Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, niungane na Wabunge wenzangu kukushukuru sana wewe binafsi kwa uongozi wako mahiri katika Bunge letu hili, pia nichukue nafasi hii kwa dhati ya moyo wangu kabisa kusema Taifa hili lina historia kubwa.

Mheshimiwa Spika, nchi hii imetoka mbali sana kwa ambao tunasoma historia tunajua Taifa hili limetoka wapi katika zana zote za maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Transformation katika Taifa letu ni kubwa sana. Ninaomba niseme maneno yafuatayo na hili ninaomba niseme kwa dhati ya moyo wangu.

Mheshimiwa Spika, kuendesha na kuongoza Serikali ni jambo ambalo kwanza wanaoaminiwa huwa ni watu wachache sana lakini pia kuendesha na kuongoza Serikali ni jambo ambalo linaweza kuwa captured na kumudiwa na watu walio makini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita nilikuwa nafuatilia mienendo ya siasa katika Taifa hasa katika mikutano ya hadhara. Nimesikia baadhi ya vyama vya siasa nje wakimkejeli Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan na wamemkejeli katika maeneo wakisema kwamba Rais ameweka mabango mengi hata ndoto za kufikisha umeme kila kijiji hizi ni historia hakuna kitu kitakachowezekana.

Mheshimiwa Spika, naomba nikupe rekodi mimi kwenye Jimbo langu mimi Serikali ya Awamu ya Sita kwenye mambo ya umeme wametufanyia ndani ya miezi mitatu iliyopita. Ndani ya miezi mitatu iliyopita, Jimbo la Singida Magharibi na nina uhakika mifano hii iliyofanyika Singida Magharibi imefanyika nchi nzima. Hivyo nataka tutoe watu waelewe, Serikali ya Chama cha Mapinduzi iliyoko madarakani chini ya Rais Samia Suluhu Hassan siyo Serikali ya porojo, siyo Serikali ya maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mawaziri wetu akiwemo Kaka yangu January pamoja na Naibu wako, trust mliyopewa na Rais nataka nikuambie January mchana kweupe Bungeni hapa leo, kazi hii wewe na Wizara yako mnaifanya kwa uadilifu na uaminifu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndani ya miezi mitatu, Jimbo la Singida Magharibi ndani ya miezi mitatu nimewashiwa umeme Kijiji cha Germany, Igombwe, Chungu, Irisya, Munyu, Mwasutianga, Kintandaa, Maswea, Kipunda, Mtunduru, Mpugizi, Mpetu, Kinyampembee na Mhintiri, nimewashiwa umeme ndani ya miezi mitatu iliyopita. Hapa ninapozungumza, ninakwenda kuwashiwa umeme mwezi huu Vijiji vya Igilansoni, Msosa, Minyughe, Misake, Makilawa, Mteva, Mtavira, Mayaa, Mlandala, Kaugeri, Mduguyu, Uyumbu, Makyungu, Mgungira mpaka wamefika mpakani mwa Tabora kilometa 225 kutoka Makao Makuu ya Wilaya. Nani kama Mama Samia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jamani tunapozungumza utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ndiyo maana nataka niseme watu wasije wakatuona sisi Wabunge tunakuja hapa, Wabunge wa kusifia. Sisi ni Wabunge wasomi. Hiki Chama chetu ambacho kiko madarakani humu ndani kimeleta cream ya Wabunge wenye akili kichwani. Hapa siyo watu wa kuja kupigapiga makofi. Mkiona tunapiga makofi mjue yale tuliyoiagiza Serikali kwenye Ilani yetu ya chama yanafanyika kwa uzalendo na uaminifu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nataka niseme kwa kazi inayofanyika wale wanaomkejeli Mama Samia nataka nikuhakikishie kwa sababu nimeona yamefanyika kwenye Jimbo langu, Rais Samia anakwenda kuandika rekodi ambayo mtangulizi wake Hayati Magufuli aliianzisha na Mama anakwenda kumaliza kazi, vijiji vyote vinakwenda kuwaka umeme. Nataka niwaombe Wabunge wote tuendelee kumuunga mkono January na Mama Samia na Wizara hii tuendelee kuwashika mkono, kazi wanayoifanya ni kubwa. Sisi kwenye Ilani tuliwatuma mtuwashie umeme, umeme unawaka unataka nisikusifie? Umeme unawaka tusiseme? Tutasema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule wanakopita watu wa CHADEMA wanapiga propaganda kwamba Rais anaweka mabango, nataka nikwambie ukiona mtu anapiga kelele jua umembana vizuri, Mama amewashika kwelikweli kupitia Wizara yako January.