Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Emmanuel Papian John

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ninalopenda kuzungumzia ni juu ya reli hii ambayo imepangwa kujengwa lakini napenda kushauri kwamba ujenzi wa reli hii uwe kwa awamu kwa sababu kila anayesimama anazungumzia reli, lakini reli haiwezi kujengwa kwa wakati mmoja, nafikiri tujenge reli kwa awamu kama ni Dar es Salaam - Tabora, kama ni Dar es Salaam – Mwanza. Hilo ni jambo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kuna barabara ya kutoka Handeni - Kibirashi - Kijungu - Kibaya - Njoro nimeiona kwenye mpango. Barabara hizi kuzijenga ni gharama kubwa kwa Serikali na ukiangalia gharama na jinsi zinavyotakiwa kwa maana kwamba kila mtu anaomba barabara, ningeshauri mambo yafuatayo:-
Naomba Mheshimiwa Waziri safari hii ajenge barabara kutoka Handeni - Kibirashi aishie hapo, mwakani ajenge Kibirashi – Kibaya - Kiteto aishie hapo, mwaka unaofuata ajenge Kibaya - Chemba aishie hapo, mwaka unaofuata ajenge Chemba – Singida, ndiyo njia pekee inayoweza kusaidia barabara hizi kuisha. Hizi barabara unaweka upembuzi, pesa inaingia, feasibility study baada ya muda fedha zikikosekana mnaanza upya tena, hizi zote ni gharama kwa Serikali na tunapata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kushauri barabara zijengwe kipande kidogo kidogo na kwa awamu. Barabara itakayopata mfadhili wa nje kama ni kilometa 400, 500 akiianza amalize yeye mwenyewe lakini kama ni fedha za ndani tujenge kidogo kidogo ili na maeneo mengine yapate na fedha nyingine zitumike kujenga barabara hizi za vumbi na changarawe katika maeneo mengi ikiwa ni sehemu ya kufungua barabara zetu za vijijini. Hilo ni jambo la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti jambo la tatu, naomba kushauri kama inawezekana tubadilishe mfumo wa manunuzi itusaidie kwenye mambo haya yafuatayo; hizi fedha zinazotengwa kwenda kwenye halmashauri zetu kwa ajili ya barabara hebu toeni asilimia 20 tukopesheni vifaa kwa ajili ya barabara. Mkoa mzima wa Manyara kama umetengewa shilingi bilioni tatu au shilingi bilioni nne, asilimia 20 Serikali tukopesheni vifaa, weka government guarantee tupate katapila na vifaa vingine vya ujenzi wa barabara, sisi wenyewe tu-fuel halmashauri zetu kutokana na collection za ndani, tutumie gharama nafuu kutengeneza barabara zetu za halmashauri vinginevyo ni gharama kubwa kwa Serikali. Tusipobadilisha hii sheria hatuwezi kupata hiyo guarantee na kuweza kununua vifaa vyetu. Najua hii inaokoa fedha nyingi za Serikali lakini kama kuna mikono ya watu wanaotafuna haiwezi kupita. Naomba Wabunge mniunge mkono kwa hili tuweze kuwa na vyombo vyetu vya kutengeneza barabara zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Arusha – Kibaya - NARCO, nimekuwa namwambia Mheshimiwa Spika barabara ya NARCO - Kiteto mbona huizungumzii anasema nimebanwa. Sasa Mheshimiwa Waziri useme leo umembanaje Spika, kwa nini hutengenezi barabara hii? Barabara hii ni ahadi ya Serikali, ni ahadi ya Mheshimiwa Kikwete mwaka 2013 mpaka leo imeshindikana. