Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti ya Wizara hii muhimu, lakini pia nataka nikuahidi kwamba nitaenda hoja kwa hoja.

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa umeme nchini ipo katika sura mbili. Sura ya kwanza ni utekelezaji wa miradi mikubwa ya kuzalisha umeme lakini vilevile na miradi mikubwa ya kusambaza umeme. Sura ya pili ni kuunganisha umeme kwa watumiaji; ndivyo ilivyo hali ya upatikanaji umeme.

Mheshimiwa Spika, mimi nataka nijikite kule kwenye kuunganisha umeme. Hali ya kuunganisha umeme kwa watumiaji bado si nzuri; na siasa kubwa ya umeme kule kuwaunganishia watumiaji hali yetu bado si nzuri.

Mheshimiwa Spika, mimi kwenye jimbo langu vijiji vyote vimepata umeme lakini vitongoji takriban vyote havina umeme. Na bahati mbaya REA walikuwa wakishafikisha kwenye Kijiji wanalambisha umeme basi, kisha wanaondoka. Na kitu ambacho nashangaa hata zile scope nani alikuwa anaenda kukagua? Maana yake ni mtaa mdigo unalambishwa na kijiji kiwe tayari kina umeme.

Mheshimiwa Spika, kuna mambo mawili ambayo mimi nataka Serikali iwe bold. Suala la gharama ya kuunganisha umeme kwa 27,000 hebu Serikali ilijadili jambo hili, je, ni jambo la kiuhalisia? Maana sisi tumesema sana kwenye mikutano kwmaba umeme ni 27,000, lakini uhalisia siyo 27,000. Serikali iseme, kama inatakiwa kiasi fulani iseme kwa uhalisia wake. Wananchi wanajiunganishia umeme wanaweka ile connectivity ndani, kwa maana ya miundombinu, lakini akija kwenye kuunganishiwa 27,000 wanaambiwa kuna nguzo moja inatakiwa ije kwako inabidi utoe 300,000. Jambo hili wananchi wanashindwa kuelewa. Lakini mentality ya TANESCO inaangalia, kwamba kitongoji kile kina watu wachache na hivyo tukipeleka umeme hatina wateja. kwa hiyo kuna conflict hiyo.

Mheshimiwa Spika, mimi nashauri kuwe na muundo mathubuti, muundo wa kwanza REA iendelee na shughuli ya miradi mikubwa, iwe kama na sura ya TANROADS, lakini vilevile tuwe na Wakala wa Umeme Vijijini ambaye sasa ata-deal yeye na ku-connect kwenye vitongoji atafute nguzo atafute transformer ili kazi ya kuunganisha aifanye yeye; lakini anayehusika na wateja ni TANESCO.

