Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ambayo ni mwanga wa nchi na uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu, maneno hayatoshi jinsi gani ya kumpongeza Rais kwa jinsi ambavyo ameamua kweli kututumikia Watanzania na kututoa hapa tulipo kutufikisha kwenye nchi ambayo ni ya asali na maziwa, kikubwa cha kumuombea ni uzima na afya njema ili malengo yake haya yatimie ya kuifanya nchi hii kuwa nchi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze Waziri na Naibu wake, vijana hawa wanamtendea Mama haki kwa sababu wanafanya kazi ile ambayo Mama anaitaka kwa weledi na kwa upendo na kwa uhakika mkubwa, ninawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, kichwa chako kimetulia mimi nakufahamu vizuri ni kichwa ambacho kinaweza kufanya mambo makubwa katika nchi hii. Nikutie moyo fanya kazi, sisi tuko nyuma yako tunakuamini na tutaendelea kukupa ushirikiano wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda leo mchango wangu ujikite sana TANESCO na TANESCO nataka niende kwenye suala la bei za umeme. TANESCO inafanya biashara ya umeme kwenye tariff lakini pia sehemu ndogo mimi ninaiita ndogo kwenye kuunganisha umeme. Kuunganisha umeme kwa shilingi 320,000 ni sehemu ambayo TANESCO inategemea iingize mapato, lakini watu wanaoweka umeme kwa shilingi 320,000 ambao ni watu wa mijini, rate yao ya kuweka umeme ni ndogo sana, kwa sababu ya gharama hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi ambacho ilitangazwa kwamba umeme uwekwe kwa shilingi 27,000 nchi nzima maombi ya kuweka umeme yalijaa TANESCO mpaka wakashindwa kufanya kazi lakini watu hawa ambao walipeleka maombi mengi ni watu wa mjini ambao wana matumizi makubwa ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona hii ni fursa ambayo tumeiacha, ni bora tungetumia gharama ya kuhakikisha tunaweka umeme kwa shilingi 27,000 lakini baada ya muda mfupi watu hawa wote wanatumia umeme na TANESCO wataingiza umeme kwa tariff kwa sababu watu wa mjini wana matumizi makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunaweza kupeleka umeme zaidi ya kilometa 200 kutoka kijiji kimoja kwenda kijiji kingine na tunafika kwenye kijiji kile kaya zitakazoweka umeme ni kaya labda 10,15 mpaka 20, kama Serikali hii inakubali hiyo gharama ya kupeleka huduma hiyo kwa wananchi tunaachaje kumuwekea mwananchi wa mjini umeme kwa shilingi 27,000 ambaye nguzo moja, kuna maeneo ambayo nguzo moja ya umeme inaweza kubeba mpaka mita 10,15 nguzo moja. Sasa hiyo nguzo moja kwa shilingi 27,000 ikabeba nyumba 15 maana yake watu hao wa mjini ndiyo wenye friji, ndiyo wenye nini matumizi ni makubwa na TANESCO itaingiza fedha nyingi sana kupitia tariff za hawa watu kuliko kuwawekea shilingi 320,000 halafu hawavuti umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunakusanya property tax kubwa sana nchi hii kupitia mita za umeme. Leo hata mtu aliyeko kijijini mwenye nyumba ya tembe akivuta tu umeme atalipa shilingi 12,000 kwa mwaka ya property tax kwa sababu atalipa shilingi elfu moja moja kwenye mita kila mwezi. Kwa nini tusitumie hii fursa ya kukusanya property tax kubwa kwa kuhakikisha watu wengi wanavuta umeme na ili watu wengi wavute umeme maana yake tukifanya shilingi 27,000 watu wote watavuta umeme. TANESCO watafanya kazi masaa 24 ili kuweza kuweka haya maombi yaweze kutimia kwa sababu watu wote wa mijini wataweka umeme na matokeo yake ni kwamba property tax itakuwa kubwa kwa sababu watu wote hawa watakuwa wanatozwa shilingi 12,000 kwenye mita zao kwa mwaka kwa hiyo mapato ya Serikali yataongezeka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tena katika hili ina maana hata tunaweza tukaweka asilimia kidogo ya hii property tax ikaenda REA kwa sababu REA wanaongeza watu wa kutumia umeme matokeo yake wanaongeza property tax kuwa kubwa, maana yake kama tukichukua hata percent tatu tu kwenye ile property tax ikaenda REA maana yake tayari tutakuwa tumeipa REA uwezo mkubwa zaidi wa