Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Nishati ya Ndugu yangu Mheshimiwa January Makamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kwenye mchango wangu naomba nichukue fursa hii kwanza kabisa, kwa kipekee kabisa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mama yetu, Mama wa Watanzania, Mama mpenda maendeleo, Mama la Mama, Mama mwenye mvuto kati ya Marais wanawake Duniani, kwa kazi kubwa sana ambayo Dkt. Samia Suluhu Hassan anaifanya kuhakikisha kwamba Taifa letu linaendelea na linakuwa la mfano Barani Afrika na Duniani kwa ujumla.

Mheshmiwa Mwenyekiti, mama yetu anaupiga mwingi, Mama yetu anaonesha mapenzi na mahaba makubwa kwa Watanzania, Watanzania fuatilieni mambo anayoyafanya Doctor Samia Suluhu Hassan, muone upendo anaounyesha kwetu na sisi Watanzania kazi yetu iwe ni kumuombea inshallah na kumuhakikishia kumuombea ili Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya aweze kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nipende kumshukuru na kumpongeza January Makamba, yule Mtoto wa Yusuf Makamba Waziri wa Nishati na Kaka yangu Byabato - Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mkurugenzi wa REA na Wakurugenzi wote wanaoendesha taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Nishati, hawa watu wanafanya kazi kama nyuki. Kama ni mpira uwanjani wanapeana pasi, wanapiga magoli tu na ndio maana tunaona hii Wizara ya Nishati ndugu Watanzania, tunaona Wizara ya Nishati hii kuna ubunifu mwingi sana ni kwa sababu kuna master minder January Makamba ambaye ameonyesha ubunifu mkubwa katika kuendesha Wizara ya Nishati hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania ni mashuhuda, Watanzania wanafahamu kwamba mwaka 2010 lilitokea jambo kubwa kwenye historia ya nchi yetu. Wataalam wetu wa TPDC wakishirikiana na jopo la watalaam lililotoka nje ya nchi, walifanya utafiti na kugundua uwepo wa gesi asilia kubwa sana kwenye bahari iliyopo ndani ya Taifa letu. Ugunduzi huu umeiweka Tanzania kwenye sura ya dunia na kutufanya sasa Tanzania tutambulike kama Taifa ambalo lina gesi asilia safi duniani ukilinganisha na Mataifa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Doctor Samia Suluhu Hassan ambaye baada ya kimya kirefu cha muda wa miaka saba Rais wetu ameona sasa ni muda muafaka tuweze kuendeleza rasilimali yetu hii ambayo Mwenyezi Mungu ameweza kutupatia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Watanzania wote tuweze kuelewa dhamira nzuri ya Rais wetu nasi Wabunge na Wananchi wa Jimbo la Ngara tunawaunga mkono, tunamuunga mkono Rais, tuna muunga mkono Waziri na timu yote ya Wizara ya Nishati na madini, nendeni mkawekeze kwenye eneo hili la gesi asilia. Wekeni fedha za kutosha ili Watanzania tuondokane na adha mbalimbali ambayo tumeipata kutokana na kutumia nishati chafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamkini tokea asubuhi wazungumzaji wameelezea nishati chafu, watu wanafikia hawajaelewa vizuri, naomba sasa mimi niwaambie Watanzania, tunaposema nishati chafu, tunazungumzia matumizi ya kuni, mkaa na matumizi ya mafuta ya taa kwenye kupikia. Kuna mahali katika nchi hii kuna wanaume walikua hawatoi mahari maana wanafahamu kwamba mabinti wazuri wanakwenda kutafuta kuni mbali. Anachokifanya yeye anajipanga binti ameenda kutafuta kuni mbali, jioni anambemba mgongoni ameshaoa na mahari hatoi. Sasa, hii kazi nzuri inayofanywa na January Makamba ya kutuleta nishati safi inaenda kuwafanya kina mama sasa wasiende kutafuta kuni mbali na wale waliozoea kubeba, sasa inakwenda kuwa mwisho. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ukombozi mkubwa sana kwa wakinamama wa Tanzania waliokuwa wanapata adha kwenda huko porini kutafuta kuni, sasa hawatofanya hivyo, watapata nishati safi na wataweza kuitumia. Kuna Watanzania kutokana na macho yao yanaathiriwa na moshi, maeneo kama ya Kanda ya Ziwa baadhi ya wazee vikongwe waliuliwa wakitwa ni wachawi kwa sababu wanapikia kuni na matokeo ya zile kuni ni ule moshi wenye carbon na kemikali nyingi zinaua macho yao yanakuwa mekundu. Watu walipigwa panga kwa sababu ya nishati chafu! