Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi pia nichangie kwenye hotuba ya Wizara ya Nishati.

Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kama watangulizi wangu waliopita Wabunge wengine waliochangia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa ambayo inafanyika katika Wizara hii ya Nishati, hususani kwa niaba ya watu wa Biharamulo uzinduzi wa substation ya Nyakanazi ambayo sasa inatuondoa katika shida ya umeme tuliyokuwa tumeipata ya ku - run katika low voltage, licha ya hiyo inaingiza Mkoa wa Kagera kwenye gridi bada ya kuunganisha na Rusumo nadhani hata ndugu zangu na majirani zangu wa Kigoma, wote ni mashahidi sasa hivi wananufaika kutokea Biharamulo, kwa hiyo nishukuru sana kwa ajili ya hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza Mheshimiwa Waziri na Msaidizi wake na Watendaji wote katika Wizara hii, kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya, ninazidi kuwashukuru tayari mgodi wetu wa Biharamulo STAMIGOLD tumepokea umeme. Hasara ile ya mafuta zaidi ya bilioni 1.2 yaliyokuwa yanatumika pale mgodini tuna umeme tayari, kwa hiyo ni hatua kubwa na mapinduzi katika Wilaya yetu ya Biharamulo, nina hakika mgodi ule kwa sababu ulikuwa unajiendesha kwa hasara sasa wataanza kufanya kazi kwa faida na hatimae hata CSR ambayo tumekuwa tunapambana nayo pale tunaweza kuipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pamoja na kubanana huko wamenisaidia juzi kwenye ujenzi wa shule ya sekondari ya Mavota, wamejenga vyumba viwili vya madarsa, ofisi, vyoo. Kwa hiyo, nina uhakika baada ya kuanza kupata umeme watafanya vingine vikubwa zaidi ili Biharamulo iweze kusonga mbele kwa kasi sawa na maeneo mengine yanayoendelea kukimbizwa chini ya utendaji wa Mheshimiwa wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wangu nilitaka kuongelea miradi ya REA kidogo, kabla ya kwenda kwenye mambo mengine ya Kitaifa. Ninayo ripoti hapa mimi kwangu nilikuwa na vijiji 25 so far ni vijiji Saba tu ambavyo vimeunganishwa na umeme. Sasa ukijaribu kuangalia kasi ya uunganishaji ni ndogo sana na sisi tunapokuwa tunazunguka kwenye ziara ukishawaambia wananchi Mkandarasi amepita hapa, wao hawajui kaunganisha kijiji gani? Kila mwananchi anataka apate umeme kwenye Kijiji chake, huwezi kwenda kwenye Kijiji ‘A’ ukamwambia Mkandarasi ameshaunganisha ‘B’ yeye akendelea kusubiria, kwa sababu umeme ni demand ya kila mwananchi hasa kwenye Jimbo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nina ushauri kama inawezekana as long as Mheshimiwa Waziri amekiri mwenyewe kwamba wanatafuta mbinu mbadala ya kutafuta Wakandarasi wa REA, hebu liangalieni hili kumpa mkandarasi mmoja Mkoa mzima it was a very big mistake, ni mzigo mzito mno, ninapopiga mimi wa Biharamulo anaondoa timu anapeleka Ngara, akipiga wa Ngara anaondoa timu anapeleka Kyerwa ndivyo hivyo inavyofanyika, kwa hiyo tulikuwa tunaomba kama inawezekana tafuteni Mkandarasi kwa kila Wilaya, bora wakimaliza wataenda hivyo hivyo, hata kama wana miradi miwili, lakini wakimbize haraka hii kazi umalizike maana wananchi wamechoka kusubiri wanataka waone umeme sawa na kule walikowasha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye miradi hii kumekuwa na maelekezo yale ya taasisi zipate umeme kwanza, sasa unakuta taasisi wanataka umeme na wananchi wanataka umeme. Sisi sote ni mashahidi, ujenzi wa Taasisi za Umma una vigezo vyake. Kigezo cha kwanza ni pamoja na taasisi kuwa na eneo kubwa ambalo wanaweza wakafanya miradi mingi, sasa unapoongelea ekari 20 za kujenga kituo cha afya, ukiongelea ekari 20 za kujenga shule automatically haziwezi kuwa kwenye center ya kile Kijiji. Kwa hiyo wengi wamejenga shule pembeni, kwa hiyo tunachoomba sasa, nilikuwa naomba nikuombe Mheshimiwa Waziri ulione hili pia andaa programu maalumu ya kupeleka umeme kwenye taasisi, achana na mambo yaani REA peleka umeme kwenye vijiji, lakini taasisi ambazo ziko pembeni pia utusaidie pia umeme ufike tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu nina shule ya sekondari kwa mfano shule ya sekondari Ruziba, shule ya sekondari Lusahunga, shule ya sekondari Nyakanazi ni shule kubwa lakini hazina umeme kabisa. