Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, ninaipinga bajeti hii kwa asilimia mia moja kabla sijachangia. (Makofi)
Kwanza kabisa naomba nitoe masikitiko yangu kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mchana huu kusitisha wanakijiiji wa Mpuguso wasiendelee kujenga zahanati ya nguvu ya wananchi. Ikumbukwe kwamba Waziri wa Afya alipita na akaona wanakijiji akawaeleza waendelee kujenga kwa sababu aligundua kuna ufisadi unaofanywa na watu wa Halmashauri ya Rungwe Magharibi.
Ndugu zangu, binafsi ninaona Taifa kama linayumba, linayumba kwa sababu ya kutetea vyama na Wabunge tuko mahali hapa kutetea haki za wananchi, vyama tumeviacha milango lakini masikitiko yangu ni kwamba imekuwa hali ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika Waziri Mkuu hayupo, nilitaka kumwambia wanaopiga makofi wengi wapo zaidi ya miaka kumi katika jengo hili, walipitisha bajeti zilizopipita, wengine waliandika risala za Rais aliyepita, leo hii wanajinasibu kusema uongozi uliopita ulikuwa haufai, kana kwamba uongozi uliopo sasa umetoka mbinguni na wao ni moja ya viongozi waliokuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalendo unaumbwa kwenye nafsi na uoga ni dhambi. Ukiwa kiongozi mwoga huitendei haki nafsi yako binafsi, huitendei haki kizazi kinachokuja na ni aibu kwa Taifa unaloliongoza. Leo hii tunazungumzia maendeleo, ni maendeleo gani yanaweza kufanyika pasipo utawala bora? Kama Mkuu wa Mkoa, kwa matakwa yake binafsi na utashi wa chama chake anaweza kuzuia zahanati inayotaka kusaidia wanawake wanaojifungua kwa shida, wapate sehemu murua ya kujifungulia anazuia kwa mantiki ipi na kasi ipi mnayoizungumzia ya hapa kazi tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku tutapita, walikuwepo watu walipita, na wengine mko humu mlikuwa Mawaziri leo mko pembeni. Nchi hii ni yetu sote, nchi hii tulizaliwa hapa, tuko hapa; mnazungumzia habari ya tv, mimi ni mtoto wa uswahilini, leo niko kwenye Bunge hili sikuwepo Bunge lililopita lakini nilichaguliwa, jambo la msingi tumesaini mikataba ya nchi mbalimbali ya haki za binadamu ndiyo maana tunadai tv, siyo kuonesha sura zetu, kama ni sura zinafaamika kwa waliotuoa, wanaotupenda, ndugu zetu, sura zetu wanatufahamu. Tunachosema ni haki ya msingi tunapozungumzia utawala bora ni haki ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu. Ndugu zangu TAMISEMI, walimu wanadai madeni, tumewakopa walimu, walimu hawajalipwa mishahara, wengine fedha za likizo kwa muda mrefu, tumewakopa. Bajeti iliyo mbele yetu haioneshi kama inaenda kulipa madeni, na walimu wako wengi katika Taifa hili. Unataka kutengeneza Taifa la viwanda, usipomtengeneza mwalimu ni nani ataingia katika hivyo viwanda? Walimu hawana nyumba, mmeeleza idadi ya nyumba mlizojenga lakini nyumba ni peanut, ni nyumba chache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe serious, tusifanye sanaa kwenye maisha ya watu, tusifanye sayansi kwenye maisha ya watu. Mimi nakubaliana kwamba kama nchi iliharibika, nilitegemea Serikali ya Awamu ya Tano itangaze janga la Taifa kwamba tumeingia hatuna fedha, mafisadi wamekula fedha, tunaanza sifuri tujifunge mkanda, ningewaelewa, kuliko kujidanganya kwamba tuna fedha wakati tuna madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wametukatia fedha za msaada ndugu zangu, Mwalimu Nyerere aliwaaminisha wananchi wakati wa vita vya Kagera, wananchi walimwelewa, wengine walitoa mali zao kusaidia Taifa. Namshauri Mheshimiwa Rais Magufuli kutangaza hali ya hatari, tangaza hali ya hatari kwamba Taifa halina fedha. Tuweke vipaumbele vichache, vitakavyotekelezeka, wananchi watatuheshimu, kuliko kusema tuna fedha nyingi TRA inakusanya fedha nyingi wakati mnajua ni madeni. Mtu unayemdai akikulipa mwisho wa siku analipa nini siyo ameshalipa? Tutabaki kwenye sifuri.
Mheshimiwa Mwenyeketi, vyanzo vya mapato kwenye Halmashauri kuna mianya mingi sana ya upotezaji wa fedha, ninashauri tujikite kukusanya fedha vizuri, tuache siasa. Halmashauri zilizoshinda kwa vyama pinzani zipewe msukumo wa kuendeleza kazi na zilizoshinda kwa CCM zifanye kazi kwa faida ya wananchi. Ubabaishaji wa vitisho vya Wakuu wa Wilaya wanaoingia kwenye Halmashauri za Madiwani sijui kwa vifungu ngani na kuwatisha baadhi ya Madiwani sidhani kama ni muafaka kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua mmetukejeli sana na mkasema hatutaki kuchangia tulinyamaza, tunapochangia mnatuwekea miongozo, mwisho wa siku Taifa ni letu sote, Taifa ni la Watanzania, ninyi siyo malaika na wala tusimfanye Rais kama hirizi, kila kitu Rais, Rais ni Taasisi inawategemea ninyi mkiwa waaminifu mtamsaidia Rais kutimiza ndoto zake. Leo hii Rais hata kama anafanya vizuri yuko peke yake, ninyi wengine...; potea mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wengine ni kama wapambe ninaomba mbadilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Tanzania mpya tutaitengeneza sisi, Tanzania mpya haitatusaidia tukipeana vijembea au kwa mabavu, ninaomba tujitafakari kama Taifa, tutetee Taifa letu wala siyo matumbo yetu, tutetee wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya siungi hoja kwa asilimia mia moja na naendelea kusema siku moja ukweli huu utajulikana. Ahsante.