Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu ya Wizara yetu ya nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kutujalia uzima kukutana jioni ya leo, pili, kama ambavyo wamepongeza wengine, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake kuifanya sekta hii sasa angalao tunaona tunaenda, hii inaonesha wazi kwenye miradi mbalimbali ambayo tunaisimamia, ukiwemo mradi mkubwa wa Mwalimu Nyerere ambao utaweza kutotolea megawati 2,115 ambazo zitaweza kusambaza umeme katika nchi nzima. Kwa hiyo, jambo hili ni kubwa, linastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Ndugu yangu Mheshimiwa Januari Makamba pamoja na Naibu wake Ndugu yangu Mheshimiwa Byabato, Katibu Mkuu pamoja na Wakuu wa Taasisi wote walioko kwenye Wizara hii ya nishati. Wanafanya kazi nzuri, tunaona kazi zao, tuna-enjoy kazi zao na kwa hakika wanatupa heshima kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kama ambavyo tumesema tunaona tunaelekea vizuri kwenye miradi ya REA - umeme vijijini. Tumeambiwa na Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake asilimia karibia 82 sasa tuna-cover nchi nzima. Ni jambo zuri tunaona tunabakia kama na asilimia 18. Asilimia 18 inaonekana kuna miradi iko kazini, iko on progress kitu ambacho ni kizuri sana. Nataka nishauri tu mfano kwenye Jimbo langu la Singida Mashariki nilikuwa na ugomvi mkubwa na Wizara yako Mheshimiwa Waziri, nilikuwa na tatizo la Tarafa nzima ya Mungaa. Tarafa nzima ya Mungaa ilikuwa haina umeme hata Kijiji kimoja katika vijiji vile 26 leo ninavyoongea vijiji vyote vimewekewa nguzo na asilimia 40 viemshawashwa umeme. Maana yake ni kwamba, tunaona dalili njema na sisi ya kuonja keki ya Taifa kwenye upande wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikuhakikishie kwamba, tutakapofika mpaka Disemba kama Wakandarsi wataenda hivi, tunaamini tutamaliza vijiji vyote vilivyobaki. Hilo nalisema kwa sababu, kuna Tarafa ya Ikungi ambayo ilianza kupata umeme ilikuwa ina tatizo la baadhi ya vijiji kama Ng’ongosoro, Matongo, pamoja na pale Mwanjiki, hivi ninavyoongea saa hizi hatuna ugomvi na wewe umeme unaenda kuwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja yangu ni ambayo tunaisema wote hapa, tunaenda kumaliza vijiji Mheshimiwa Waziri, tuna tatizo la vitongoji. Nikuombe sana vitongojini ndiko waliko wananchi. Nikuombe sana huo mpango ambao umesema angalao vitongoji 15, Mheshimiwa Waziri havitoshi, tutakuwa na kelele kubwa sana. Nikuombe sana kama utaweza unapokuja ku-wind up hapo kesho utueleze namna ambavyo utakuwa na mipango ya muda mfupi ya kuongeza angalao ili tuweze kuvifikia vitongoji vingi kwani vitongoji hivyo ndiko waliko watu, ndiko ziliko kaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilometa mbili ambazo tulikuwa tunapata hazitoshi kwenda popote, ninaamini zinagusa maeneo machache sana. Kwa hiyo, kwa sababu umeme kila mmoja anapouona anatamani na kwake upatikane. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, ninajua wewe ni msikivu, ni kijana mwenye nguvu, Mheshimiwa Rais amekuamini, hebu simamia hii sekta. Wananchi wa kule kijijini nao waweze kupata umeme kama ambavyo wengine wanapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumaliza eneo hili nihamie kwenye eneo la mambo kama matatu ambayo ni mahsusi nataka niyaeleze. Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hili la umeme wa maji tumekuwa tukisema tunaongeza uwezo, lakini tumeona umesaini mkataba juzi wa umeme wa jua pale Kishapu ni jambo zuri sana, lakini tumekuwa na kilio cha muda mrefu cha umeme wa upepo. Umeme wa upepo tumezungumzia Makambako, tumezungumzia Singida, hivi ninavyoongea kuna watu wameonesha nia ya kuweza kuwekeza, lakini mpaka sasa bado hatujaona dalili yoyote ya kuanza kwa umeme huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wenye uhakika ambao hautakuwa unaangalia tabianchi, ninaamini kabisa tukiongeza kwenye gridi ya Taifa umeme wa upepo naamini kabisa uta-cover nchi yetu vizuri. Nikuombe sana unapokuja utuambie mipango mahsusi ya Wizara yako na wewe tunakuamini unaweza kuongeza hili jambo na kuongeza speed pale