Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niungane na Wabunge wenzangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wakati Waziri anawasilisha bajeti hapa nimeisikiliza kwa makini, wakati anawasilisha sikuona kuna mahala ametaja ma-‘bi’, bajeti hii imetajwa ni ma-‘ti’ na ma -‘ti’. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mama Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha nyingi za miradi katika Wizara hii ya Nishati ya ma -‘ti’ na ma -‘ti’. Tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tunampongeza Waziri January Makamba pamoja na Naibu wake na Katibu Mkuu pamoja na DG wa REA pamoja na Msaidizi wake na wote wanaotusaidia kazi katika Wizara hii January umeitendea haki Wizara hii unafanya kazi nzuri. Leo Wabunge wenzangu hapa wakati wanachangia wamesema hapa ilikuwa ipitishwe lakini Mheshimiwa Spika akasema kwa utaratibu ni lazima tuseme, tuchangie nakupongeza tena naungana na wenzangu kwa kazi nzuri chapa kazi. Wako watu ambao huwa najiuliza wanapokusoma namna fulani au mnamabifu huko mitaani? Hayo mabifu wayapeleke huko shughuli za Wizara umeiweza kweli kweli chapa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri nije kwenye maombi sasa kwa Jimbo la Makambako, nina maombi machache sana, kwenye Jimbo la Makambako nina maombi mawili, matatu. Ombi la kwanza kuna wale wawekezaji waliokuwa wanakuja kuwekeza umeme wa upepo, jambo hilo limechukua miaka zaidi ya kumi na nane, ishirini. Wananchi wale hawawezi kufanya jambo lolote na kufanya shughuli za maendeleo yeyote yale, nikushukuru walikuja walionana na Wizara yako na watalam wako walikaa, ulimwagiza Naibu Waziri alikutana nao, walizungumza lakini mpaka sasa hatujui kinachoendelea. Nikuombe wananchi wa Makambako Viongozi wanakuja hapa kesho, kesho kutwa watakuwa Bungeni hapa ukutane nao ili uweze kuwapa majibu lakini utakapokuwa unahitimisha kesho pia ni vizuri ukasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuna Kata ya Mlowa, Makambako pale ni Halmashauri ya Mji, Kata hii kimsingi ni vijiji lakini kwa sababu ni Halmashauri ya Mji hawa wanahesabika wanalipa gharama wananchi wa Mlowa kama mjini gharama za laki tatu na kitu. Ninakuomba tuma timu yako ya watalaam waungane na wasaidizi wako pale Makambako, wakaone hivi ni vijiji typical kabisa wanatakiwa kulipa gharama wanazostahili kulipa wanakijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu katika hilo kuna Kata ya Mahongole, kijiji cha Mpanga, tangu nguzo zimewekwa transformer sasa ni zaidi ya miezi saba haijawahi kuwekwa, ninakuomba wawekewe transformer watu hawa ili waweze kuungana na wenzao kupata umeme. Kwa hiyo, transformer haipo Mtanga, transformer haipo kijiji cha Mahongole, vijiji viwili havina transformer. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine wamezungumza Wabunge wenzangu hapa juu ya gharama hizi za umeme. Mimi nilikuwa nashauri kama mwananchi huyu kulipa gharama ile hawezi, kwanini wasikopesheke wawe wanalipa kidogo kidogo, badala mtu kulipa zile laki tatu kwa wakati mmoja? kwa sababu anahitaji kupata nishati awekewe zile gharama ambazo zinatakiwa kulipwa kila mwezi awe analipa kidogo kidogo mpaka tutapomaliza tutapata wateja wengi kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine Meneja wangu wa Mkoa wa Njombe wa TANESCO anafanya kazi nzuri sana pamoja na Wasaidizi wake ndani ya Wilaya, Meneja huyu hajathibitishwa na Makambako pale ni TANESCO Kiwilaya lakini anafanya kazi hajathibitishwa kama Meneja wa Wilaya. Kwa hiyo, nikuombe ili wafanye najua hata baadhi ya maeneo inawezekana hicho kitu cha namna hiyo, ninakuomba kama anazo sifa mimi nina imani anasifa, wathibitishwe ili waweze kufanya kazi kwa uhakika za kujituma kwa sababu ni watu ambao tumewaamini na ninyi mmewaamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine wananchi wa Njombe ambayo sasa umetuwasilishia bajeti hapa, kulikuwa na mradi ule unaitwa Ruhuji wa Njombe, ndugu zangu wa Njombe Serikali ya Mama Samia ikiongozwa chini ya Rais wetu na wasaidizi wake kijana mchapakazi January Makamba na timu yake zimetengwa shilingi huko ndiyo kwenye ma- ‘B’ sasa, zimetengwa shilingi bilioni tano na milioni mia mbili, Tunakushukuru sana mradi huu utawasaidia Watanzania, utasaidia Wananjombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika Njombe kuna Mradi Rumakali uko katika Mkoa wa Njombe Wilaya ya Ludewa huko nako zimetengwa shilingi Bbilionisita na milioni mia mbili na sabini, hiki kitu siyo kidogo! Ndiyo maana tunaposema Mama anaupiga mwingi anastahili sifani kwa sababu ya Ma- B na Ma- B yanayokwenda maendeleo katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa Mheshimiwa January wamesema wenzangu hapa mradi wa LNG ambao ulikwama kwa miaka saba leo Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan amekukabidhi kazi hiyo. Sasa mradi huu unakwenda kuanza, tunampongeza Mama, tunakupongeza January. Kwamba Watanzania sasa mradi huu ambao ulikwama walikuwa hawana imani sasa tayari wanakwenda, mradi huu unakwenda kuanza na kuwasaidia Watanzania. January Makamba chapa kazi, Mzee Makamba angekuwepo ningesema Mzee Makamba nikupe na zawadi kwa kumzaa kijana huyu, ana maono mazuri huo ndiyo ukweli, penye ukweli lazima tuseme ukweli. Ndiyo maana tunasema Mama amedhamiria Watanzania kuhakikisha anawapa maendeleo katika nchi nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye maji mambo ni Ma- B, ukienda kwenye barabara mambo ni ma-‘bi’, ukienda kwenye elimu mambo ni ma-‘bi’. Leo Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo Kamati hii, Kamati ya Bunge ya Nishati ilikwenda kule Bwawa la Mwalimu Nyerere, leo Wabunge Bwawa la Mwalimu Nyerere tumeliona hapa hapa Dodoma tumeliona Mheshimiwa Makamba tunakutakia kila la kheri na timu yako na Katibu Mkuu wako na Katibu Mkuu yuko imara, huo ndiyo ukweli na DG wa REA na timu yake tunawatakia kila la kheri Mungu ambariki Mama, tuendelee kumuombea achape kazi kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana lakini vilevile na wewe Spika umeliweza kusimamia Bunge tunakupongeza na wewe kwa kazi nzuri unayofanya. Mwenyekiti na timu yako tunawashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja kwa asilimia mia mbili.