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nataka nimpongeze sana Mama Samia na kwa kweli haya mambo tunayafanya kwa sababu hata tusiposema Mungu atatushangaa. Mradi huu unazungumzwa wa LNG toka discovery imefanyika mwaka 2012, tumejaribu mazungumzo 2016, 2017 kwenye kitalu Namba Moja, Mbili na Nne mazungumzo yakakwama. Tukafufua mazungumzo miaka ya 2017, 2019 mazungumzo yakakwama, kwa dhati ya moyo wangu Mheshimiwa January Kaka yangu, kama kuna vitu ambavyo Taifa hili litakukumbuka ni kuyafufua mazungumzo ya mradi wa LNG na kuyafanikisha kwa kiwango kikubwa. Leo tunapozungumza hapa, tunapozungumza mradi ambao unakwenda kufanya generation ya fedha zaidi ya trilioni 80 huu ni uchumi mkubwa kwa Taifa, hakuna Mbunge ambaye ana akili ataacha kuunga mkono Serikali kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kukuamini, umekwenda kuyafufua mazungumzo haya na tunaona mafanikio yake. Ninataka nikuambie na wewe sasa kwa kazi uliyoifanya nzuri ya heshima, tunataka tuone matokeo mzee, transition ya dunia sasa hivi inakwenda kasi. Transition ya gesi sasa hivi dunia inakwenda kwenye umeme wa upepo, umeme wa jua na joto ardhi, mkichelewa kutekeleza mradi huu Mheshimiwa January mimi nakuambia hii gesi itabaki kuwa laana kwa Taifa. Harakisha haraka utekelezaji wa mradi huu, uweze kufanyika, Taifa liweze kupata revenue tuendelee kuwajengea watoto wetu mashule, tuendelee kuwekeza, tuendelee kutatua tatizo la ajira kwa Taifa, nchi yetu iweze kupiga hatua kwa maslahi ya watu wake, hongera sana Kaka yangu Mheshimiwa January. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka kulizungumza, nikuombe Mheshimiwa January pamekuwa na maneno huko mtaani, watu wa SONGAS wanapiga kelele kuna uwezokano mkubwa SONGAS wanahisi kwamba Serikali haina mpango wa ku – renew mkataba. Wafanya kazi kule wana – tension kubwa January, kama January umeweza kufufua mazungumzo ya LNG yaliyokuwa yamekwama toka 2016, ukaleta matumaini kwa nchi, ukaleta matumaini kwa investor. January kakipengele cha SONGAS katakushinda kufanya nao majadiliano Kaka yangu? Nenda kakae na watu wa SONGAS fanyeni nao majadiliano kama kuna vitu mnaviona kwenye mkataba wa kwanza vilikuwa havina maslahi ya Taifa piga chini tutakuunga mkono. Wakikubaliana na masharti ya Serikali na ile ndiyo PPP ya kwanza January ambayo imeleta mafanikio kwenye Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumza PPP best ambazo zimeleta mafanikio ni pamoja na watu wa SONGAS, wanatuuzia umeme kwa only senti sita na ninasikia wako tayari kushuka zaidi. January fanya nao mazungumzo tuweke tension hii tuiondoe, kazi mnayoifanya mimi nilikuja Ikulu niliona projection mlizokuwa nazo za kuwekeza umeme mpaka tuuze umeme nje ya nchi. Niliona mipango ya kaka yangu Ndugu Maharage wa TANESCO na ninasema kabisa kwa dhati, Maharage asivunjwe moyo, kijana huyu ana – vision kubwa sana, maana tumekuwa kwenye Taifa letu tunapo – hire brain zenye uwezo wa kuleta mabadiliko tunaanza kuwapiga vita mara huyu anafanya hivi, Maharage Chande ni moja ya vijana wazalendo wa Taifa hili, aungwe mkono ni kijana mwenye vision kubwa ameonesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikwenda Ikulu nikaona projection za namna nchi inataka kutengeneza umeme na kuuza nje ya nchi, nikaona plan zake ninawaomba Wabunge wenzangu tuwe wazalendo wa kuwaunga mkono vijana wote ambao ni zao la Taifa hili, ambao wanaweza wakalisaidia Taifa hili kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Sika, jambo la mwisho naomba nimuombe Mheshimiwa January. Kwenye Jimbo langu la Singida Magharibi kuna vijiji vinne mliviruka, mliruka Kijiji cha Nkhoire Kata ya Isseke. Ninarudia Nkhoire ya Isseke January ninakuomba uikumbuke. Kijiji cha Mwaru ambayo ni Makao Makuu ya Kata mliiruka ninaomba muikumbuke, mimi kwa kazi hizi mlizozifanya 2025 niletee mtu yeyote mnayemtaka atapigwa saa mbili asubuhi, kwa kazi hizi za umeme. Ninachokuomba ni kwamba endeleeni kufanya kazi kwa uzalendo, Mungu awabariki sana, mnafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niseme nataka niwaambie Wabunge Spika huyu na mimi narudia, hata jana Spika wa Afrika Kusini na watu wao wamesema wao wanamu–endorsed huyu Brigedia Jenerali akagombee Bunge la Dunia. Sasa kama Mabunge makubwa yanamu – endorsed, Congo wako nae, Zambia wako nae, Botswana wako nae, Thailand wako nae, jamani ama namna gani? Tutashindwa jamani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kazi iendelee. (Makofi)