Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. SALMA R. KIKWETE: Ahsante sana Mheshimiwa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba nianze kwa kumshukuru Mungu hatimaye nikushukuru wewe, lakini kabla ya kusema jambo lolote niongezee pale ambapo ulizungumzia kuhusu wale watoto wangu.

Mheshimiwa Spika, wale ni watoto ambao wanatoka kwenye Shule ya Sekondari ya WAMA Nakayama iliyopo Mkoa wa Pwani ndani ya Wilaya ya Kibiti, watoto hawa wamemaliza Kidato cha Sita hivi karibuni kwa hiyo wote ni watoto wa Kidato cha Sita. Jambo lingine la pekee hawa watoto wanatoka nchi nzima katika Taifa letu la Tanzania, ni watoto yatima na wanaotoka katika mazingira magumu, wapo pale kwenye shule ile wanagharamiwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana nilitaka niongezee hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Daktari Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya katika Taifa letu la Tanzania. Hakuna mashaka hata kidogo kila Mbunge atakayesimama hapa hataacha kumpongeza Mama kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya. Kazi hiyo kwenye huduma za jamii kwenye afya, kwenye elimu kwenye miundombinu ya barabara na kila eneo Mama amefika.

Mheshimiwa Spika, kufika siyo kwamba yeye afanye ziara atembelee pale kwenye aidha Wilaya au Kijiji, uwepo wa miradi mikubwa ya maendeleo ni kwamba yeye ameshafika katika eneo husika, nampongeza sana Mama Mwenyezi Mungu amjalie na ampe maisha marefu ili azidi kuwatumikia watu Watanzania hawa na kutatua changamoto zao zinazowakabili, ahsante ama tunakwenda ahsante Mama tunakushukuru, ahsante mama tunakutakia maisha marefu yenye heri na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa nianze kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri wetu wa Nishati January Makamba na Naibu Waziri wake bila kumsahau Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii, hongereni sana. Nikupongeze sana Mheshimiwa January Makamba kwa maono yako makubwa ambayo umeyaonesha katika Wizara yako, lakini maono hayo ni yapi?

Mheshimiwa Spika, tendo la kutuwekea pale maonesho yale, yaani umeonesha ubunifu mkubwa na huu wala haujawahi kutokea, hongera sana Mheshimiwa Waziri Makamba. Hii inadhihirisha kwamba wewe ni kijana mwenye maono, unategemea kufika mbali zaidi Mwenyezi Mungu akikuwezesha na tunaomba akuwezeshe, umeonesha kazi kwa vitendo na siyo maneno. Hongera sana kwa kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka niende kwenye eneo la kushamirisha Nishati safi ya kupikia. Kwa kweli, Mheshimiwa Waziri huyu ameweka historia ya aina yake na historia hiyo ni kwa mara ya kwanza nishati ya kupikia kutambuliwa, siku zote watu hawatambui nishati hiyo wakati hii ni muhimu sana. Hii nishati inatumika zaidi na wakina Mama wa kada zote, wakina Mama wenye kada ya juu, kada ya kati lakini kule kada ya chini wale maskini wale ndiyo wanaotumia nishati hii kwa kiasi kikubwa, kwa kuwatambua hawa kwa kweli umefanya jambo moja ambalo ni kubwa na jema.

Mheshimiwa Spika, kinachofurahisha zaidi asilimia 80 ifikapo mwaka 2023 tutakuwa tumeifikia nishati hii, lakini wapo wa nishati hii ina maana kwamba tutafanya mazingira yetu yawe salama zaidi watu waache kukata miti, kutumia kuni na kusababisha kutumia kwa nishati hii na mazingira yetu yanakuwa salama zaidi. Ahsante sana, Mheshimiwa Waziri wetu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Nishati ametupa majiko 100 kila mtu amempa majiko 100, Wabunge wote sisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumepewa majiko 100, hata wewe umepewa, hata Mheshimiwa Waziri Mkuu amepewa hilo jiko, Mheshimiwa Katibu wa Bunge, yaani wote wamepewa ili wakayatumie. Sasa ninachokuambia, kama Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuko tayari kwenda kuyatangaza haya majiko Majimboni kwetu ili wananchi wetu watumie nishati iliyo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uwepo wa nishati ya uhakika ni jambo la msingi kwa maendeleo endelevu na uchumi wa Taifa lolote lile hapa ulimwenguni. Nishati ni kila kitu, nishati ndiyo maendeleo, nishati ndiyo inayoinua uchumi wa watu. Nipongeze kwa nishati hii upande wa umeme, sasa hivi umeme tunao ndani ya vijiji vyetu, umeme tunao ndani ya Kata zetu hali kadhalika umeme utapelekwa ndani ya vitongoji vyetu ili baada ya miaka michache ijayo ndani ya kata kutakuwa na umeme, ndani ya vijiji kutakuwa na umeme na ndani ya vitongoji vilevile kutakuwa na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, umeme huu ambao umepelekwa kule vijiji, kwa mfano mmesema vituo 66 vya afya vimepelekewa umeme nchi nzima. Ongezeni kupeleka umeme huu kwenye vituo vya afya, kwenye zahanati zetu ambako kule ndiyo kuna watu wengi, wakati mwingine watu wanatumia sijui nikisema vikoroboi mtanielewa, zile taa zile ndogo ndogo wanatumia vikoroboi wakati mwingine ya kufanyia hata mambo makubwa ya msingi. Pelekeni umeme huo kule vijijini na kwenye zahanati na vile vituo vya afya, hali kadhilika kwenye shule zetu, baadhi ya shule umeme hakuna, msisahau hili kwa sababu tunataka tuwe na elimu iliyokuwa bora, elimu haiwezi kuwa bora kama wanafunzi hawana umeme kule shuleni, hawatapata muda wa kujisomea. Huo ndiyo ushauri wangu tupeleke umeme wa kutosha kule kwenye taasisi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka nije kwenye lile lenyewe kabisa. Jambo lenyewe kabisa ni suala la LNG. LNG inapatikana kule kwetu ndani ya Mikoa ile ya kwetu lakini hasa Manispaa ya Lindi, Manispaa ya Lindi iko ndani ya Mkoa wa Lindi, huu mradi unapatikana katika Manispaa lakini Jimbo la Lindi Mjini, Jimbo la Lindi Mjini Manispaa ile ina Majimbo mawili, Jimbo la Lindi Mjini na Jimbo la Mchinga. Sasa nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa dhamira ya dhati ya kuleta ukombozi ndani ya Mikoa yetu ya Kusini, ndani ya Mkoa wa wetu wa Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema haya? watu wa kule wanaambiwa kila siku kipato chao kidogo, maskini. Huu mradi utakuwa ndiyo ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Lindi, wananchi wa Mtwara, wananchi wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla. Mapato yatakayopatikana hapa pia yatawanufaisha wanalindi, wanamtwara, wanaruvuma, yatanufaisha Taifa la Tanzania, yatanufaisha na watu wengi mbalimbali katika dunia hii, kwa sababu kitakachopatikana kitauzwa nchi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona muda wangu umekaribia. Baada ya kuyasema hayo, mwisho kabisa mambo ni mazuri, ni makubwa, ninachoshauri, bajeti iliyopangwa ipelekwe kwa wakati. Kupelekwa kwa bajeti kwa wakati ndiyo mafanikio ya mipango yote katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)