Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuhitimisha hotuba yangu. Kabla sijaendelea nianze kwa kukushukuru wewe kwa kuliongoza Bunge letu kwa weledi mkubwa. Nafahamu umekuwa kiongozi bora wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vile pia kule Mbeya Mjini wananchi wanakupa ushirikiano. Natumia nafasi hii kuwashukuru Wanambeya Mjini na kuendelea kuwaomba waendelee kukupa ushirikiano, Taifa linakutegemea. Kwa kweli tunakushukuru sana kwa uongozi wako mahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naishukuru sana Kamati ya NUU inayoongozwa na Mheshimiwa Vita Kawawa, Makamu Mwenyekiti Vincent Mbogo pamoja na Wanakamati. Tunawashukuru sana kwa namna ambavyo mnaendelea kutuelekeza na kutushauri ili Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iendelee kuwa ni Wizara ambayo inamsaidia vyema Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao mmechangia katika kikao hiki. Tunawashukuru sana kwa ushauri wenu ulikuwa very constructive. Tunawashukuru kwa madini ambayo mmetupatia, yanaenda kutuimarisha kama Wizara ili tukajipange vizuri kuendelea kuhakikisha tunamsaidia Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, kuendelea kuyasaidia majeshi yetu, kuendelea kujenga ustawi na kujiimarisha.

Mheshimiwa Spika, kama Dada yangu Mheshimiwa Jesca alivyosema, pia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni sehemu ya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama alivyoinukuu. Kwa hiyo, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushauri na maoni ambao ametupa. Nawashukuru hata wale ambao hawajapata nafasi ya kuchangia kwa sababu ushiriki wao na support yao kama tulivyo hapa ni sehemu ya mchango. Kwa hiyo, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, mpendwa wetu, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli anafanya kila aina ya jitihada kuhakikisha majeshi yetu na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kutimiza wajibu wake. Yapo mambo makubwa ambayo Mheshimiwa Rais anawezesha vyombo vya ulinzi na usalama, lakini kama mnavyojua, yapo ambayo tunaweza tukayaweka wazi na yapo ambayo yanaendelea kuwa classified, lakini Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu anafanya kazi kubwa sana ya kuviwezesha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Tunamshukuru.

