Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani ya hotuba ya Wizara ya Nishati. Kwanza nianze kutumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa hakika tumekuwa tukisema kwamba, hakuna kilichosimama na hilo limedhihirika kwa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao sasa umefikia asilimia 86.89 na kwa kweli tunaimani kubwa kwamba, ule muda uliowekwa wa kukamilika Juni 2024 tunakwenda kuingia kwenye historia nyingine katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendela kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wananchi wa Mkoa wa Mtwara habari ya mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia tulishasahau na tukajikatia tamaa, kwa sababu kwenye bajeti ya mwaka jana ni kama hatukuiona hivi, lakini kwenye kitabu cha bajeti ya mwaka huu kwa maneno yaliyoandikwa na hotuba ya Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Mtwara kwa sababu shughuli ya gesi asilia ilikuwa imelala kwa miaka hii yote, tunaendelea kuwa na matumaini makubwa sana na Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hakika wananchi wa Mtwara na Watanzania wengine wote kule Mtwara mlitukimbilia sana, watu walijenga hoteli, walifungua shughuli mbalimbali za kibiashara lakini baada ya kuona huu mradi kama umekwama waliondoka, kwa hotuba ya leo tunaamini Watanzania watarudi Mtwara kwa sababu nimeuona mradi upo kwenye kitabu na nitakuja kusema mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kwa nia njema. Lakini kipekee nimpongeze kwa usikivu, unyenyekevu na kuchukua hatua. Kwa nini, nitasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika Mkoa wa Mtwara ninapoitumikia nafasi yangu ya uwakilishi. Tunazo changamoto mbili kubwa, ya kwanza ni upatikanaji wa umeme, kwetu sisi imekuwa ni changamoto kubwa sana. Mkoa wa Mtwara, Mheshimiwa Mbunge aliyekaa sasa hivi anasema kwao kunakatika katika umeme, lakini nitamkaribisha aje Mtwara, alikuja kwenye shughuli moja ya kikazi, Mtwara ndiko mahali ambako umeme kwa siku unaweza kukatika mara 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua nguvu ya umeme na kwa kukatika huko hakuna shughuli za kiuchumi ambazo zinaendelea vizuri, wajasiriamali wadogo wamekuwa wakilalamika, wanaotunza samaki kwenye friji, wanaofanya shughuli za uchomeleaji, yaani wajasiriamali wote ambao wanatumia umeme wamekuwa wakitoa kilio kikubwa sana. Matokeo yake inasimamisha mtiririko ule wa shughuli za kiuchumi kwa sababu mambo yanasimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitangulia kusema hapa, Mheshimiwa Waziri ametuambia, na kwenye kitabu chake cha hotuba mimi nampongeza kwa sababu ameweka hoja mahsusi kwa Mkoa wa Mtwara, ametujibu kwamba tutasubiria kwa miezi mitatu (siku 90) lakini kwa hatua za awali tumeona na tumemsoma. Ninaamini pia tutaanza kuona hayo matokeo ya kukatika katika kwa umeme mwishoni mwa mwezi Juni, tuna matumaini, tunamwomba Mwenyezi Mungu atuweke mpaka Desemba ili tuone na tuthibitishe kwa vitendo hayo ambayo ameyasema kwenye hotuba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ukiacha changamoto nyingine, lakini kwetu sisi nishati ya umeme ni changamoto. Tunaamini Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu na kwa kuwa imedhamiria kutuondolea hii changamoto hata yale madai niliyokuwa nayo ya wananchi ya kuunguziwa friji, TV na vitu vingine, ninayaweka nyuma nisubiri suluhisho ambalo limetolewa na Mheshimiwa Waziri na kwamba ninaamini tutakwenda kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya pili ni upatikanaji wa umeme vijijini katika Mikoa ambayo vijiji vyake bado havijafikiwa kwa asilimia 50 kwa Mradi wa REA unaoendelea sasa ni Mkoa wa Mtwara. Tunao Wakandarasi wawili NAMES pamoja na Central, mmoja anaendelea vizuri lakini huyu mwingine anasuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina shaka kuwa Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi itafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Nishati zikiwemo pia na changamoto ambazo tunakumbana nazo za Mkandarasi wa Mtwara, hili ninaamini kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri unalichukua na umelipa kipaumbele na ndiyo maana umeweka mkakati wa muda mfupi na muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tusiendelee kusubiri vile vijiji 200, 300 ambavyo pengine Mkandarasi anasema anavifanyia kazi tukasubiri mpaka Desemba; tunaamini deadline ni Desemba lakini basi tuanze kuona hayo matokeo, ikishindikana hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria, yaani