Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninashukuru sana pia kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Niungane na wenzangu wote ambao kwa namna ya pekee kabisa wamempongeza Mheshimiwa Waziri, wamewapongeza Wasaidizi wake wote akiwemo Naibu Waziri, REA na mimi niwapongeze kwa namna ya pekee na niwataarifu kwamba, ule mradi wetu wa kuweka taa kwenye Jimbo la Ndanda wenye thamani ya shilingi milioni 400 tunategemea kuusaini hivi karibuni na Mheshimiwa Waziri umenisaidia sana kwenye hili, sasa Ndanda kwenye Kata zote za eneo la barabara kuu inayoelekea Masasi linakwenda kuwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kazi zako nzuri ndizo zinazotufanya leo tusimame na kukupongeza kwa sababu, kwa namna ya pekee kabisa umetugusa kwenye maeneo yetu. Tulipoanza mijadala ya masuala ya REA, mimi binafsi nilikuja ofisini kwako tukiwa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa Mtwara na nikakuambia pamoja na scope kubwa iliyopo kwenye Jimbo la Ndanda ninaomba concentration tupeleke kwenye maeneo mawili. Ulinikubalia na nimshukuru sana pia, Mkurugenzi wa REA na yeye alinielewa ombi langu na kazi sasa ya kuweka umeme kwenye vijiji vyote vya Kata ya Mpanyani na vijiji vyote vya Kata ya Msikisi inaendelea. Nafikiri kufikia mwezi Julai kwa sababu kuna baadhi ya maeneo wameshaanza kuwasha na mimi nitakwenda kushiriki zoezi hili la uwashaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiyasema haya siyo maana yake kwamba, kazi imekamilika kwa asilimia 100, bado mahitaji ni makubwa ya masuala ya umeme kwenye Jimbo la Ndanda ukiangalia vijiji vya Mbemba, Mbaju na vijiji vingine vingi vinavyozunguka Jimbo la Ndanda tuna mahitaji ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee naweza nikakuambia Mheshimiwa Rais ameamua ugomvi. Wewe mwenyewe unakumbuka juzi tulipokuja ofisini kwako mimi pamoja na Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Mtwara tulikuja kweli tuna kilio kwako kwamba Mtwara tuna tatizo kubwa, umeme umekuwa unakatika kila mara maeneo yote ya Mkoa wa Mtwara, hasa kwenye Wilaya ya Masasi, Wilaya ya Newala, Mtwara Mjini na Wilaya zingine zote, lakini umetuhakikishia ndani ya miezi mitatu ijayo unapeleka turbine yenye uwezo wa kufua umeme megawati 20 ambayo itakuwa kama ni suluhisho la awali la kuhakikisha Mkoa wa Mtwara unapata umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ndiyo maana nasema Mama ametuamulia ugomvi. Wewe mwenyewe umetuelekeza na umetuambia kwamba, pamoja na mradi huu wa REA unaotokea Songea wa Gridi ya Taifa kuleta umeme Masasi umepata pesa nyingine ambayo itatoa sasa umeme Masasi kupeleka Mahumbika. Kwa hiyo, maeneo yote ya Ndanda, Chikukwe, Chigugu na vijiji vyote vya katikati hapa vitakuwa vinapata umeme wa uhakika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pamoja na hayo mazuri ambayo wewe unakusudia kwenda kuyafanya nizidi kukupongeza. tumeshuhudia hapa suala la mradi wa LNG na faida zake sisi kama Watanzania wote tunazifahamu. Bado narudia kauli yangu ile ile ya mwazo kwamba, mama ametuamulia ugomvi, Wabunge wa Mkoa wa Mtwara tulikuwa hatueleweki kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mtwara kwa sababu, Mkoa wetu miaka kumi iliyopita ulikuwa juu kimaendeleo kwa sababu ya miradi mbalimbali ya gesi. Walikuwa na hamu kubwa ya kusubiri ili waweze kuona sasa utekelezaji wa miradi hii utafanyika lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndoto kubwa tuliyoisubiri kwa muda mrefu na mimi niwatangazie Wabunge wenzangu, niwatangazie wananchi wa Mtwara na Lindi, sasa inakwenda kutimia, inakwenda kuwa kitu halisi. Kwa namna ya pekee kabisa pia, nimpongeze na Mheshimiwa Hamida kuhakikisha amepambana na wewe Mheshimiwa Waziri kupata pesa za fidia kwa ajili ya wananchi wa eneo la Kikwetu na lile eneo lote ambalo ni kama 5.5 billion wanafidiwa. Hii tafsiri yake ni kwamba, mradi sasa unakwenda kutekelezwa. Haya ni mambo mazuri Mheshimiwa Waziri ambayo tulikuwa tunayasubiri kwa muda mrefu, lakini tunakushauri sasa hakikisha shughuli zinazofuata kutokea sasa za kutiliana saini tuseme, utekelezaji wa miradi, maandalizi yanafanyika kwenye maeneo ya Lindi na Mtwara ili kuweza kusisimua uchumi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, shughuli zitakazofanyika kwenye maeneo haya, badala ya kutumia Uwanja wa Ndege wa Dar-es-Salaam, badala ya kutumia Bandari ya Dar-es-Salaam, hakikisha unawasisitiza hao wawekezaji, ikiwezekana tena kwa mikataba maalum kwamba, mizigo yao, shehena zao zishukie Bandari ya Mtwara, zishukie Bandari ya Lindi kama wataboresha, pamoja na kuondoa mizigo, lakini pamoja na Uwanja wa Ndege wa Lindi ili tuweze kunufaika zaidi. Hayo tu ni baadhi ya mambo ambayo tutakuwa tunayapata pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa nikusisitize, tumesikia