kuongeza watumiaji wa umeme kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano hii inayoenda kwenye vitongoji maana yake vitongoji vitakwenda vingi kwa wakati mmoja kama REA ina pesa na kadri wanavyoingia maana yake property tax inaongezeka, mapato ya Serikali yanaongezeka. Hii ni win win situation ambayo ningeomba hii property tax angalau ipelekwe asilimia chache ziende REA ili mita nyingi ziongezwe kwa shilingi 27,000. Nyumba ni nyingi mjini tuko wengi milioni 61 na nyumba ni nyingi hii ni fursa ya kukusanya mapato ambayo tunaiacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri na TANESCO mkae muangalie hili suala la shilingi 27,000 liende nchi nzima ili watu waweke umeme wa kutosha tutapata mapato ya kutosha kwa TANESCO na tutapata mapato ya kutosha kwenye Serikali kupitia property tax. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye shilingi 27,000 kwa mfano mimi katika Jimbo langu, Iguguno ni kijiji, Nduguti ni kijiji, Makao Makuu ya Wilaya waliangalia geographical position hawajaangalia kwamba uchumi au wakaangalia kwamba sijui wana nyumba nyingi Hapana! Walichoangalia ni kwamba Nduguti ni katikati ya Wilaya ya Mkalama, hapa ndiyo patakuwa makao makuu lakini ni kijiji. Iguguno ni kijiji maisha ya wananchi ni ya kawaida ya kijijini. Sasa unapomwambia alipe shilingi 320,000 kuweka umeme ni kama ni kumnyima umeme tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wakati unalifikiria hili la kuweka nchi nzima shilingi 27,000 basi haya kwenye maeneo yetu ya vijijini kama Iguguno na Nduguti ianze mara moja shilingi 27,000 kwa sababu ni wanakijiji kama walivyo wanakijiji wengine ili kuweza kuvuta umeme katika maeneo haya. Kwa kuwaambia watu wa Nduguti, watu wa Iguguno wavute umeme kwa shilingi 320,000 ni kuwaambia wasitumie umeme jambo ambalo kwa kweli sidhani kama ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine hapo hapo kwenye hizi mita, TRA wanatumia kukusanya property tax kwa mita lakini sasa uzembe wao pia wanataka kukuponza Mheshimiwa Waziri. Wamekadiria vibaya nyumba zao. Kuna nyumba zinatakiwa zilipe zaidi ya shilingi 12,000 kwa mwaka. Matokeo yake hawakuwaambia mwanzoni wakakata shilingi elfu moja moja yakajilimbikiza madeni, leo wanashtuka wanakwenda kujaza kwenye mita madeni ya mwaka mzima, lawama zinakuja kwako Waziri, lawama zinaenda TANESCO kwa uzembe wa TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kushtuka kwa nini wasingeingiza hata kidogo kidogo kwa sababu wao wenyewe walikadiria hawakuingiza kwenye mita madeni yanavyotakiwa. Leo hii kuna watu wanakuja kukosa kununua umeme kwa sababu amewekewa deni la mwaka mzima ambalo siyo makosa yake ni uzembe wa TRA kwenye kuingiza. Leo inaingizwa kwenye mita wewe Mheshimiwa Waziri unaonekana wewe kwenye mita zako ndiyo kuna tatizo. Kaa nao TRA uzembe wao wasikuponze wewe kijana tunakujua ni kijana mwema, mchapakazi, uzembe wa TRA usiingizwe kwako Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tena hapo hapo, TANESCO wamekuja sasa wanakusanya madeni yao ya nyuma mengine ya miaka 20 iliyopita. Waliokuwa wanadaiwa wameshakufa wengine, hawa-exist. Leo hii wameshtuka sijui wapi linakusanywa deni mtu unashangaa kwenye mita unaambiwa unadaiwa shilingi 2,000,000, 1,500,000 mwananchi wa kawaida deni hujui lilikotoka. Nyumba zingine mtu alishafariki nyumba wanaishi wapangaji wengine hata hawajui kilichotoka unaambiwa mnatakiwa mlipe deni. Naomba Mheshimiwa Waziri hili jambo TANESCO mkae chini muangalie upya namna ya kukusanya madeni, kuna madeni mengine yanatakiwa yafe tu. Mtu miaka 20 mlikuwa wapi siku zote?

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Isack.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba nimalizie kwa kusema kwamba TANESCO hili jambo waliangalie vinginevyo itabidi watu wengine wako tayari kushtaki, wanaenda EWURA kushtaki kwa jambo ambalo linaweza kukaa chini na kuzungumzika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)