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, jenga barabara ya NARCO – Kongwa na NARCO - Dosidosi tu. Jenga Kongwa kwa mwaka huu mwaka unaofuta jenga Dosidosi mpaka Kibaya kilometa 39, kidogo kidogo mwisho wa siku utafika Oljoro, Arusha. Mimi naomba tujenge barabara kwa awamu ili hii barabara itengenezeke, lengo ni kufungua barabara hii ili mazao yaweze kutoka. Kiteto ndiyo inayolisha Tanzania kwa maana ya Dar es Salaam, ndiyo inayolisha Kanda ya Kati, kwa nini hamfungui barabara hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi wa pili ndani ya barabara ile zimeanguka gari saba kwa siku moja zikipeleka chakula cha msaada. Sasa kwa nini msifungue hii barabara tukaweza kupita, ni zaidi ya kilometa 91 tu. Nadhani jitihada za makusudi hazijachukuliwa kukamilisha ujenzi wa barabara hii. Barabara ya Oljoro - NARCO iliwahi kutengewa shilingi milioni 900 mwaka 2013 za upembuzi mpaka leo hatujui zilienda wapi. Tunaomba hii barabara iangaliwe na itengenezeke, tutaamini kama Thomas tutakapoona wakandarasi wako site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya ndege, ndege tunazihitaji, tunahitaji Watanzania watembee lakini kuna jambo nataka kushauri. Viwanja vyote vya ndege ambavyo sasa vina vumbi, vimekwanguliwa hebu suburini kwanza, jengeni hivi viwanja vyote ambavyo mmeanza vya Dar es Salaam, Arusha, KIA, Mwanza ili vimalizike, tujenge kwa awamu na tutakapomaliza tuanze kiwanja kimoja kimoja kwani kushika miradi mingi kunatupotezea mambo mengi. Bajeti ya nchi ni ndogo, fedha zinazokusanywa ni kidogo, tufanye jambo liishe tukirudi hapa tuseme liliisha. Kila siku unazungumzia habari ya kiwanja cha Mwanza, miaka 10 unahangaika na nini kama kimetushinda kiacheni! Jenga Dar es Salaam ukimaliza hamia Arusha, ukimaliza hamia Mwanza, ukimaliza hamia Kigoma, ukimaliza hamia Kagera, maliza kwanza kimoja ujue kwamba kiliisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndege. Rwanda ina ndege mpya 14 na ni nchi ndogo, ATC imebaki alama, kwa nini? Mmeonyesha mpango wa kununua ndege lakini kama tunanunua ndege, niwashauri Wabunge wenzangu tukubaliane tutafute CEO wa kampuni au shirika hilo kutoka nje, siyo Mtanzania watalifuta, litaliwa! Watafunaji ni wengi na kwa sababu hakuna anayeiunga mkono Serikali, leo tunalalamika ndege, ndege, tumeuwa wenyewe, tunatafuna wenyewe, kilichoko kinaliwa, mashirika kutoka nje yanatutafuna, tuna-sign wenyewe, mnahangaika na nini? Tu-import wataalam watufanyie kazi tuwalipe ili tuokoe vinavyowezekana. Naomba kushauri hizi ndege zitakazonunuliwa punguzeni watumishi wote wa ATC bakiza wachache, zitembee ndege chache, zifanye kazi, wakope wanunue nyingine ziweze kutembea ndani ya nchi yetu at least kwa hesabu tukijua kwamba wamekopa watalipa, wakishindwa magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mbunge mmoja amesema barabara za lami wanabandua wanabandika, ndiyo! Kitaalam lami life span yake ni miaka 15, ikiisha biashara imekwisha lazima ubandue. Ukiona imedemadema mkandarasi alikuwa mzuri, unashukuru Mungu. Leo hii reli ya kati life span yake ilishaisha, ukiona inademadema Mungu ametusaidia. Mimi naomba watu wazungumze kwa data, tuone ni jinsi gani tunatakiwa tutoke hapa, hizi barabara nyingi kushindikana kwake ni kwa sababu hata wakandarasi wetu wengi wamekuwa wachakachuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri leo, kama leo Dangote Mtwara simenti inaweza kuwa shilingi 8,000; kwa nini tusijenge barabara za zege? Kama tunaweza kupasua mawe, tukachukua simenti ya gharama nafuu, mwaga zege barabara toka Mtwara kwenda Songea, kwenda Ruvuma pasua huko kote, una haja gani ya kuhangaika? Kama tuna kiwanda Tanga, jenga barabara ya zege kutoka Handeni njoo mpaka Singida watu watambae huko. Una haja gani ya kuagiza lami Ulaya ambayo tunatoa pesa za nje wakati pesa hizo hatuna? Internal collection yetu, simenti ni yetu, mawe ni yetu, mwaga zege barabarani wakandarasi tunao ili barabara ziweze kupitika kwa muda ambao sisi tumekusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kushukuru na naunga mkono hoja.