za EFD ili Serikali yetu ipate kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameeleza sasa ameongeza wigo wa usajili wa VAT kutoka turn over ya milioni mia moja kwa mwaka hadi turn over ya milioni mia mbili. Hili ni jambo zuri. lakini sidhani kama wamefanya utafiti mzuri wakaona kwamba turnover kuwa ndogo litaleta tatizo kubwa sidhani, tatizo kubwa ni wafanyabiashara kukwepa kodi. Kwa sababu duka A yeye hajasajiliwa VAT, duka B amesajiliwa VAT, mauzo huyu item ile ile anauza shilingi elfu mbili na kwa sababu hajasajiliwa ile VAT anauza elfu mbili, aliyesajiliwa na VAT inabidi aongeze asilimia kumi na nane, atauza elfu mbili mia tatu sitini, lazima huyu atauza zaidi kuliko huyu, nini kinatakiwa kufanyika hapo? Hapa jambo siyo kuongeza tu…

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sekiboko, taarifa.

TAARIFA

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Simon ameweka mchango mzuri sana, lakini nimpe taarifa kidogo kwamba kuongeza wigo wa VAT kunam-comfort mfanyabiashara kutoa risiti ya EFD bila kuogopa kufikia ukomo wa milioni mia kwa mwaka. Jambo ambalo litaongeza mapato zaidi kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Simon, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea, lakini sidhani kama ni tija sana, ninachotafuta hapa, natafuta fairness ya wafanyabiashara. Kwa sababu turn over ya milioni 180 haina tofauti kubwa na turn over ya milioni 210. Huyu mwenye turn over ya milioni 210 anakuwa amesajiliwa na huyu mwenye turn over ya milioni 190 yeye hajasajiliwa, lakini unakuta wanauza item ile ile. Huyu anauza simu hii hii na huyu anauza simu hii hii, huyu lazima auze bei ndogo na huyu lazima auze bei kubwa sababu ana VAT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kinachotafutwa ni kuwasababisha hawa wafanyabiashara kila mtu ajue kwamba kuna fair kwenye kodi. Nataka kumshauri Mheshimiwa Waziri, hapa ili kila mtu awe na fairness katika kulipa kodi wasajiliwe watu na VAT haijalishi turn over ni milioni 50 ili kila mtu sasa ajue kabisa kwamba hapa bei ya simu ni shilingi 200,000 na hapa bei ya simu ni shilingi 200,000, hakuna sababu ya kukwepa kutoa risiti kwa sababu wote mnauza bei sawa. Huyu anakwepa kutoa risiti kwa sababu anajua akitoa risiti itabidi aongeze asilimia 18 na mteja atamkimbia, ataenda kwa mtu ambaye hajasajiliwa na VAT kwa sababu anajua yeye hatachajiwa ile asilimia 18. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili kuwe na fairness naishauri Wizara itafakari na ifanye upembuzi yakinifu ikiona inafaa wasajiliwe watu wengi regardless of the turnover ili watu wengi waone kabisa kwamba there is fair katika biashara na waache kukwepa kodi. Ninachozungumzia hapa ni kuacha kukwepa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona umewasha microphone. Naomba niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)