Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa dhati kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia bajeti ya mwaka 2023/2024. Kwanza nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kupambana na kuimarisha nchi yetu, hasa katika eneo zima la uchumi. Sote ni mashahidi katika nchi za Afrika Mashariki ukiacha indicator zingine lakini sisi ndio tumekuwa na nafuu kubwa ya kuwepo na kiasi cha dola kwenye nchi yetu. Pamoja na miradi mikubwa tunayoifanya tumeweza kustahimili. Na kama nilivyosema, pamoja na upungufu tuna reserve ya dola kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi nimpongeze Waziri wa Fedha ndugu yangu Mwigulu Nchemba kwa namna ambavyo ameendelea na utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kiuchumi, na nchi yetu imeendelea kustahimili na kuweza kuimarika katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kwa kuamua kuirudisha Tume ya Mipango. Jambo hili limesemwa sana na Waheshimiwa Wabunge kipindi kilichopita. Kwa vyovyote vile, Tume ya Mipango ni kitu cha msingi, ni taasisi ya msingi katika kuangalia maeneo gani Serikali ifanye na kuangalia dira katika upana mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inaongozwa na mama Samia, dira na maono ya nchi yetu yeye ndiye amevishikilia. Lakini ni wapi anaposhusha, anashusha pale kwenye Tume ya Mipango. Kwa hiyo mimi nataka niseme kwamba pamoja na kwamba sasa Tume ya Mipango imerejea utekelezaji wake uanze haraka. Kazi ya Tume ya Mipango ni kwanza kupanga, kufatilia na kufanya evaluation, kuona maeneo gani ambayo tunafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niseme kwenye suala zima la upungufu wa dola, fedha za kigeni hapa nchini. Sote ni mashahidi kwamba tuna miradi mikubwa. Ni kweli kwamba tunatumia fedha nyingi kuagiza vifaa vya ujenzi. Lakini vilevile bado tuna tatizo la kununua vyakula na hata mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Tunanunua sana ngano kutoka nje ya nchi kwa kipindi kirefu, tunaagiza mafuta ya kula ya kutosha kutoka nje ya nchi, mbolea, dawa na vitu vingine vyote. Suala hili linasababisha kutozalisha sisi wenyewe ili tuweze kuzuia matumizi ya dola nje ya nchi. Vilevile hatuzalishi tuweze ku-export kile tunachokizalisha katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naishauri sana Serikali; katika suala zima la uwekezaji tuendelee kuweka mazingira mazuri kwa kutoa incentives kwa wawekezaji wetu. Lakini kubwa zaidi bado ziko changamoto. Changamoto kubwa tulionayo kwenye uwekezaji ni suala zima la ardhi. Wanakuja wawekezaji wanataka kuwekeza lakini kinacholeta kikwazo ni kwamba TIC hana ardhia ambayo anaweza akampa mwekezaji, na bahati mbaya mifumo hii hai-link. Wizara ya Ardhi na TIC bado hawakai pamoja. TIC anamleta mwekezaji anamwahidi kuja kuwekeza lakini ikija hapa inachukua miaka mingi kuweza kulipa fidia kwa wakulima wetu au kwa watu walioshikilia ardhi. Kwa hiyo jambo hili tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, zipo kampuni kubwa zenye uwezo wa kuzalisha hapa nchini katika baadhi ya maeneo ambayo ni nyeti, iwe katika eneo la vioo, glass na mambo mengine. Serikali inaweza kuongea nao, kwamba, je kama tukiwapa mtaji zaidi mnaweza mka-double production? Na tukaangalia, yapo maeneo tunaweza tukauza. Sisi katika nchi za SADC ni wazalishaji wakubwa katika maeneo mbalimbali. Masoko yetu tunayo; Congo ni soko letu kubwa. Tunafanyaje ili tuweze kuongeza uzalishaji na tuweze kupata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Serikali ilileta hapa Sheria ya Local Content lakini sheria hii haisimamiwi katika maeneo mbalimbali. Bado kuna material ya kwenye viwanda yanaagizwa kutoka nje ilhali katika nchi yetu yapo. Sasa kwa mfano kwenye cement tulikuwa tunatumia chuma ya hapa nchini. Imetokea gafla sasa viwanda vinaagiza clinker kutoka nje ya nchi. Mimi katika jimbo langu tulikuwa tunazalisha sana chuma ambayo tulikuwa tunatumia