suluhisho litakuwepo tu. Waitwe watu wengine waje kufanya kazi ambayo mkandarasi ameshindwa ili na sisi kwenye hivi vijiji, mnajua Mtwara tuna ardhi kubwa, tuna msitu mnene, tupate umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kule kwetu, hasa maeneo ya Newala, ukiona mahali kunawaka taa wanasema kwa Ali Ma-solar, yaani ni kwamba tumezoea kwenda dukani kununua ile panel ndogo na kuweka kwa sababu umeme bado haujafika vijijini. Hizo ndizo changamoto kubwa ambazo tukitatuliwa na Serikali kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ametuahidi, tutakwenda kupona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshukuru sana, kwa mara ya kwanza najaribu namna ya kurudisha sauti yangu, ninaishukuru Serikali na ndiyo maana nilimpongeza Mheshimiwa Waziri, nimeona maeneo kadhaa ambayo Mkoa wa Mtwara umetajwa. Kwanza ni huu mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa megawati 300 kutoka Mtwara, na wote tunajua. Ndiyo maana Mtwara kwa maana ya gesi ya Madimba iko kwenye chanzo kimoja wapo cha umeme katika nchi hii. Sasa lililonipa faraja ni kwamba Serikali itaanza kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha eneo la ujenzi wa kituo na mipaka ya Mkuza kuanzia Mtwara kwenda Somanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba muanze sasa, ukimaliza bajeti hamia kule Mzee, ukaanze kuwaambia wananchi wa Mkoa wa Mtwara namna ambavyo huo utaratibu mzima wa kulipa fidia na kwenye maeneo yote ambayo tunaweza tukanufaika ili kuepusha ile migogoro wanasiasa tutakaporudi kule tuambiwe mbona hakuna kitu. Kwa hiyo, ukitangulia utakuwa umeturahisishia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG). Hapa niseme kwa dhati ya moyo wangu kwamba, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amerejesha matumaini ya Wanamtwara kwa asilimia 100. Hii gesi ambayo huko nyuma ilituletea vilio na kutupatia misiba, lakini sasa Mama tunasema ahsante kwa sababu tunajua kurejeshwa kwa huu mradi kwetu utakuwa ni furaha na matumaini ya pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo tunajua sasa hata zile Wizara nyingine ile Miji ya satellite ambayo tulikuwa tunaiona itakwenda kutekelezwa, Mheshimiwa Waziri wale watu wa Madimba na maeneo yanayotoka kule nendeni mkaone namna ambavyo mtawatia moyo hata kabla hamjafika hatua ya mbali kwa kuboresha shughuli zao za kijamii, shule, vituo vya afya, zahanati na nyumba zao pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo nilipata nafasi ya kwenda kwenye nchi ambayo inazalisha gesi wanaiita Trinidad and Tobago tuliona. Tunatamani kuona manufaa kama ya nchi hizo ambazo wamekuwa wakizalisha gesi kwenye maeneo yao, mabadiliko yale ya haraka ya kimaendeleo tunayapata na kule kwetu Mtwara kwenye maeneo ambayo gesi inatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kuna eneo la kwenda kuwaelimisha wananchi na hapa tumeambiwa jitihada mahsusi itawekwa katika Mkoa wa Mtwara. Mheshimiwa Waziri mimi naona kama utakuwa unachelewa, kwamba tusubiri mpaka Julai 01, lakini naomba wakati unapokwenda kufanya hili litakuwa kwetu la heshima sana kwa sababu wananchi wa Mkoa wa Mtwara sasa wataelimishwa namna ambavyo wao watashiriki na kunufaika na huu mradi ili sasa tusiwe wasikilizaji na ndugu watazamaji. Tunataka sisi tushiriki kikamilifu ili tuweze kwenda pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la mradi ambalo kwenye kitabu cha hotuba nimeona linalotupa faraja ni usambazaji wa gesi asilia ambao unatekelezwa na TPDC ambao sasa umefika asilimia 60 na utakamilika Juni, 2023. Hapa tumeambiwa kwa kuanzia Mkoa wa Mtwara ndiyo umeanza na nyumba 209 zitakuwa zimefikiwa. Tunakusihi sasa ukiweka tu kwenye nyumba hizi 209 lakini tunajua Mtwara ina Wilaya zake Tano za Serikali na za Kichama Sita na huko hatujawahi kuwa na viwanda hata vidogo kwa kutokuwa na umeme wa uhakika, tusipopata hii miradi ya gesi kwenye taasisi za umma kama vile shule, hospitali, vituo vya afya na kwingine kote kunakohitaji, bado kwetu manufaa tutachelewa sana kuyafikia, ninakusihi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waliosoma zamani kama jirani yangu hapa, kwenye shule zao za sekondari walikuwa wanapika kwa gesi. Hivyo, kwa nini sasa hivi wananchi wakakate marundo ya kuni kule. JKT, Shule za Sekondari, Shule za Msingi, Vituo vya Afya, Magereza na maeneo mengine. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Agnes.

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)