Mheshimiwa Spika, TANESCO sasa yeye ni kuangalia namna gani anaweza kupata fedha baada ya wananchi kuunganishiwa umeme. Tukienda na muundo huu hali yetu ya upatikanaji umeme na kuunganisha umeme kwa wananchi itakuwa imekaa sawasawa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuwe na REA ambasyo itakuwa na sura kama ya TANROADS lakini tuwe na Wakala Umeme Vijijini ambaye atakuwa na sura kama ya TARURA halafu TANESCO yeye a-deal sasa na masoko, namna gani anaendesha Wananchi wapate huduma ile sasa ya umeme.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Serikali ikiwezekana wakati Waziri ana wind up tupate uhakika kwamba 27,000 inakidhi au 27,000 haikidhi? Kama kuna kiwango ambacho tunaona inafaa basi ipendekezwe na wananchi wataona kweli hiki kina uhalisia, lakini tunavyoenda hivi kila mmoja anamdanganya mwenzake, sasa hatuwezi kwenda na utaratibu huo.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ni kuhusu suala la nishati ya umeme katika maeneo mbalimbali (power mix). Private sekta inakuja na miradi kama ya solar kutaka iweze kuiuzia TANESCO umeme. Lakini mimi nataka niseme pamoja na sera yetu kusema hivyo lakini kuna uzito mkubwa sana. Ili kuja kupata mradi wa solar uiuzie TANESCO it takes ages, na ni ngumu kweli kweli. Sasa turuhusu watu waje tupate umeme wa kutosha watu waweze kujiunganishia. Lakini ni jambo gumu kweli kweli kwa mtu mwenye kutaka kuzalisha ueme lakini hata tariffs ambazo inatakiwa walipe haziendani na namna ambavyo wameweza kufanya kazi ya kuwekeza hili suala hilo; kwa hiyo nilikuwa naliomba hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ni kuhusu upatikanaji wa vifaa. Kinachosumbua tusiunganishiwe umeme vijijini ni kukosekana kwa transformer na kukosekana kwa nguzo. Haijulikani, na ndilo jambo gumu. Kule kwenye ofisi za TANESCO wanasubiri wapate nguzo, wanasubiri wapate Transformer, transformer hazipatikani. Sasa jambo hili kuna kipindi tulizuia hakuna transformer kutoka nje zitengenezwe hapa ndani. Sasa Mheshimiwa Waziri aje atuambie kama tunaruhusu transformer zije kwa wingi lakini na shida ni nini, nguzo tunazalisha hapa kwetu, na zenyewe nazo tulizuia kwamba zisitoke nje ya nchi kama inawezekana nguzo zije za kutosha za ndani ya nchi na hizo zitakazotoka nje ili kwamba kuwe na uhakika wa kupata nguzo, hapo ndiyo tutaenda kila kitongoji kitapata umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo lengo la Mheshimiwa Waziri, hata mwaka jana, alitaka vitongoji vyote vipate umeme. Lakini kuna uzito, hata hivi 15 bado ni vitone vya maji. Kwa hiyo, jambo hili nalo tuliangalie ni namna gani tunakuja na utaratibu madhubuti, kwanza kimuundo, kwa maana ya kuwa na wakala wa usambazaji wa umeme vijijini lakini REA yeye awe na sura nyingine ya TANROADS.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo jingine ni kuhusu usambazaji wa gesi. Mkoa ambao unakula mkaa kwa wingi ni Mkoa wa Dar es Salaam. TPDC wana mradi wa kusambaza umeme kwenye nyumba, lakini jambo hili nalo haliendi sawa sawa. Serikali iangalie, kama TPDC hawezi basi apatikane muwekezaji ambaye ataweza kufanya kazi ya kusambaza umeme. Kufanya hivyo tutazuia matumizi ya mkaa kwenda Dar es Salaam na tutailinda miti yetu. Kwa hiyo jambo hili nalo liweze kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine, nimepitia maoni ya Kamati. Kamati inaongelea habari ya kwamba TBS kwenye suala la vinasaba ipewe uwezo, ijengewe uwezo wa kutosha na ipewe muda ili iweze kuja na utaratibu wake. Jambo hili ni zuri; lakini kwa maana nyingine tena tayari tender imetangazwa kwamba ipatikane kampuni ambayo inaweza kufanya kazi ya vinasaba. Kwa hiyo kuna contradiction kati ya Kamati lakini mimi nachotaka kusema hali ambayo TBS ilichukua, ilichukua katika wakati mgumu sana na jambo hili TBS wamejitahidi. Sasa kama Serikali inaona ipo haja tuone kwa nini tunatoka tunamuacha TBS ambaye katupitisha kwenye kipindi cha mpito kama kuna mambo ya kurekebisha basi yaweze kurekebishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi mimi naipongeza sana Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Sisi sasa katika ukanda huu wa Afrika hasa hasa Kusini mwa Afrika tunaingia katika idadi ya nchi ambazo zina umeme mkubwa na tunaweza kusambaza nje. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. Wizara hii ni kubwa, ina mambo mengi na Wizara yenye mapambano mengi; lakini anafanya kazi kubwa na aendelee kufanya kazi kubwa ili kwamba Taifa letu liwe na umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)