tulipokwama. Kumekuwa na siasa nyingi, naomba hizo siasa tuziondoe, tuhakikishe kama mradi ule wa Singida uanze mapema ili tuweze kuingiza kwenye Gridi ya Taifa wakati tunasubiri vyanzo vingine. Ninaamini hili utalifanya na litatuongezea uwezo mkubwa wa kusambaza umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili kwenye eneo la kiwanda. Kiwanda ili kiweze kufanya kazi, kwa maana naongelea Shirika la TANESCO, lazima uwe na vitu kama mitambo na mashine na technology, jambo la pili lazima uwe na fedha za kuwekeza ambazo tunazitafuta wote, tatu ni rasilimali watu. Ukishakuwa na rasilimali watu yenye furaha, yenye motisha, yenye kupewa support muda wote, utafanya kiwanda kifanye kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimemsikia Mheshimiwa Mkundi amesema asubuhi, kumekuwa na manung’uniko kidogo, kwa upande wa wafanyakazi wa TANESCO, kumekuwa na dalili ya kwamba, mnaweza mkapunguza wafanyakazi. Leo hii Shirika unao wateja milioni nne nchi nzima katika nchi yetu, lakini unao wafanyakazi 9,900 tu wastani wa mfanyakazi mmoja anahudumia wateja 424. Maana yake ni kwamba, kuna mfanyakazi mmoja anahudumia wateja wengi sana, maana yake huwezi kutegemea tija pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo unapotaka kwenda kupunguza wafanyakazi maana yake unaenda kupunguza uwezo wa kuwahudumia wateja ambao leo tunasema tuende vijijini tukaongeze idadi ya wateja wetu. Usitegemee kupata ufanisi kama hili jambo lipo kweli na tumeendelea kupata taarifa kwamba mnaendelea kupita kwenye Mikoa kuwaambia kuna mpango wa kupunguza, mfano kama Mkoa wa Ilala wa ki-TANESCO, kuna wafanyakazi 288 unasema utabakiza wafanyakazi 86, unategemea uta-cover vipi huduma pale katika Mkoa wa Ilala? Mkoa wa Dodoma kadhalika una wafanyakazi 162, unategemea wabaki 86, watahudumiaje wateja wa Mkoa huu? Maana yake ni kwamba, unaenda kuanguka, unaenda kufeli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Mheshimiwa Waziri najua hili huna taarifa, kumekuwa na fukuto ndani kwa ndani linaendelea kwenye Menejimenti, lifanyie kazi, waite kama Vyama vya Wafanyakazi mzungumze ili muwafanye wafanyakazi hawa waendelee kufanya kazi ambayo tunaitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana niongelee jambo moja la mwisho ambalo ni kuhusiana na wenzetu hawa ambao wanafanya vinasaba, ambao ni TBS. Mheshimiwa Waziri umesikiliza Wabunge wengi wanaongea, kumekuwa na kampuni ya SISPA ilifanya kazi hiyo ya kuweka vinasaba na ilikuwa ina uwezo mkubwa lakini cha kushangaza tulivyowapa TBS wanatoka hawana uwezo wa kutengeneza vinasaba wanaenda tena kwa SISPA kuchukua tena vinasaba wanavileta huku. Mheshimiwa Waziri wakati tunaamua maamuzi mengine tuwe tunafikiria kwa kina, tunaweza kuwa tunataka Serikali ifanye, lakini mwisho wa siku uwezo tunao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kujikuta wenyewe, kama hivi mmeambiwa Mheshimiwa Mwambe anakwambia tunaongeza gharama ya mafuta, tunamtesa nani, tunamtesa mlaji ambaye ni mwananchi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri eneo hili ukalifanyie kazi, ninaamini kabisa tunayo nia njema wote kama Taifa, kuna baadhi ya mambo kama tumefeli tuangalie nyuma tulikotoka turekebishe ili nchi yetu iweze kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza, niendelee tena kurudia kuomba sana kwenye kuhakikisha kwamba, umeme unakuwa wa uhakika. Mnajua mna miradi ya gridi imara, mnafanya kazi vizuri, niombe sana tuangalie maeneo yote. Tunayo maeneo ambayo umeme unakatika mara kwa mara, mfano leo Wilaya ya Manyoni na Ikungi umeme unakatika bila utaratibu, kumekuwa na malalamiko mengi sana. Ninaamini kabisa tuki-stabilize umeme tutafanya uchumi uende mbele na tutafanya watu wafanye kazi zao vizuri kwa uhakika na waendelee ku-enjoy kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya Mheshimiwa Waziri ninaomba sana suala la vitongoji tutazame tuweze kumalizia vitongoji vilivyobaki ili tuende pamoja kama Taifa. Mungu akubariki sana na ninaomba Waheshimiwa Wabunge wote tumpitishie ndugu yangu aweze kupita aende kufanya kazi zake vizuri. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)