Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kwa siku hii njema ambayo tunaizungumzia kwa maendeleo ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya TWPG naomba nikupongeze sana na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuridhia wewe kugombea Urais wa IPU. Watu wakisikia wanadhani ni jambo dogo, huu ni Urais wa Mabunge yaliyopo Duniani. Dunia ina Mabara Saba, ina nchi 195, ina Mabunge 190 lakini ina chambers 268. Leo hii anasimama Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson kwenda kugombea. Jambo hili ni la Kitaifa, jambo hili ni letu wanawake tunakuwekea dua na ninawaomba Tanzania nzima tukushike mkono kwa dua, kwa hali na mali. Baraka hizo pokea unakwenda kupita. Baada ya maneno hayo, ukituona tunatembea unadhani tuko kawaida, Hapana, tuko na wewe tumekubeba kwenye mioyo yetu tunakuombea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo naomba niunge mkono sana hii Wizara ya Nishati, hotuba aliyoisoma Waziri wetu January Makamba asubuhi ya leo, tumekuelewa. Tumekuelewa Mheshimiwa January tunakuombea upitishiwe hizo hela ulizoomba asubuhi hii ambazo ni shilingi trilioni tatu na ushee na nitashangaa sana nikiona mtu anaziletea kutokuelewa sijui kamata mishahara ya Waziri, mimi sielewi hiyo mambo inataka nini kutupotezea muda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme nina raha kwa ajili ya jambo lake Waziri alilosema katika mambo aliyoyapa kipaumbele lile la tisa, kuendelea kutekeleza mikakati ya programu mbalimbali za kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia (clean cooking) nchini na uanzishwaji wa vituo vidogodogo vya mafuta vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnamo Tarehe Mosi mwezi Novemba, uliniruhusu nikaenda Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais akazindua jambo hili la nishati safi na salama ambalo linakwenda sambamba na lengo la Saba la Millennium ambalo ni Clean and Affordable Energy. Sasa tumeshakamata ile affordable energy na ametuhakikishia Waziri kwamba sasa tunakwenda kupika bila kulia machozi, tunakwenda kupika bila kunuka moshi, tunakwenda kupika kwa haraka na wepesi, tunakwenda kuwahisha watoto shule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kidogo tu, nikiwa mdogo nikiwa darasa la nne nilikuwa nasoma shule ya kijijini, nikaambiwa nikapike chai ya Mwalimu. Jambo hilo lilinifanya wazazi wangu wanihamishe shule ile nikapelekwa kusoma Kifungilo kwa sababu haikuonekana ni vema mwanafunzi kwenda, yaani wao hawakuona sawa nikaokote kuni na kuwapikia walimu. Leo hii inakuja clean energy ambayo sasa walimu wote wanaenda kupika chai kwa gesi. Nitangulize kumuomba Mheshimiwa Waziri naomba hayo majiko 200,000 uzipatie shule za primary wale watoto wetu waache kwenda kuokota kuni za kuwapikia walimu chai, waache kwenda kuwapikia walimu chai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo gumu sana, mwnafunzi badala ya kusoma anaenda kupika chai, haiwezekani siyo miaka hii, tena lakini sambamba na hilo umetueleza kwenye hotuba yako kwamba, tutakuja tuchague. Mimi naomba nitamke hapa hapa naomba uzipelekee zile taasisi za mission kwa ma-sister wale, wakiwemo ma-sister wa Huruma uwatengenezee ile miundombinu waletewe gesi waweze kupikia. Wao haya majiko madogo hayatawatosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliwahi kumuomba mdau mmoja, mdau huyo ni wa Oryx, Benoit. Endapo utazungumza na hao wadau wako wengine waende huko kwenye hizo taasisi kubwa kubwa wakatengeneze hiyo miundombinu. Benoit wa Oryx alikubali na mimi hapa niseme wazi unao wengi. Siwafahamu wote kwa sababu mimi situmii gesi nyingine zaidi ya Oryx. Kwa hiyo, naomba waungane wakatengenezee Magereza yetu, wakatengenezee shule za sekondari, wakatengenezee huko mission na kwingine kote sekondari ili sasa tuachane na kukata miti na