Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naomba nitumie nafasi hii kukutakia kila kheri kwenye uchaguzi wa nafasi ya Urais Bunge la Dunia, wengine wanakusikia lakini sisi tumekuona na tunajua utendaji wako na competence yako kwenye nafasi hii ya Uspika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa namna ambavyo wameendelea kufanya kazi kwa umahiri mkubwa, lakini pia Viongozi mbalimbali wa Taasisi za Wizara ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita zaidi kwenye eneo moja na kutokana na umuhimu wake ndiyo maana nahitaji muda wa kutosha sana kuchangia eneo hili. Nitajikita zaidi kwenye eneo due diligence (Uchunguzi wa Kina).

Mheshimiwa Spika, tunajua ya kwamba hili ni eneo muhimu sana pale inapokuja wakati anatafutwa Mzabuni au Mkandarasi wa kutekeleza miradi ya maendeleo. Kuna Mwandishi mmoja wa vitabu anaitwa George Richard aliwahi kusema “No man can find out the truth of something without doing investigation” akimaanisha ya kwamba hakuna mtu yeyote anayeweza kugundua ukweli bila kufanya uchunguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tunajua madhara ya kutofanya due diligence ya uhakika kwenye sekta au wakati unahitaji mkandarasi wa kutekeleza miradi ya Serikali. Moja ya madhara makubwa ni lazima utapa mkandarasi wa mchango kwa maana ya kwamba utapata Mkandarasi ambaye hana sifa, lakini cha pili endapo utafanya due diligence ambayo haina umahiri, utapata changamoto ya ucheleweshwaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na la tatu hata kama miradi hiyo itatekelezeka basi itatekelezeka chini ya kiwango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatambua worldwide yapo maeneo ambayo ni key areas kwa ajili ya kufanya investigation kwenye kuchagua Mkandarasi. Kwanza kabisa, huwezi kumchagua Mkandarasi au mzabuni bila kufanya financial due diligence. Nikisema financial due diligence nina maana kwamba unakagua financial muscles, misuli ya kifedha ya kampuni. Utaangalia masuala ya cash flow, utaangalia masuala ya tax record, utaangalia masuala ya historical financial statements za kampuni. Pia ni lazima utaangalia masuala ya legal and regulatory compliances, lazima ujithibitishie kwamba kampuni hiyo imekidhi matakwa ya kisheria. Utaangalia masuala ya leseni, utaangalia masuala ya vibali kama vimethibitishwa ili usije ukachukua kampuni ambayo iko kinyume na utaratibu na lazima pia uangalie masuala ya legal disputes, kama kampuni hiyo imeshapata pingamizi maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima uangalie masuala ya operational due diligence, ujithibitishie uwezo wa kampuni wa kutekeleza miradi. Utaangalia masuala ya technology lakini pia utaangalia masuala ya products zinazotakana na kampuni hizo na mambo mengine mengi sababu ya muda siwezi kusema yote, lakini kuna masuala ya risk assessment lazima wafanye, lazima ufanye due diligence kwenye management profile, lazima uangalie timu ya kwenye kampuni wale wahusika wa management team kama una profile nzuri unaweza ukachukua kampuni kumbe ni wala rushwa watupu, kwa hiyo lazima ujiridhishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, ni bahati nzuri sana nimeshiriki ziara zote za Kamati hii. Umetutuma tukaenda kukagua miradi ya Serikali, mambo ambayo tumeyakuta kule mengine yanatia kichefuchefu kwelikweli ni lazima tuseme. Tumekwenda Korogwe tukakagua miradi ya REA. Miradi ya REA kuna changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tumefika Korogwe tumekutana na Mkandarasi anaitwa Tontan, Mkandarasi huyu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemkabidhi bilioni 3.9 kama malipo ya awali kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Vijiji vya REA vijiji 54, kwenye Wilaya ya Korogwe lakini Mkandarasi huyu tulipombana akathibitisha mbele ya Kamati ya kwamba fedha zile amezipiga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amethibitisha mwenyewe kwamba fedha zile ambazo amepewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bilioni 3.9 kwamba amezila kinyume na utaratibu. Tukauliza kuhusiana na