Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kuwahisha zawadi yangu kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia bajeti ya Nishati nikiwa mtu wa kwanza.

Mheshimiwa Spika, Mwezi Julai nitakuwa nakamilisha miaka 39 tangu nianze utumishi kwenye sekta hii ya nishati, kwa hiyo kwa kuniteua niwe wa kwanza kuchangia umewahisha zawadi yangu ya miaka 39. Kuna lingine niliseme kwa wapiga kura wangu masuala ya umeme nimeyamaliza jana kwenye maonesho ya umeme ya karne. Maonesho yale yaliyofanyika jana hapa hoja zenu zote nimezipeleka kwa Meneja wa Wilaya na wa Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumza kuhusu mafuta na gesi tu umeme nimemaliza. Pia nimuombe Waziri ukatafute kitabu kinaitwa Tanzania Oil and gas cha Mzee Sylvester Barongo, kinaelezea historia ya mafuta na gesi kuanzia mwaka 1952, mwaka 1974 tukapata gesi ya kwanza Songo Songo akiwepo, 1982 Mnazi bay tukapata gesi Mzee Barongo akiwepo. Pia nafurahi Mzee Ntomola yuko pale, Mzee Khalifan yuko hapa, Mzee Mwandosya bosi wetu yuko hapa. Kitabu ni kizuri ana kitawasaidia Wabunge waelewe sekta ya gesi Tanzania tunapojiandaa kwenda uchumi wa gesi.

Mheshimiwa Spika, suala la kwanza nizungumzie bomba la mafuta. Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Rais Dkt. Jenerali Mseveni kwa kuwa na msimamo thabiti kuhakikisha bomba la kutoka Hoima mpaka Chongoleani linajengwa. Ujenzi wa bomba hili pamoja na kuleta faida za ajira litafungua njia za kuweza kuchochea wawekezaji katika sekta ya mafuta waweze kuweza zaidi. Sisi tunayo rasilimali ya mafuta lakini watu wengi wamekuwa hawaji hapa wakijiuliza mafuta ya Kigoma utayafikishaje Dar es Salaam, Eyasi Wembere utayafikishaje Dar es Salaam. Sasa kwa kujenga bomba la mafuta ni kwamba wawekezaji wengi watapata motisha. Kwa hiyo, kwa sababu hiyo mimi ninaunga mkono.

Mheshimiwa Spika, suala lingine kwa kutumia bomba la mafuta ajira zitakazotengenezwa zaidi ya 10,000 ni kwamba vijana wa Kitanzania sasa wanakwenda kufundishwa stadi za Kimataifa, baada ya ujenzi wataweza kutumika katika viwango ya Kimataifa mahali popote duniani. Sambamba na hilo ninaipongeza Wizara na naipongeza Serikali kwa kumaliza rejea ya product sharing agreement, hili suala la OPSA limechelewesha utafutaji mmefanya maamuzi mmeweza kushughulikia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la bulk procurement ununuaji wa mafuta kwa wingi. Bila kusema mengi naunga mkono mapendekezo ya Kamati iliyopewa dhamana ya kusimamia shughuli hii ya bulk procurement. Kama huwezi kujua adha angalia kwa mwenzako, mwaka mzima tumemaliza pamoja na mitikisiko ya kidunia hatukuweza kupata ukosefu wa mafuta nchini. Majirani wetu wamepata hiyo adha, hata Watasha huko Ulaya wamekosa mafuta lakini sisi tumekwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu wamehangaika kutafuta njia mbadala lakini ule ulinganisho wa kiasi cha kununua mafuta wengine wananunua bei ghali mara nne. Premium yetu iko kwenye 40 kuna wenzetu wananunua premium ya 160. Kitabu kile cha Mzee Barongo ambae ni bosi wangu kinaelezea namna ya kutafuta premium mkitafute muweze kukisoma.

Mheshimiwa Spika, sasa zaidi niende kwenye mradi wa LNG, nilimwona Mama salma anapiga makofi, anashangilia tunakuja Lindi na mimi nakuja Lindi ujombani nami nifaidi. Mradi wa LNG ni mradi mkubwa wa dola bilioni 42 zaidi ya bajeti au sawa na bajeti yetu ni mradi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, mimi nimesoma suala la maamuzi. Nichukue fursa hii kipekee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kufanya maamuzi amefanya maamuzi, hivi visima havikuwepo leo lakini imekuwepo dana dana kwa miaka saba kama alivyosema Waziri, lakini Mheshimiwa Rais akatoa maamuzi. Mwezi Juni nilimsikia mwenyewe akasema nendeni mtekeleze haraka. Sasa niko hapa kuwaelekeza kwa nini Mheshimiwa Rais anataka tutekeleze mradi huo kwa haraka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu wa LNG utakapokuwa umefanyika uwezo wa Tanzania kuuza nje kwenye masoko ya Kimataifa utaongezeka, tutapata pesa nyingi za kigeni, ulali wa kuuza na kununua Tanzania tutakuwa na advantage tuta-export zaidi. Sasa hivi Tanzania tuna-export bidhaa zenye dola bilioni 12 kwa mwaka. Gesi peke yake itakuwa na uwezo wa kusukuma katika soko la Kimataifa zaidi ya uwezo huo.(Makofi)

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mwijage kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Profesa Mkumbo.