kuhusu miradi mikubwa sana ya kimkakati, ndio maana hawa ndugu zetu wa Ludewa wanalia mpaka leo kuhusiana na suala la Liganga na Mchuchuma. Bado mradi huu umekuwa unatajwa lakini hautekelezwi. Tuiombe Serikali sasa kwa sababu, wawekezaji wameshapatikana jambo hili lifanyike kwa haraka ili sisi tuweze kuanza kuona manufaa haya ikiwezekana kabla hata mwaka huu wa fedha kuisha kazi hizo zianze kufanyika, eneo lile la Lindi lichangamke, maeneo ya Mtwara yote yachamke na wananchi waone kwamba,Serikali yao sikivu inawasaidia kuhakikisha haya yanafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo Mheshimiwa Waziri, nikukumbushe jambo moja, Mheshimiwa Kingu hapa asubuhi aliongea vizuri sana suala la SONGAS. Kwa sasa hivi mahitaji ya umeme ni makubwa, hatujakamilisha bado mradi wa LNG Lindi, ule mradi wa Mtwara wa megawatt 300 haujakamilika na mradi wetu wa Bwawa la Nyerere haujakamilika. Kwa hiyo, ona namna ya kukaa na watu wa SONGAS, boresheni hii mikataba inayotumiwa sasa hivi ili wananchi waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala jingine limeongelewa hapa na ukienda kwenye ukurasa wa 36 wa taarifa ya Kamati wanasema kwamba, jukumu la vinasaba ambalo lilikuwa EWURA mwanzoni lilipelekwa TBS, kimsingi inachosema Kamati ni kwamba TBS wameshindwa kufanya hii kazi, kutokuweza kufanya hii kazi maana yake ni kwamba, gharama za mafuta zinaongezeka kwa sababu, sasa hivi wanasema TBS iwezeshwe ili iweze kutengeneza vinasaba, wanataka waanze kutengeneza vinasaba sasa hivi wakati bei ya mafuta inaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBS iongezewe watumishi, urasimu wa kupata watumishi unaufahamu na kuna taratibu zake za kupata, tuachane na hawa TBS kwenye hili jambo tuwape watu ambao wana uwezo wa kulifanyia kazi ili twendenao sambamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilisema pale toka mwanzo kwamba, kutokana na umahiri wako kwenye kazi zako, maeneo yetu sisi yanatofautiana. Kuna maeneo ambako kuna tatizo kweli la umeme, lakini nadhani una nia njema ya kwenda kutekeleza hilo, lakini kuna maeneo ambapo kuna afadhali, sasa tukamilishe haya maeneo yote mawili yaweze kufanana. Mkoa wa Mtwara una vijiji zaidi ya 780 vijiji 800, lakini katika vijiji hivi karibia vijiji 300 havina umeme. Kwa mikakati ambayo umetueleza sisi juzi na ndio maana nakwambia hapa tena kwamba, Mheshimiwa Rais ameamua ugomvi kati yetu sisi Wabunge wa Mkoa wa Mtwara na wewe, lakini kati ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Lindi pamoja na Serikali yao sikivu ya Chama cha Mapinduzi. Tatizo kubwa ambalo lilikuwepo la umeme kwenye Mikoa ya Mtwara na Lindi sasa linakwenda kuisha kwa hatua ulizotueleza za muda mfupi, muda wa kati pamoja na muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasisitiza tu kwamba, hawa watu wanaokuja kuwekeza kwenye masuala ya gesi ninaamini ofisi zao ziko Dar-es-Salaam, ofisi zingine uliniambia wakati ule ziko Arusha na ulisema kwamba, mko kwenye a cell, kwenye contained room ili muweze kufanya majadiliano kwa karibu zaidi. Nikuombe sasa Mheshimiwa Waziri tayari tumeshafikia hatua nzuri na tunakwenda kwenye implementation. Ninaamini na wewe unatamani kufika Lindi kila mara ukaone namna tunavyoishi watu wa Lindi, tunavyoishi watu wa Mtwara, kuwarudisha watu hawa nyumbani tafsiri yake tunakwenda tena kusisimua uchumi wa maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi kirefu tumekuwa tunategemea korosho tu, lakini sasa tunakwenda kutegemea mazao ya gesi, ikiwa ni pamoja na masuala ya mbolea, lakini pamoja na usafirishaji. Bandari yetu ya Mtwara Serikali imeweka pesa nyingi sana kuhakikisha inatumika. Sasa tunapata bahati nyingine mradi wa Gesi unakwenda kutekelezwa kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana, ninaamini una timu sikivu na jana nilipata taarifa pia, timu yako watu wengine tayari wameshashuka chini kwenda kufanyia kazi haya malalamiko ambayo tulikuletea ofisini kwako. Mheshimiwa Waziri, mimi niungane na wote waliokupongeza, sasa tunataka tuyaone yale uliyotuambia juzi yanakwenda kutekelezwa. Tatizo la kukatikakatika kwa umeme Masasi, Ndanda na maeneo mengine yote ya Mtwara pamoja na Wilaya za Lindi yawe yamekwisha kwenye kipindi tulichokubaliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku 90 siyo nyingi, tutarudi tena hapa, tutakuja kuulizana kwamba, Mheshimiwa Waziri ulituahidi kwamba, ndani ya siku 90 matatizo haya ya umeme yatakuwa yamekwisha, kwa hiyo tunataka tuone haya mambo unakwenda kuya-implement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze tena sana Mheshimiwa Rais na nitumie ileile kauli yangu ya mwanzo kwamba, Mheshimiwa Rais ametuamulia ugomvi Wabunge wa Mtwara. Ahsante sana kwa nafasi hii, nikupongeze kwa kazi zako, ahsanteni kwa kunisikiliza. (Makofi)