Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuitendea haki Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kwa hiyo sifa zote ambazo Mheshimiwa Rais anapewa na Mheshimiwa Waziri anapewa, naweza kusema ninaziishi kwa sababu nipo kwenye Kamati hii. Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima wanazingatia vizuri ushauri wa Kamati na ushauri wa Wabunge. Kwa hiyo, ninachoweza kusema hapa tu ni kwamba ninaipongeza Serikali kwa kazi nzuri sana ambayo inaendelea kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika Nyerere Hydro – Electric Power, tumefika Chalinze tumeona kazi kubwa inayofanywa lakini tumepata taarifa ya kina kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa TANESCO, kuona namna ambavyo Tanzania ambayo inaandaliwa kuwa na umeme wa uhakika kazi ambavyo inafanyika. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwa na timu nzuri. Jambo moja tu la msingi hapa Mheshimiwa Waziri tunacho chombo kwenye Wizara yako kiko EWURA (Consumer, Consultative Council) natamani sana ukiongezee nguvu.

Mheshimiwa Spika, kadri unavyoongeza kupanua huduma za umeme, matumizi ya gesi na kadhalika, wananchi wanahitaji chombo cha kuwatetea, wanahitaji chombo cha kutatua migogoro yao kabla haijawa mikubwa. Utakubaliana na mimi kwamba yamekuwepo malalamiko mengi ya utumiaji wa gesi, wengine mara gesi haitoshi, mara gesi iko hivi mara umeme uko hivi. Lazima chombo hiki kipewe nguvu, kipewe fedha kizunguke nchi nzima, kitoe elimu ili kuwafanya Watanzania wawe salama, naomba nikupongeze sana kwa juhudi kubwa ambazo zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo mawili mahsusi. Kwanza, Jimbo langu la Geita Mjini, limekuwa kwenye kuchelewa kupata umeme kwa takribani sasa tangu awamu ya kwanza ya REA, awamu ya pili sasa tunakwenda lot ya pili phase three kwa nini? Kwa sababu tuko Mjini tunayo ahadi ya peri-urban. Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwa juhudi kubwa ulizofanya, ulikuja Geita tukaenda Kata ya Burera ukazungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara wakakufurahia sana, ukawaahidi umeme utawaka itakapofika mwezi wa 12 mwaka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sauti ya unyenyekevu nimefika kwenye banda pale nimeona mipango inaendelea, nimepata taarifa wameanza kuchimba nguzo lakini umeme haukuwaka Desemba. Mimi ni imani yangu kwamba baada ya bajeti hii kupita speed tuliyoiona kwenye mabanda yale itakwenda kufanya kazi yake wananchi wapate umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza na wewe Mheshimiwa Waziri Jimbo la Geita Mjini mitaa 32 bado haijapata umeme na hiyo ndiyo iko kwenye peri – urban, vijiji 10 ambavyo kati ya 18, vinane vimepata umeme, kumi bado ndiyo kazi inayoendelea. Kuna maneno mengi kwamba bado Mkandarasi hajapitishiwa, sijui Mkandarsi bado kuna ushauriano, nikuombe Mheshimiwa Waziri kama tunaanza mchakato wa kupeleka umeme kwenye vitongoji, lakini tuna vijiji na tuna mitaa yenye tafsiri ya vijiji ambayo haijafikiwa na umeme tutakuwa tunawaacha watu wengine nyuma, tutakuwa na double standard kwenye nchi moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kwa kuwa hivi ni vijiji isipokuwa vile viko Geita Mjini, sijui Bukoba Mjini, huyo Mheshimiwa Naibu Waziri ana kesi kama ya kwangu. Ana vijiji na mitaa haijafikiwa umeme kwa sababu peri-urban haijaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri kama inawezekana tufike kwenye vijiji vyote na mitaa yote, halafu tuende kwenye vitongoji. Ni jambo jema Mheshimiwa Waziri umetushirikisha tutachagua vitongoji ambavyo vina uhitaji wa umeme na Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana kwa jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine la pili Mheshimiwa Waziri mimi ni Mjumbe kama nilivyosema wa Kamati ya Nishati na Madini. Tunakupongeza sana kwa kuchukua deni lililokuwa la TPDF na kuligeuza kuwa mtaji, jambo jema sana. Wanaomba hawa watu na siyo tu wanaomba, ni maoni ya Kamati kwamba, Serikali inadaiwa fedha nyingi sana na fedha hizi ni Serikali yenyewe labda ufanye kama ulivyofanya kwenye deni lile Wizara, zile zikatwe juu kwa juu badala ya kuilipa TANESCO, ili TANESCO waweze kuwalipa TPDF kwa sababu visima ambavyo wanachukua vingine inavyoonekana vimeanza kupungua capacity na kwa nini? Ni kwa sababu pia hata uwezo wao wa ku - service kwa muda, kwa sababu wanakuwa hawana liquid umekuwa mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi kwamba speed yao ya kusambaza hata gesi ambayo ni domestic ni ndogo, kwa nini? Kwa sababu hawana pesa ya kutosha. Sasa kulichukua deni ni jambo moja kuwa na cash mkononi ya kuzunguka ni jambo jingine, Wizara yako iwasaidie kulipwa pesa hizo. Serikali iko humu, bilioni mia tatu na kitu kwa TANESCO ni pesa nyingi zingeweza kusaidia pia maeneo mengine tukapunguza madeni tukawahisha huduma kwa wananchi. Wananchi kwa kweli wanaipongeza Serikali kwa uwekezaji lakini wanasikitika wanapoona umeme upo unapita lakini TANESCO haina uwezo wa miezi miwili, mitatu kumuhudumia mlaji ambaye yuko tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo umewekeza umeme una Megawati 1,800 unatumia 1,400 plus, una surplus ya 300 though haiko very stable, lakini una watu wanataka umeme wakupe pesa ili uweze kujiendesha halafu unachukua miezi minne, mitano haujawapelekea huduma, mimi nadhani hili jambo siyo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maoni tofauti kwa mfano, Mheshimiwa Waziri tunafahamu zamani vifaa vilikuwa vinanunuliwa madukani watu wanafungiwa umeme kwa bahati mbaya hapa katikati pakawa na vitu feki. Pengine mngelikuja na mkakati mwingine wa kuangalia mkawa na quality assurance, mkatafuta vendors, mkaondoa kabisa tatizo la mtu kusubiria mpaka vifaa viende. Unakuta kuna sehemu watu wamelipia umeme wanaanza kushindana na vishoka sasa kutoa rushwa ili waweze kupata huduma ya umeme. Mheshimiwa Waziri nadhani jambo hili siyo jambo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kule Geita kwangu kuna wachimbaji wa madini. Wachimbaji wa madini wanatumia gharama kubwa sana kusukuma mitambo na kutoa maji kwenye mashimo. Ikikupendeza ungemteua mtu aka-deal na hilo eneo tu, kwa sababu wapo watu kule Nyarugusu, kule Nyakabale, kule Ngusu wameomba umeme, wanataka umeme kwa ajili ya kusukuma mitambo, wanachukua muda mrefu sana na gharama ya uendeshaji inakuwa kubwa, hawa ni watumiaji ambao Mheshimiwa Waziri watakuongezea kipato kikubwa sana hata kuliko watumiaji wa ndani wa umeme wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa sababu hili ni jambo la kiuchumi nakupongeza sana kwa ku-diversify pia uwekezaji wa umeme, leo tunapokwenda kuanzisha Bwawa la Umeme la Malagarasi tukawa na bwawa la umeme la Julius K. Nyerere, tunaifanya nchi iwe na mitandao ya umeme iliyogawanyika ambayo ni vizuri kuisalama. Wenzetu waliliona hao wa Ukraine kama wangelikuwa wana chanzo kimoja cha umeme na yule jamaa anayewapiga leo wangelikuwa giza, lakini ukipiga mtambo mmoja unawaka wa kaskazini, unawaka wa kusini, unawaka wa magharibi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri kuwa na sources nyingi za vyanzo vya umeme, uwekezaji mwingi ili kusudi siku moja nchi isije ikaingia gizani kwa sababu tu Mwalimu Nyerere Hydroelectric Power imeshindwa kufanya kazi au gesi imeshindwa kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana.(Makofi)