kwenda kukoka moto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaona kwamba wanaoteseka zaidi kwa kutumia hiyo nishati inayokatazwa sasa ya kuni ni wanawake. Hakuna jambo ambalo unaweza kulifanya bila kupika, hakuna anayekula chakula kibichi zaidi ya matunda labda hata matunda lazima yaive. Leo Mheshimiwa January Makamba ametuambia tunakwenda kuachana na hilo jambo ifikapo mwaka 2030. Kwa nini nisiseme kwamba leo ninasherehekea? (Makofi) Mheshimiwa Spika, ninaomba pia sambamba na elimu hiyo ya kutumia, kwa hii nishati ambayo tuliyonayo sasa kama huu umeme pia wanafunzi na hata sisi wengine tujifunze kutumia nishati hii kwa uangalifu. Ukitoka zima taa ili na mwingine afaidi, lakini siyo hilo tu, ukitoka zima AC, ukitoka tunza hata ile socket. Kwa kutumia nishati hii vibaya unakuta lift zinawakatikia watu, umeme umekatika, tunaishia kuilaumu TANESCO. Siamini kama kila umeme ukikatika ni TANESCO. Hili jambo nalikataa hata watumiaji sisi pia tunachangia. Tunachangia kwa sababu tunaacha vyombo vyetu hovyo vya moto, moto unawaka tunaanza kuita zima moto kumbe na sisi pia hatukufanya majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, ninachokuomba Mheshimiwa Waziri na timu yako bila kuwataja kwa sababu hii salutation ilikuwa na protocol ndefu sana na mimi naunga mkono, kwa kuunga mkono ile hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Kitandula. Yale yote yaliyosemwa Wabunge wote tunakubaliana nayo na tunasema yaende hivyo hivyo lakini niseme neno moja tu kuhusu hii bulk procurement (hii kununua mafuta kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona kama inaenda kupata shida kwa sababu tumemsikia Mheshimiwa ambaye pia ni mmojawapo mwenye kufanya biashara hizo wanapata shida kwa kutokupata hela za kulipia sasa mzigo uliokwisha fika. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nilikuwa nakuomba tu hili jambo ulifanyie kama dharura, wapate hiyo hela ili lisije tena likatuingiza kwenye matata, amesema yeye aliye-site pia amesema Mwenyekiti wa Kamati. Ninaomba tu kwamba hili jambo lifanyiwe dharura ili wiki mbili zijazo tusije tukapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba kusema hapa kwamba vyote tumeoneshwa kwenye maonyesho ni kweli lakini kuna Kamati ambazo hatujafika maana yake wanakwambia seeing is believing. Tumeoneshwa kama runinga, zile Kamati ambazo hazijafika kwenda kuona Bwawa la Mwalimu Nyerere, bwawa ambalo Mheshimiwa Rais amelifanya kwa nguvu sana na umetuhakikishia linaenda kufunguliwa karibuni, basi ikikupendeza utoe ruhusa tukaende kuliona na sisi tuweze kuelezea kwa ukaribu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye randama tumeona kwamba kuna maeneo ambayo hayataweza kufikiwa ni kwa sababu ya ukomo wa bajeti, lakini kama hapo kadri tunavyoelekea ikipatikana bajeti nyingine kidogo, tunaomba hii Wizara iongezewe kwa sababu hata pamoja na kuwa na simu zetu hizi, bila kuwa na umeme wa kuchaji simu huwezi kuitumia. Ukiwa na gari bila kuwa na mafuta ya kuendeshea gari huwezi kulitumia. Chochote kile kinahitaji hii sekta na ndiyo maana inaitwa sekta mtambuka, iweze kutumia nishati ili kutufikisha huko tunakotaka kufika. Kwa hiyo, ni sekta ambayo ni nzito sana lakini nishukuru Mungu Wizara hii imepatiwa kijana ambaye ni mchacharikaji. Wahenga walisema mzigo mzito mpe Mnyamwezi lakini nasikia yeye siyo Mnyamwezi lakini basi kama hiyo ndiyo lugha, basi pokea Unyamwezi wa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayo mengi lakini kutokana na muda niseme kwamba narudia kuunga mkono hoja, niwapongeze sana wale aliewaona wabobezi wa kwenye siasa na pia wa huku ndani, tumemuona Profesa Mwandosya, tumemuona Mheshimiwa Janeth Mbene, tumemuona Balozi Mathias Chikawe na Mheshimiwa Abuu Bin Juma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana nakushukuru. (Makofi)