Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

kunipatia nafasi ili niweze kuchangia kwa niaba ya watu wa Tarime. Kwanza nimesoma hiki kitabu cha bajeti na hotuba ya Waziri na niseme tu kwa niaba ya watu wa Mkoa wa Mara, nina masikitiko makubwa sana, na watu wa Mkoa wa Mara, hawataunga mkono bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba Rais alichoahidi wakati wa kampeni akiwa Mkoa wa Mara mzima, aliahidi uwongo, kwa sababu nimesoma kitabu hiki, Mkoa wa Mara mzima umepewa 0.8 kilometa za lami, haikubaliki; watu wa Mkoa wa Mara ndiyo wenye mbuga kubwa kuliko zote, Mbuga ya Serengeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Mkoa wa Mara ndiyo waliokuwa na mgodi wa Buhemba, ambao umechimbwa umekwisha madini pale, wana mpaka wa Sirari, wana Ziwa Victoria wanatoa samaki pale, wana Mgodi wa Nyamongo ambao unaendeea kuua watu. Halafu inapofika kwenye maendeleo, hamuwapelekei pesa haikubaliki, haitakubalika kwa viwango vyovyote vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nitamtaka Waziri aje atujibu hapa na nimesoma kitabu cha Mpango hiki hapa, Mheshimiwa Waziri amepeleka kiwanja cha ndege Geita Wilaya ya Chato; kutoka Geita Mjini kwenda Chato kwanza ni kilometa zaidi ya 100 na kitu, sijui amepeleka kwa kujipendekeza kwa Rais au ni Rais mwenyewe amemwagiza akipeleke nyumbani kwake sijui hilo atatujibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwangu hapa ni kwamba, Mkoa wa Mara ambao una mbuga ya wanyama ya Serengeti, ina ziwa pale Musoma tunashindwa kujenga uwanja wa Mkoa wa Mara, uwanja wa ndege na kuuboresha uwe wa Kimataifa, wazungu washuke pale walete uchumi kwa watu wa Mkoa wa Mara. Tunachukua mikoa mipya ambayo imeanza juzi, tunaitengea mabilioni ya pesa kwenda kujenga viwanja ambavyo havina muunganiko wowote wa kiuchumi, ni viwanja vya watu kusafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja huu wa Mkoa wa Mara tunauhitaji kwa kweli; naomba sana Waziri anapokuja kuzungumza hapa azungumze hili, kwa sababu ni aibu kwa watu wa Mkoa wa Mara ambapo Mwalimu Nyerere anatoka kule na kila siku mnamsifia, lakini kutendea watu hawa haki hamfanyi hivyo. Hivi kweli watu ambao tunachangia madini yetu mnachukua, samaki wetu mnachukua, kila kitu mnachukua pale, wanyama mnachukua. Jana Mheshimiwa Maghembe alikuwa anasema hata kuchunga hataki tuchunge, anasema ng‟ombe wetu ni tatizo, kwenye ardhi ya kwetu wenyewe, ng‟ombe anasema ni shida; tunachoambulia na mbuga ile ni ng‟ombe wetu kupigwa risasi, ni watu wetu kubaki vilema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kukubali hali hii, unapofika wakati wa kutuletea pesa, hospitali ya Kwangwa pale imekuwa wimbo. Haya ni matusi na nitaomba Waziri aje atuambie ni lini mnakwenda kujenga uwanja wa ndege wa Mkoa wa Mara ili kuunganisha watalii waje Serengeti na sisi tuna ziwa pale, watalii wanapenda beach, sisi tuna beach pale, watakuja kuogelea pale, mtuunganishie mtuletee uchumi, hilo ni la muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu barabara. Barabara ya kutoka Tarime kwenda Serengeti ni barabara muhimu. Wote mnajua watu wa Serengeti chakula wanachokula kinatoka Tarime na hii barabara bahati nzuri inapita kutoka Tarime Mjini inakwenda inapita Nyamongo, mnakochukua mawe ya pesa, lakini mnataka wale watu waendelee kufa na vumbi, wakati dhahabu yao mnachukua, na kila siku wanapigwa risasi na jana walipigwa risasi pale, hata kuwapelekea barabara, hamuoni aibu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarime nzima hakuna hata mita moja ya lami ambayo mmetujengea pale, wakati madini yanatoka pale. Kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri aje atujibu, hii barabara ndiyo inalisha watu wa Musoma, ndiyo inalisha Bunda, ndiyo inaleta ndizi Mwanza, tofauti na zile zinazotoka Kagera. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kujibu atuambie na hili siyo la kwangu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati akihutubia Nyamwaga na wakati akihutubia Nyamongo, aliwaahidi watu hawa barabara hii ya lami ya kutoka Tarime mpaka Serengeti. Tunaomba Mheshimiwa Waziri aje atuambie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu vingine vinafanyika unashangaa, nimeona hapo mnafumua barabara ya lami hapa Dodoma, yaani watu wengine wanalala porini siku hata 10 hawana hata barabara mbovu, hiyo mnafumua eti imetoboka, mnaweka lami mpya. Hivi haya maamuzi mnayafanya mkiwa wapi? Kwa nini mnafanya maamuzi ya aina hii? Tunahitaji mje mtuambie majibu hapa, ni kwa vipi watu hawa wanapata barabara nzuri ya kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Ndege; nchi hii ni miongoni mwa nchi zinazotia aibu kweli kweli, karibu kwenye kila kitu, leo Rwanda nchi ambayo hailingani hata na Mkoa wa Mara, ina ndege zinaruka dunia nzima. Sisi ndege yetu ni Fast Jet ambayo hata Waziri anajua ukienda hata na begi unalipishwa. Nimelipishwa begi shilingi 200,000 kwenye ndege, Taifa halina hata ndege ya kuruka ndani kwa ndani hapa, acha kwenda Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka 55 ya uhuru hatuna ndege, sasa Waziri anakuja kutuambia hapa kwamba watanunua ndege, mtazitunza vipi, wakati watu wanahujumu, wanauza ndege ambazo zingefanya kazi wanauzia trip ma-fast jet, sijui wanahongwa. Kuna watu wako pale Air Tanzania wanakaa kwenye ofisi asubuhi mpaka jioni wanasubiri mshahara, halafu hawafanyi kazi, aibu, yaani hawarushi ndege hata moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mhasibu, kuna Engineer sijui kuna pilot sijui wanarushwa popo mle ndani? Labda kuna popo wanaendesha mle, wanaruka mle ndani, ndiyo ma-pilot wa hao popo.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, anapokuja hapa utoe majibu kwa Watanzania, ni kwa vipi au wana mpango gani wa kwenda kufufua Shirika lao la Ndege na lirushe ndege kwa nchi nzima. Kwa nchi ambayo tuna Maziwa tuna kila kitu, ndege haiwezi kuwa anasa kwa Watanzania kusafiria. Haya ni majibu ambayo Watanzania wanahitaji na tunahitaji kuyasikia hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana bajeti ya nchi yetu imekuwa ni formality tu; watu wanakuja hapa wanapiga kelele, mwaka baada ya mwaka, kuwa Serikalini, liwe jipu ni la CCM, uwe usaha ni wa CCM, viwe vyombo vya kutumbulia ni vya CCM, hatuna sababu yoyote ya kutetea majipu, yaani haipo kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa nasema, ni kwa nini mpaka sasa watu wa TANROADS ambapo hata mtoto anajua wamejenga barabara ambazo ni sawasawa na zile sahani tunazotumia kwenye hoteli zile disposable yaani barabara ukipiga teke hivi lami inaruka juu. Wamejenga barabara za kiwango kibovu cha aina hiyo, lakini mpaka sasa hatujasikia hata mtu mmoja ametumbuliwa kutoka TANROADS au ni kwa sababu mkubwa ambaye mmesema asiguswe humu alikuwa hapo? Hivi anashindwa vipi kuungamanishwa na hilo? Leo mmetumbua mpaka watu wa nyuki lakini watu wa TANROADS hatujaona wakitumbuliwa. Hatuwachochei mtumbue, tunataka mtumbue waliokosea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.