Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Silvestry Fransis Koka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara hii muhimu, Wizara ya Nishati ambayo kwetu na wananchi wetu ni huduma muhimu lakini ni siasa kubwa katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Wizara pamoja na watumishi wote na Mashirika yanayohusiana na Wizara hii, kwani wamekuwa wakiendelea kufanya kazi nzuri ya kutoa huduma hii kwa wananchi wetu. Katika Jimbo letu la Kibaha Mjini au Mji wa Kibaha ni Mji unaokua kwa haraka, lakini ni Mji ambao pembezoni mwa Mji huu kuna maeneo mengi ambayo bado yako katika mfumo ule wa REA na hakikia wananchi wake wengi hawawezi ku-afford kufungiwa umeme kwa ile gharama ambayo siku zote wanachaji ile ya Mjini ya kati ya shilingi laki tatu na ishirini mpaka laki tatu na Hamsini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Wizara kwa sababu siku za karibuni Waheshimiwa Wabunge tuliombwa tuainishe yale maeneo ambayo hakika hawawezi kufikia gharama hizo ili waingizwe katika utaratibu wa REA wa kulipa shilingi 27,000 na kuweza kufungiwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wangu wa Kibaha, maeneo hayo ni pamoja na Mbwawa, Hekani, Kichangani, Kidugalo, Miomboni, Ghaza, Jerusalemu, Mtaa wa Vitendo, Zogoale, Saenii, Yonuga, Simbani, Sagale, Muheza, Mbwate, Bungo, Kokotimiza, Pumba, Galagaza, Rulanzi, Mwanaugali na Mwale vilevile Mkombozi na Lumumba. Maeneo haya tulikwisha yawasilisha REA na tayari tulikwisha ahidiwa kwamba utaratibu unafanyika ili na wenyewe waunganishwe katika ule utaratibu wa REA waweze kufungiwa umeme kwa hii gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Wizara au kwa Serikali, sasa utaratibu ufanyike wa haraka kupitia bajeti hii ili wale wananchi wanaosubiri kupata huduma hii waweze kufungiwa umeme huu na wenyewe waweze kunufaika na kufurahia matunda ya kazi kubwa yanayofanywa na Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara hii kwenda kuwapelekea wananchi umeme wa bei nafuu, kwa maana mbali na kazi za kiuchumi, mbali na kwamba umeme ni biashara lakini kimsingi kwa wananchi hawa ni huduma kubwa kwao ambayo inakwenda kuwakomboa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi wa kusafirisha umeme kutoka Kinyerezi hadi Arusha ule wa Msongo wa KV 400. Nafahamu Serikali ilikwishafanya jitihada ikawalipa wale wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa kupisha mradi huu, lakini bado kuna wananchi ambao hawajalipwa na wananchi hawa hawajalipwa kwa sababu maeneo yao yalihesabiwa chini ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha sasa malipo yalipofanyika taasisi za Serikali ziliwekwa pembeni au zilisemekana kwamba zitachelewa kulipwa wananchi walipwe kwanza, lakini kimsingi kwa maana ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuna wananchi wengi ambao maeneo yao bado yalikuwa chini ya Halmashauri kwa sababu ya kiumilikaji na hadi leo bado hawajaweza kupata fidia, kwa hiyo wamekuwa wakinung’unika wakati wenzao tayari walikwisha pata fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Wizara kwa Mheshimiwa Waziri kabla hatuja-wind up kesho, basi ningeomba Wizara itoe tamko ni namna gani hawa na wenyewe wanakwenda kupatiwa fidia ili sasa na wenyewe waweze kuwa sawa na wale wengine ambao tayari walikwishapata fidia kwa kupisha mradi huu wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba Shirika letu la TANESCO ni kubwa na linahitaji ufanisi mkubwa, tunafahamu utawala una mikakati ya kufanya transformation kubwa au mabadiliko makubwa ya kimuundo lakini kiutawala na kiutendaji. Mimi naunga mkono jambo hili kwa sababu ndiyo njia pekee ya kuendesha shirika hili kisasa, tunafahamu wazi katika kwenda kulitekeleza hili zitatokea fursa nyingi kwenda katika sekta binafsi na ndiyo mtindo wa kisasa wa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi mahali popote Duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ombi langu kwa shirika hili au kwa Wizara, tunaomba sana wakati wanaenda kufanya mabadiliko haya kipaumbele cha kwanza au watu wa kwanza kufikiriwa ziwe ni kampuni za nyumbani kwa maana zisimamie ipasavyo local content ili makampuni ya ndani ya nchi ya wazawa waweze kupata nafasi ya kushiriki katika kazi hii au shughuli hizi kubwa zitakazotokana na mabadiliko ya kiutendaji na kiutawala ambayo yatakwenda kufanywa na shirika hili la TANESCO, ili tija ile isiishie tu kuliboresha Shirika lakini tija ile vilevile iweze kwenda kwa makampuni yetu, wananchi na hatimae kupeleka uchumi kwa wananchi wengi kama wanavyosema wenzetu waingereza kwamba tuwe na ile economical multiply effect kwenda chini kwa Watanzania wengi ambao watashirikishwa katika utaratibu huu wa kwenda kufanya transformation katika shirika letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuipongeza Wizara hakika tulisharudi nyuma sana kwa kuacha kuchukua nafasi ya awali kwenda kujenga ile LNG plant kule Lindi. Tulianza vizuri na watu walichangamka kweli kweli, Mtwara ilichangamka, Lindi ilichangamka na hata wawekezaji wa ndani na nje walifanya kazi kubwa ya kuanza kuwekeza katika maeneo haya, lakini baadae kwa bahati mbaya tukasuasua wenzetu wa Msumbiji wakaenda mbele, lakini nina imani kwa mkakati tulionao sasa siku si nyingi mradi huu mkubwa kupita miradi mingi ambayo imekwishafanyika hapa nchini unakwenda kutimizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kwamba kwa kuwa tumekwishaamua tusirudi nyuma kwa maana nishati hii tayari inakwenda kuwa muhimu sana katika matumizi mbalimbali Mjini, lakini inakwenda kutuondolea adha kubwa ya kutumia nishati ambayo inatuathiri kimazingira na hususan ukataji wa miti pamoja na matumizi ya kuni na mkaa ambayo inakwenda kutuathiri katika ustawi na upatikanji wa mvua na hatimae kufanya nchi yetu ipatwe na janga la kiangazi. Kwa hiyo, ombi langu na ushauri wangu ni kwamba kwa kuwa tayari kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri tumekwisha fikia mahali pazuri basi niombe Serikali na yenyewe iendelee kuweka nguvu ili mradi huu uweze kufanyika na uweze kukamilika ili matunda yake tuweze kuyaona ndani ya nchi na hata kwenda chini kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ulikuwa ni huo na niunge mkono hoja. (Makofi)