masharti ya kimkataba, tulichoona mpaka leo ninavyozungumza hapa yule Mkandarasi hajachukuliwa hatua yoyote baada ya ubadhirifu mkubwa alioufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kibaya zaidi Tarehe 14 Februari, mwaka huu Mkandarasi huyo huyo aliyefanya ubadhirifu mwaka jana, ndiyo huyo huyo kapewa tena tender kwenye gridi imara mwaka huu. Wote humu ndani tumekuwa tukizungumza kwamba Mama yetu anazunguka usiku na mchana kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Ni wajibu wetu kama Serikali na kama Bunge kuhakikisha kwamba fedha hizi zinatumika ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie wananchi wa Korogwe popote walipo kwamba Rais wao alitenga shilingi bilioni 3.9 kwa ajili ya watu hao kupelekewa umeme, kwenye vijiji vyao 54 lakini wameponzwa na Mkandarasi asiyekuwa na maadili, wameponzwa na baadhi ya watendaji kwenye Wizara ikiwepo watendaji wa REA kutopeleka fedha hizo mahali panapohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeisikiliza vizuri sana hotuba ya Kamati imeeleza vizuri suala hili na imeomba kwamba hatua kali zichukuliwe kwa kampuni hii na wahusika wote. Mambo haya yameendelea siyo tu Korogwe peke yake. Tumeona hata maeneo mengine kuna mradi wa Kinyerezi One extension wa megawatt 185. Alikuwepo Mkandarasi wa kwanza ambaye Serikali ikatenga fedha dola milioni 133, kati ya dola milioni 188 akatangazwa kufilisika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najiuliza hichi ni kitu gani? Tunakwenda wapi? Hii due diligence inafanyika kwa kiwango gani? Kama tuna kitengo ambacho kinaweza kuwapa nafasi wakandarasi kutekeleza miradi halafu wakawa wanatabia ya kutangaza kufilisika, halafu wakawa wana tabia ya kutafuna fedha za wananchi wa Tanzania hatuwezi kukubaliana na suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninao ushauri, kwanza ushauri wangu wa kwanza ninaliomba Bunge lako Tukufu ikikupendeza iiunde Tume ambayo itakwenda kukagua vitengo vyote vinavyo- deal na due diligence kwenye Taasisi ya Wizara ya Nishati. Yaani kwa maana ya kwamba due diligence na wenyewe ifanyiwe due diligence. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ninaomba baada ya kubainika taarifa ya kutoka kwenye ukaguzi huo iletwe Bungeni na Bunge liweze kuchukua hatua, wale wote wanaohusika kwenye masuala ya ten percent wachukuliwe hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ningependa kuomba sana. Mheshimiwa Waziri pelekeni hawa watu wapate taaluma, vitengo hivi wapate taaluma. Wahusika waendelezwe. Ipo mifano mingi duniani ambayo imepitia changamoto kama hizi, ambapo Wakandarasi wakipewa tender wanatangaza kufilisika. Maeneo mengi Wakandarasi wanafuja fedha ya Serikali, kuna maeneo mengi ya kujifunza.

Mheshimiwa Spika, maeneo machache ambayo nimeweza kuyaangalia na ninaweza nika-share hapa Bungeni, kuna mradi wa Solyndra Project huko California, wali-face the same coincidence kama ya kwetu, nendeni kajifunzeni kule. Kuna Bwawa la Bakun ni project iko kule Malyasia wali-face changamoto kama ya kwetu, nendeni mkajifunze kule. Kuna Bujagali Project iko Uganda hapo, nendeni mkajifunze kule, kuna Fukushima Power Plant Japan wali-face masuala tunayoya-face sisi Wakandarasi kutangaza kufilisika, Wakandarasi kutafuna fedha za Serikali, nendeni mkajifunze kule walichukua hatua gani, mkiwa hamna ninazo hapa naweza nikawapatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme hivi, tusiwe na haraka sana ya kuona matokeo ya mambo makubwa na wakati tuna mengine ya kawaida ambayo bado hatujayakamilisha. Nimesikiliza taarifa nzuri sana ya Mheshimiwa Waziri lengo lake ni zuri sana, lakini napenda nishauri kwamba kama kuna vijiji 12,000 ambavyo bado havijapatiwa umeme, hakuna sababu ya kwenda kukimbilia vitongoji 36,000 kuvipatia umeme kabla ya kukamilisha vijiji hivi 12,000. Tuende tumalize hatua ya kwanza ya vijiji vyote, vikamilishiwe umeme, tuende hatua ya vitongoji. Lengo ni kuona kwamba watu wote kwa wakati sahihi wanapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba nikushukuru sana, ahsante. (Makofi)