Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, nipo, nashukuru kwa kunipa nafasi naomba nami sasa nianze kuchangia Hotuba ya Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano. Nianze kwa kusema kwamba Mkoa wetu wa Njombe ni mkoa mpya, sitoacha kusema hivyo, kwa sababu tunahitaji maendeleo ili mkoa uweze kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kati ya barabara ambazo zimeshafanyiwa usanifu ndani ya Mkoa wa Njombe ni pamoja na barabara ya Njombe - Makete inayopita Mbunga ya Kitulo kwenda kutokezea Isonja, Mkoa wa Mbeya. Barabara hii iliwekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi namba moja, lakini vilevile barabara hii iliwekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2005 mpaka mwaka 2010 iliwekwa tena upya. Hiyo haitoshi, barabara hii Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati anakuja kuomba kura za Urais kule Makete na Wilaya ya Wanging‟ombe alisema kwamba barabara hii ndiyo ya kwanza ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali itekeleze ahadi ya Mheshimiwa Rais, barabara hii ina umuhimu mkubwa sana kwa sababu, barabara hii kama itatengenezwa kwenye kiwango cha lami itainua uchumi wa Taifa, katika zao la Pareto, lakini vilevile katika masuala ya utalii. Sisi kule Makete kuna Mbuga ya Kitulo kwa sababu barabara hii imepita kwenye mbuga ya Kitulo, sasa hivi watalii wanashindwa kwenda kwa wingi kwenye ile mbuga ya Kitulo kwa sababu barabara ile haipitiki. Hasa kipindi cha mvua ndiyo haipitiki kabisa. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kujenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kule katika barabara ile pia kuna mazao ambayo yanasafirishwa ya mbao, viazi mnavyokula Dar es Salaam vinatoka Makete. Barabara hii ina umuhimu mkubwa, naiomba Serikali iweze kujenga barabara hii. Vilevile ndani ya Mkoa wa Njombe bado kuna barabara nyingine ambayo imefanyiwa usanifu, barabara ya Njombe-Mdandu-Iyayi ambayo nayo inakwenda kukutana na Mkoa wa Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara hii wakazi wa Wanging‟ombe wanaolima mazao ya alizeti pamoja na mbao wanashindwa kusafirisha kwa urahisi kupeleka Mbeya, lakini vilevile wanashindwa kusafirisha kwa urahisi kuja Njombe ili kwenda mikoa mingine kama Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna barabara nyingine ambayo imefanyiwa usanifu, barabara ya Njombe - Ludewa, Manda – Itoni. Barabara hii ni muhimu kwa sababu kule Ludewa kuna makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma. Naiomba pia Serikali ikamilishe barabara hii kwa kuijenga kwa kiwango cha lami barabara yote ili kuweza kusafirisha makaa ya mawe kwa urahisi.
Mheshimwia Spika, pia tuna barabara ya kibena - Lupembe-Madete ambayo inaunganisha Mkoa wa Morogoro, tunaomba pia barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami. Nakumbuka asubuhi Mheshimiwa Hongoli aliuliza swali na Mheshimiwa Waziri alisema kwamba, barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami mwaka 2016 - 2017. Ukienda kwenye hotuba ukurasa wa 37 inasema kwamba Lupembe-Madete Kilometa 125 taratibu za kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu zinaendelea. Nimwambie tu Mheshimiwa Waziri, stage hii ilishapita, nilitegemea sasa hivi watatuambia kwamba labda tender inatangazwa kwa ajili ya kujenga barabara hii.
Mheshimiwa Spika, nina ombi moja kwa Serikali kuhusiana na Jimbo la Lupembe. Lupembe kuna barabara ambayo inatoka Lupembe-Lukalawa, inapita Ikonda kutokea Makambako. Barabara hii ni business road, kuna wakulima wanasafirisha sana mbao, maharage, pamoja na chai. Naomba sasa barabara hii itoke katika ngazi ya Halmashauri ipelekwe iwe barabara ya TANROAD, ili iweze kujengwa kwenye kiwango cha lami kwa uharaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitoke kwenye barabara niende kwenye kiwanja cha ndege. Mkoa wetu wa Njombe kiwanja chetu cha ndege cha Njombe kina hali mbaya sana. Kwa nini naomba kiwanja hiki? Ruvuma hakuna kiwanja cha uhakika cha ndege, lakini kama tutakarabati kiwanja kile cha ndege cha Njombe na kuweka kwenye kiwango cha lami ina maana ndege nyingi sana zitakuja. Kwa hiyo, Mkoa jirani wa Ruvuma watafaidika na kiwanja kile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, istoshe kule Njombe tunalima zao la maua haya, tunalima maua mazuri sana, kuna roses nyingi sana kule, tunashindwa kusafirisha kufikisha Dar es Salaam zikiwa fresh kwa sababu hatuna kiwanja cha ndege cha uhakika, hakuna ndege zinazokuja mkoani pale. Hivyo inasababisha kulega lega kwa kilimo hiki cha maua. Naiomba sasa Serikali ione umuhimu wa kiwanja hiki, wakarabati katika kiwango cha lami ili na sisi tuweze kusafirisha maua kwa wingi kuja Dar es Salaam na kwenda nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika nimalizie kwa kuipongeza Serikali kwa mradi wa DART, mabasi yaendayo haraka. Naipongeza Serikali kwa kuweza kutengeneza mradi mkubwa kama huu ambao umegharamia takribani bilioni 322. Hata hivyo, katika mradi huu bado kuna upungufu mwingi sana, kitu cha kwanza nilichokuwa naiomba Serikali ihakikishe kwanza lile suala la hisa. Suala la hisa halijakaa vizuri kwenye mradi huu, Serikali irudi iende ikaangalie kwa umakini jinsi gani ya utaratibu wa hisa. Vilevile nashangaa kwa nini mradi huu hauanzi? Mradi umetumia gharama kubwa sana, bilioni 322, uanze kufanya kazi ili wananchi waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna vituo ambavyo havijakamilika katika mradi huu, kituo cha Kimara pale mwisho, kuna kituo cha Ubungo Terminal, kituo cha Morocco, kituo kule Posta ya zamani. Vituo hivi viko wazi, ni hatari kama mradi utaanza ina maana watu watakuwa wanaingia kwenye mabasi bure. Naiomba Serikali sasa iangalie umuhimu wa kukamilisha vituo hivi na Serikali iwape fedha huu mradi uweze kukamilika ili uweze kutumika.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, naunga mkono hoja.