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunamuona Rais yuko mbele, leo hii tunamuona Waziri yuko mbele, wanakwenda kuwaokoa Watanzania kutoka kwenye hiyo adha ambayo tulikuwa tukiipata. Naomba Watanzania waelewe tunaposema nishati safi ni kuondokana na hii adha ya kutumia nishati chafu ambayo imegharimu maisha mengi ya Watanzania. Achana na hilo, muda tu kina mama waliokuwa wanaupoteza kwenda kutafuta kuni ulikuwa ni muda ambayo kwa sasa badala ya kwenda kutafuta kuni ulikuwa ni muda ambao kwa sasa badala ya kwenda kutafuta kuni sasa watautumia kwenye uzalishaji mali na wataweza kuongeza tija katika uwekezaji na kazi wanazozifanya kwenye familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, achilia mbali macho mekundu, achilia mbali kupoteza muda, achilia mbali watu kutumia fursa hiyo kubeba mke hata bila kutoa mahari, njoo kwenye suala la uharibifu wa mazingira. Miti imekatwa kweli kweli, watu wanafanya nishati chafu kama chanzo cha biashara. Kuna mtu yeye kazi yeye yake tokea awe mtu mzima miaka 18, yeye ni kukata miti na kuchoma mikaa na kuuza mikaa, ameharibu vyanzo vya maji, wameharibu misitu, matokeo yake Dar es Salaam sasa hivi kuna kipindi tunaingia kwenye crisis ya ukosefu wa maji kwa sababu miti mingi imekatwa kwenye Mto Ruvu ambapo maji ndiko yanapozalishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia na huu mradi wa LNG unakwenda kuokoa Watanzania. Ninawaomba Wizara ya Nishati, endeleeni mbele, wekeni hela ya kutosha katika hilo eneo, Wabunge tunawaunga mkono kwa sababu tunafahamu jambo zuri mnalolifanya kwa ajili ya Watanzania. Tunakuomba Mheshimiwa Makamba usirudi nyuma kwa watu wanaopiga vijembe huko vijiweni ambao hawaelewi, mimi hapa ni Mwakilishi wa wananchi, nimesimama kuelezea faida kubwa za Mradi huu wa LNG kwa Taifa. Ninaomba Watanzania waweze kutuelewa, dhamira nzuri uliyonayo Mheshimiwa Waziri sisi tunakuunga mkono, endelea moja kwa moja, usirudi nyuma, weka fedha za kutosha, wote tutapitisha miradi hii iende ikatekelezwe iweze kutusaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa REA tunakushukuru Mheshimiwa Waziri umefanya kazi kubwa sana. Tunafahamu Tanzania ina vijiji zaidi ya 10,800. Kati ya vijiji 10,800; vijiji zaidi ya 10,000 vimeweza kuwashwa umeme vimebaki vijiji vichache nchi nzima. Hii kazi ambayo umeshaifanya Mheshimiwa Waziri ni kubwa na ni nzuri na inatambulika kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mkoa wa Kagera Mkandarasi anaendlea vizuri. Amepeleka nguzo maeneo yote ambayo yanahitaji umeme. Hata kule kwangu Ngara Mheshimiwa Waziri tumejipanga kuanza kuwasha umeme kijiji kimoja baada ya kingine mara tu baada ya Bunge hili kuisha. Nichukue fursa hii Mheshimiwa Waziri nikukaribishe uungane nami twende tukawashe umeme Murusagamba. Murusagamba tokea Mwenyezi Mungu awaumbe hawajawahi kuona umeme. Ni sasa hivi wewe Mheshimiwa January Makamba umetuletea mkandarasi, mkandarasi amepeleka umeme kwenye taasisi na hivi tunavyozungumza tunashirikiana kufunga umeme kwenye vijiji. Tuende tukawawashie umeme Murusagamba na maeneo mengine ambayo wanahitaji huduma ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mradi wa densification Mheshimiwa Waziri. Kwa unyenyekevu mkubwa nikuombe kule Ngara nisaidie angalau niongezee vitongoji hata 10 kwa neno lako tu Mheshimiwa Waziri unaweza ukanipa vitongoji hata 10 Mheshimiwa Waziri. Kule kwangu Mheshimiwa Waziri sijui ilikuwaje sijui ni typing error badala ya kuniandikia vitongoji 50, waliniandikia vitongoji vitano. Sasa nikajiuliza ndugu yangu sasa huyu January Makamba nini tena hii? Nikasema sasa Mheshimiwa Waziri leo nikuombe kwa unyenyekevu mkubwa niongezee kidogo pale nipe hata 20 viongezwe kwenye vile vilivyopo ili Mheshimiwa Waziri vile vitongoji ambavyo vinahitaji huduma ya umeme na vyenyewe tuweze kuvipelekea umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri utakumbuka ulipokuja Ngara kutembelea mradi wetu wa Rusumo nilikuomba unisaidie kwenye mitaa 17 ya Rulenge ambayo haina huduma ya umeme kabisa, ile ni mamlaka ya mji lakini ile mitaa yake yote ni vijiji. Mheshimiwa Waziri nilikuelezea kuhusu hili, ninakushukuru ulituma Wataalam wakaja wakakagua pale wakakuta kweli vile ni vijiji vinatakiwa kuhudumiwa. Kwa unyenyekevu mkubwa naomba unisaidie tena vitongoji vyangu hivi 17 vya Mamlaka ya Mji Rulenge viweze kupata huduma ya umeme angalau mimi niogelee inapofikia 2025 Mheshimiwa Waziri nafikiri unajua nachokimaanisha ni nini. Nikipita pale iwe ni shangwe na vigelegele wala hakuna maswali mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri endeleeni kuchapa kazi. Watanzania wanaona kazi nzuri mnazozifanya, sisi ni mashuhuda wa mambo makubwa mnayoyafanya, tunawaunga mkono wewe na timu yako yote, Mwenyezi Mungu awabariki awape afya njema muendelee kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya ninaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)