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba siyo kwangu tu, huenda na maeneo mengine yapo vitu kama vituo vya afya, vitu kama shule ya sekondari, hebu iandalie package yake peke yake. Wapelekewe umeme wao separate tofauti na kwenye vijiji, maana ukienda kwenye ziara wanakijiji wanasema umeme hauko kwenye taasisi hawa wanasema umeme ubaki kijijini, kwa hiyo kidogo inaleta confusion hata kwa Mbunge uwaambie nini wale watu unaowawakilisha au wakutume nini? hilo nilikuwa naomba ulione ili uweze kutuisaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri nilikuwa napitia na andiko hapa pia. Mimi ni mdau wa mambo ya gesi kwa sababu kidogo ni idara ambazo tumezipitia pitia huko hata kwenye masomo yetu. Kwanza ni pongezi, nitakuwa mnafiki na nitakuwa mtu ambaye kweli sitawatendea haki kwa uamuzi huu mkubwa ambao mmeufanya wa kulitoa Taifa letu hapa na kulipeleka mbele. Niyaaseme haya, walio wengi tumekuwa tuna - deal na nchi kama China na vitu vingine kama hivyo, nchi kubwa China na India.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaposimama hapa China kwa mara ya kwanza hata sisi tunaeza tukasema ndani ya Bunge hili tutaanza kum - supply gesi, kwa sababu China hana LNG anaagiza, India hawana LNG wanaangiza, yale mataifa makubwa ambayo yanatumia hii gesi kwa wingi lakini hawana wanachokifanya wanaagiza. Sehemu kama China leo wana nchi zaidi ya 20 ambazo wana - import ile gesi pale ya LNG. Zaidi ya hiyo hata bei China nilikuwa naangalia mwezi uliopita tani moja ya LNG inaenda dola 808, kwa hiyo unaweza ukaona soko kubwa tulilonalo kwenye hilo eneo, mimi siongelei uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji ni investment ambayo tunaenda kufanya pale ya zaidi ya trilioni 8.7 hiyo tuiache, lakini baada ya hapo Taifa linapata nini baada ya uwekezaji. Tuko na ajira za kutosha tuko na power yaku - supply kwenye viwanda, tuko na gesi ya ku - supply kwenye magari. Kwa sababu dunia inapoenda leo tunaenda kwenye clean energy. Unapoongelea clean energy, LNG hata kwenye EACOP nadhani kwenye mkutano, LNG leo wanavyochoma kwenye gari au ukachoma sehemu nyingine ina 40 percent gas ya carbon dioxide tofauti na diesel au tofauti na petroli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo unapoongelea hapo ina less than 35 percent ya Sulphur oxide, zile ni gesi mbaya na ni gesi ambazo zinaua, lakini leo tunapoingia kwenye project kubwa kama hii ya Kitaifa. Siyo tu kwamba tunaenda kujulikana duniani lakini tunaenda kutoa kitu cha maana, kitu ambacho kitaitangaza hii nchi kwa miaka na miaka nenda rudi. Nilikuwa naandika hapa na nilikuwa napitia, umeongelea gesi hii for more than 500 years wanansema stock tuliyonayo au reserve ya gesi tuliyonayo ni more than 500 years tunaweza kuitumia hiyo gesi at current rate. Kwa hiyo, unaona ni mradi mkubwa ambao unaenda kulipeleka hili Taifa miaka na miaka na miaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza zaidi uamuzi wenu wa kumfanya TPDC akawa mbia, maana tumekuwa tunafanya miradi hii unaweza ukaleta Mkandarasi lakini leo chochote kitakachotokea as long as mradi huu umeanza we are the owners, sisi ni wa wabia tutakaopata faida na zaidi ya kupata faida tutapata kodi kwenye hizi bidhaa. Kwa hiyo, kitu kikubwa ambacho mmekifanya leo kwa ajili ya kulinyanyua Taifa hili history ya nchi hii itawakumbuka lakini zaidi uwekezaji mkubwa ambao anaufanya Mheshimiwa Rais kuzunguka huku na huku na hatimae maongezi haya akawa ameyakamlisha ni lazima tumpe sifa na ni lazima tumpongeze kwa juhudi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama hili jambo limeenda muda mrefu halikufanyika ni kwamba kuna imani ambayo watu wameijenga mpaka wakaamua kuja hapa. Unapoongelea kampuni kubwa kama Shell leo unaingia nao mkataba wa ku - run LNG project siyo kampuni ndogo. Ina visima 12 vya gesi duniani ambavyo inachimba leo, ina visima vingine vitatu ambavyo inajenga kwenye nchi mbalimbali, ina maana na Tanzania tunaingia kwenye ramani ya kufanya kazi na kampuni kubwa kama Shell. Kwa hiyo, kitendo cha kuingia kwenye ramani hii haitatutangaza tu kwenye upande wa gesi, inaenda kututangaza