TAARIFA

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mwijage, amesema dola bilioni 42 ni sawa na bajeti yetu, actually ni sawa na GDP yetu. Kwa hiyo, ni fedha nyingi ambazo ni pesa nyingi kwa kweli uamuzi anaouzungumza ni uamuzi mzuri na ni uamuzi mkubwa sana, kwa sababu ni fedha nyingi na zitabadilisha kabisa uchumi wetu. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mwijage, unapokea taarifa hiyo?

MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nizungumze taratibu aliyenipa taarifa ni Profesa na amesema anatoa taarifa kusisitiza Mheshimiwa Rais kufanya maamuzi, weka kwenye mabano nakubali taarifa hiyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa nini Mheshimiwa Rais amesema tuharakishe? Mafanikio ya kuanza kutumia gesi yataharakisha ujenzi wa uchumi wa viwanda. Siyo ujenzi wa viwanda ni kujenga uchumi wa viwanda ina maana chuma utakayoipata shughuli za kuendeleza sekta ya gesi LNG itatupatia pato, itafundisha watu. Kwa hiyo, tunapozungumzia sekta za uzalishaji iwe kilimo, mifugo, sekta zote tutaweza kuzalisha kwa tija. Pamoja na kuwa na mafuta tutaweza kuwa mabingwa katika dunia kwa kutumia haya mazao ambayo yamekuwa yakitusaidia siku moja, siku nyingine, tutauza kahawa nyingi, maziwa mengi, pamba nyingi ile C to C sasa tutaweza kuwa na viwanda vyetu hapa.

Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwenye bomba la mafuta tunakwenda kutengeneza huo ndioy mfano kwenye chuo cha Lindi, tunakwenda kufundisha vijana wetu wawe wataalam katika sekta za mafuta ili Tanzania sasa miaka ijayo wawekezaji wanakuja kuchukua vijana wetu hapa na kwenda kufanya kazi sehemu nyingine.

Mheshimiwa Spika, kwa kutenegenza huu mradi kwa kukubnaliana sasa wawekezaji mahili wa dunia wanajua kwamba Tanzania sasa ni mahali salama pa kuwekeza. Makampuni yanakuja sisi tuna TCF zaidi ya 68 hizi mlizonazo, mimi sio mtabiri lakini najua kwa uhakika hapa tuna mafuta, hapa tuna gesi lakini hauwezi kuyapata mafuta mpaka uyachimbe.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe sababu nyingine kwa nini tunafaidi kitu hiki. Faida nyingine katika utafutaji wa mafuta ni kwamba sisi Watanzania kwa fursa tuliyonayo tunakwenda kubeba nchi nyingine zilizotuzunguka. Tulikuwa na mradi wa mbolea ulikwama kwa kuangalia gesi tuitumie kwa namna gani, sasa bila kutetereka tutatengeneza kiwanda chetu cha mbolea na kitaweza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwakumbushe Wabunge wenzangu, na Mheshimiwa Jafo naona simuoni na wenzangu niliokuwa sisi ni mahiri wa gesi, sisi tunajua gesi. Gesi inayokuja ni neema tumekaa nayo tumejitafakari. Kwa hiyo, wale wanaofikiria kwamba gesi ni laana ni kwao. Sisi gesi tunaijua tumedhibiti mafuta tunajua namna ya kuitumia. Pia, lengo la nishati hii ni kwa ajili ya mapato na matumizi na ustawi wa Watanzania. Tunakwenda kujenga uchumi imara, uchumi wezeshi na uchumi ulio jumuishi. Kwa hiyo, naunga mkono maamuzi ya Mheshimiwa Rais kwamba tuharakishe ujenzi wa gesi ili iweze kuwafikia wananchi ili kusudi ichangamshe uchumi nan chi yetu iweze kuwa ni nchi yenye ushindani ambayo inakwenda kwenye uchumi mkubwa, uchumi wa Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono bajeti ya Wizara hii. (Makofi)