kwenye viwanda vya hapa nchini, sasa hatuzalishi halitoki hata lori moja. Sasa mambo kama haya tungeweza kuzuia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile yapo madini mbalimbali ambayo yanapatikana kwa wingi katika nchi yetu, bado nayo tumeruhusu viwanda vinaamua kuweza kuleta hapa nchini, jambo hili tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nimelesema sana kwenye suala zima la nyama. Dodoma sisi tuna kiwanda cha machinjio ya Kizota, na bahati mbaya sisi baadhi ya nchi zimetufungia tusipeleke nyama kwenye nchi zao kwa sababu ya machinjio yalivyokuwa na uchakavu. Vipo viwanda viwili, vitatu vya wawekezaji lakini havikidhi matakwa ya kupeleka nyama kwenye nchi hizo. Lakini kiwanda hiki cha Kizota kinahitaji bilioni mbili kuweza kukarabatiwa. Mimi huu ni mwaka wa tatu naongea na Serikali, hadi naona huruma kama ningekuwa na bilioni mbili ningeweza kutoa mimi mwenyewe kukarabati pale. Sasa miaka mitatu consecutively bilioni mbili hatuwezi kukarabati pale

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tatizo lililopo ni kwamba mimi nimewahi kufanya biashara ya nyama; hakuna sehemu ambayo inategemewa kama central zone. Na viwanda vingine siwezi kusema ambavyo vya watu binafsi, ukianza kupeleka kwake kuuza baadaye anachukua lile soko. Kwa hiyo wafanyabiashara wetu wanapata shida vilevile hatupati faida ya mifugo. Mheshimiwa Waziri wa Fedha nakuomba sana bilioni mbili tuweze kukarabati kiwanda kile, nakuomba sana sana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu wakandarasi wetu katika nchi yetu. Naishukuru sana Serikali imetoa kipaumbele kikubwa kwa wakandarasi nchini. Shida iliyoko ni kwamba wanachelewa kulipwa malipo yao, jambo hili Serikali iliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba, duniani kote mashirika ya bima (insurance) ndio yanayobeba riski katika biashara. Sasa siku hizi wakandarasi wetu wakienda kuchukua bima kwenye mashirika ya bima wanaambiwa watoe collateral. Sasa kwenye benki naambiwa nitoe collateral na kwenye shirika la bima nako naambiwa nitoe collateral; sasa kazi ya bima wanasema ni risk aging. Sasa bima nayo inataka nipeleke collateral. Na tunakoelekea kuna siku tutaona bima inatangaza kuuza nyumba ya mtu fulani ambacho duniani kote hicho hakipo. Sasa jambo hili kwetu unaambiwa kwamba lete collateral ili uweze kupata bima. Sasa risk anayoichukua mtu wa bima iko wapi? jambo hili naomba tuliangalie sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tuna ushindani wa makampuni ya wakandarasi kutoka nje ya nchi. Wenzetu wanapewa mazingira mazuri, wana benki zao, lakini vilevile wana risk company zao ambazo ukilinganisha na kiasi ambacho tunawatoza wakandarasi wetu ni tofauti kubwa sana. Kwa maana hiyo unataka mimi nilyefungwa miguu wote tukimbie mita 100 ilhali mwenzangu hajafungwa miguu. Jambo hili kama tunataka kuinua wakandarasi wetu ni makusudi kabisa tufanye hivyo na kufanya hivyo kwamba fedha yetu itabaki hapa. Mheshimiwa Waziri naomba jambo hili tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kazi ya Serikali duniani kote ni kuhudumia wananchi wake, iwe katika eneo la afya na katika maeneo mengine. Tuna tatizo. Wapo wahisani wanatusaidia katika maeneo ya afya na katika haswa suala zima la majiā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa sekunde 30 muda wako umeisha.

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie; ni kwamba wahisani hawa wanavyoleta vifaa vya kuja kuleta miundombinu ya maji wanatozwa fedha kwa kodi na jambo hili linawavunja moyo. Kwangu nina mwisani ambaye ameleta takriban bilioni mbili ametoa kodi kama milioni 600, fedha ambayo ingeweza kutumika kujenga mradi mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru lakini nataka niseme kwamba Serikali iangalie namna ya kuweza kuondoa kodi kwa wahisani wanaoweza kutusaidia katika maeneo ya huduma za wananchi. Nakushukuru sana, ahsante sana.