pia kwa investors wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuwa unatafuta watu wa kuwekeza lazima kuna watu wengine wataanza kujiuliza Tanzania kuna nini? Kwa hiyo, kama wanajiuliza Tanzania kuna nini maana yake miradi na uwekezaji mkubwa utakuja hapa. Kwa hiyo hilo jambo nilitaka niligusie. Niwapongeze sana kwa bidii kubwa naamini Mungu atatutangulia sawa na hiyo mikataba ambayo mmesema imeandaliwa ya Inter Governmental vilevile mkataba wa operation iende ikafanikiwe salama kwa maslahi ya Taifa hili, lakini kikubwa katika kupitia nimeona hata gawio kwamba tutakuwa tunagawana 50 per cent ya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli leo mtu ana - invest katika kiwango kikubwa kama hicho, mnaenda kugawana faida kubwa kiasi hicho, jamani tunataka nini zaidi ya kumshukuru Mungu aliyetupa hili Taifa. Kwa sababu unavyoongelea gesi leo ya LNG, upande huu wa ukanda huu wetu wote huu, soko kubwa ni China, soko kubwa ni India. Maana yake meli zitakuwa zinakuja hapa zinabeba gesi zinapeleka kule. Hii siyo gesi ya mabomba labda tuelezee kwa sababu huenda mtu mwingine anaweza akaanza kuwaza kwamba utalaza pipe hapa mpaka India, hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gesi hii inakuwa compressed. Ni gesi inachimbwa inakandamizwa kwa moja ya mia sita, yaani tumezoea moja ya mbili, moja ya tatu lakini unaongelea kwamba volume inayochimbwa inakandamizwa kwa moja ya mia sita ya original volume. Kwa hiyo, baadae ikitiwa kwenye meli zile zinazoondoka itaenda kuuzwa kule, kwa hiyo itauzwa sehemu yoyote ile duniani. Siyo gesi ya kutumia mabomba kwa sababu LPG ndiyo wanapampu kwenye bomba lakini hii itaenda direct kuuzwa kwenye maeneo hayo ya nchi hizo ambapo itauingizia faida lakini zaidi ya kutuingizia faida inatuletea pia kutangaza pia hili Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapomalizia nikiondokana na gesi. Tulihudhuria utiaji wa saini za mikataba ile ya kuimarisha gridi ya Taifa au gridi imara Ikulu pale. Ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri zaidi ninampongeza Mheshimiwa Rais, ambaye amekubali kuwekeza zaidi ya trilioni 4.42 kwa ajili ya kuimarisha gridi yetu ya Taifa. Kwa nini nasema hayo, Ndugu zangu umeme una-stage ya kuuzalisha, Wahandisi wanaelewa. Unakuwa na sehemu ya production lazima uanze kuzalisha umeme kabla ya kufanyia transmission, sasa wote ni mashahidi hata engine ya gari ukichukua gari lililotengenezwa mwaka 2023, ukachukua gari the same type na same engine iliyotengenezwa mwaka 2010 au labda 1995 ulaji wake wa mafuta unakuwa tofauti, efficiency inapungua kadri linavyoendelea kubaki. Kwa hiyo, investment mnayoifanya leo ukiunganisha na mradi wa Mwalimu Nyerere maana yake mnatuweka kwenye sehemu nzuri hata wawekezaji mnaowaleta hapa wataweza kuja na watakubali kuja kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa ni aibu unaona mtu anataka aje awekeze kwa matrilioni ya shilingi, halafu mtu huyohuyo anatakiwa aje na pesa ya kununua generator megawatt moja, megawatt mbili, megawatt tatu, lakini yote haya tunavyofanya stabilization ya gridi ya Taifa maana yake hali ya kukatikakatika kwa umeme haitakuwepo. Kwa hiyo, investor anachokuja anakiwaza ni kuja kufanya biashara, kuzalisha na kupata faida na hatimae aweze kuajiri Watanzania walio wengi. Siyo aanze kuwaza ku-run generator kwa sababu, generator la megawatt moja unaweza ukajua linakula mafuta kiasi gani, kwa hiyo, walio wengi at the end of the day anakuwa amewekeza, lakini hawezi kuzalisha kwa sababu, aki-invest kwenye mafuta hataweza kuuza akashindana na watu wengine wanaozalisha kwenye soko katika umeme ule wa maji au umeme wa gesi ambao tunautumia leo kwa asilimia 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo ninakushukuru kwa mara nyingine, lakini niwapongeze Mheshimiwa Byabato, Mheshimiwa Makamba, kwa kazi kubwa mnayoifanya. Mungu awatangulie, haya tunayoshauri Wabunge leo myachukue, hasa kwenye upande wa REA mkatusaidie wananchi wapate umeme, hapo ndiyo tutakapokuja hapa tukaanza kuimba wimbo mmoja na wimbo wa parapanda tutauimba kipindi tunaelekea huko mbele. Asanteni sana nawashukuru. (Makofi)