Mheshimiwa Spika, vile vile tunamshukuru Mheshimiwa Rais, kwenye dira yake ya kuwezesha kukua kwa diplomasia ya kiuchumi. Kama mnavyofahamu, Diplomasia ya Kiuchumi inapofanikiwa hata Diplomasia ya Ulinzi inafanikiwa. Kwa hiyo, nasi upande wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kupitia Diplomasia ya Kiuchumi pia ametusaidia kuimarisha Diplomasia ya Ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nchi yetu ina amani ambayo tunaipata kwa gharama kubwa ya wanajeshi na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuendelea kushirikiana wakiwezeshwa na Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, wakati wa amani ndiyo wakati wa kujenga uchumi wa Taifa letu. Kwa hiyo, tuendelee kumpa ushirikiano Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Waheshimiwa Wabunge wenzangu pamoja na Watanzania ambao mnanisikiliza. Mheshimiwa Rais ametengeneza mazingira wezeshi ya kuzalisha, kuendesha shughuli za kiuchumi, sasa tushikamane naye bega kwa bega kuhakikisha tunaendelea kujenga nchi yetu, kujenga uchumi na kuhakikisha kwa kweli Mheshimiwa Rais tuna kila sababu ya kumuunga mkono kwa asilimia mia moja ili azidi kutenda maajabu.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, mnaona kwa namna ambavyo tunapata miradi ya maendeleo kwenye majimbo yetu. Tutembee kifua mbele tuwe na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumpe moyo, tushikamane naye bega kwa bega. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niende kwenye kujibu hoja ambazo zimejitokeza kwenye mijadala, na kwa sababu ya muda sitaenda hoja baada ya hoja, lakini niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kila hoja tumeichukua, tunaenda kuifanyia kazi. Kamati ya NUU ni Kamati ambayo iko makini sana. Wana mfumo wa monitoring and evaluation. Hoja ambazo zilijadiliwa hata kwenye miaka ya fedha iliyopita, wana utaratibu wa kusema hii bado, hii tayari, hii hebu tueleze. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kupitia Kamati ya NUU tutaendelea kufanyia kazi haya ambayo mmechangia na kutuelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la ajira JKT. Huku jeshini tunakuita kujiandikisha, siyo ajira, lakini kwa sababu ya kuelezea tulichukulie hivyo hivyo “ajira”, lakini huku tunajiandikisha kwa sababu mwanajeshi anajiandikisha kwa sababu ya kuwa tayari kutumikia Taifa lake na mahali popote na kwa gharama yoyote ikiwemo maisha yake. Kwa hiyo, tunaendelea kuwashukuru sana askari wetu pamoja na maafisa kwa kujitoa kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ajira za JKT nimefanya uchambuzi, 45% ya vijana ambao wanajiunga na JKT ndio wanapata fursa ya kuajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama. 55% kwa sababu vyombo vya ulinzi na usalama nafasi ni chache, ndiyo hiyo JKT inawafundisha ujuzi wa ufundi stadi ili warudi wakajiajiri au kupitia mifumo mingine ya Serikali waweze kusaidiwa kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba Waheshimiwa Wabunge kama walivyochangia, tunalo jukumu la kushirikiana kuhakikisha hii 55% ambayo inarudi mtaani, kwa kadiri inavyowezekana tunashirikiana kuipunguza. Hapa mmetupa mawazo tufanye nini ili kuweza kupunguza hii 55% ya vijana ambao wanahitimu kwa kujitolea JKT lakini wanarudi mtaani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na mawazo ya Bunge kwamba, kama nilivyosema kwenye hotuba yangu, sisi kupitia JKT tayari tumekaa na Wizara ya Kilimo, tayari tumekaa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Waheshimiwa Marais wetu; Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi, kwenye mkakati wa kuhakikisha Uchumi wa Bluu unakuwa ni sehemu ya kuzalisha ajira na kujenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumekaa na tunaendelea kuchambua namna ambavyo tunaweza kushirikiana kama ile MoU ambayo tumeisaini na Wizara ya Kilimo vile vile tulisaini MoU na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kutekeleza haya ambayo mmetushauri. Hivyo hivyo, hata kwenye Sekta ya Viwanda tutafanya hivyo. Pia mmetuboreshea zaidi kwamba tunahitaji kukaa hata na Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana tujadili na tuwe tuna mkakati wa pamoja ambao ikiwezekana tuulete mbele ya Kamati ambazo zinasimamia watupe ushauri halafu uwe ni mkakati wa pamoja wa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuzalisha ajira za vijana wengi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, hili tumelichukua ngoja tukalifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la exemption, hili naizungumzia pamoja na bonded warehouse. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha yupo, tutakaa tuangalie namna bora ya kuweza kulifanyia kazi jambo hili. Ni jambo ambalo linahitaji uchambuzi na kuangalia fiscal implications na nini zikoje, hata Kamati imeshauri hivyo hivyo kwa sababu ni jambo zito. Nikiri hata kwenye upande wa majeshi yetu, tukiweza kulitekeleza bila kuathiri fiscal projection za Serikali, litaleta weledi na ufanisi mkubwa kwenye majeshi yetu. Kwa hiyo, hili tumelichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwathibitishie na kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, jukumu kubwa na la msingi la majeshi yetu ni kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata kwenye masuala ya ajira, formula ya 21 kwa 79 inazingatiwa kwa 100%. Kwa hiyo, ningependa kumtoa wasiwasi kaka yangu Mheshimiwa Ussi Pondeza, labda ni kwa sababu za kimawasiliano tu lakini majeshi yetu yanaheshimu Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tutakaa pamoja na ndugu zetu upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kwamba hili jambo hata kama kuna miscommunication, linakaa sawa. Ila niwathibitishie kwamba tunaheshimu na kusimamia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia lilijitokeza suala la Shirika la Nyumbu, mmeelezea vizuri kwamba mashirika haya ukiangalia sababu za kuasisiwa kwake bado ni mashirika muhimu. Tumshukuru Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu alituelekeza na tukaandaa mpango kazi wa miaka 10 ya Shirika la Nyumbu, lakini baada ya kufanya mapitio, tumeona tunaweza tukafanya vizuri zaidi. Kwa hiyo, tunafanya mapitio ya mkakati huu wa mpango wa miaka 10 ili Shirika la Nyumbu liweze kujikita kwenye mambo ambayo yataleta tija kama tulivyo-discuss hapa.

Mheshimiwa Spika, sambamba na mkakati huo, tayari Shirika la Nyumbu liko kwenye mjadala wa kutengeneza magari ya Zimamoto zaidi kusaidia Wizara ya Mambo ya Ndani. Tumetengeneza magari ya Zimamoto matatu, tuliyafanyia testing, yanafanya kazi nzuri. Hata Shirika la SCANIA lilipokuja Shirika la Nyumbu, kwa sababu tunatumia engine za SCANIA, ilibidi waje wafanye accreditation, engine isiingie kwenye body ambayo inaenda kufanya vitu ambavyo ni substandard. SCANIA walipofika Shirika la Nyumbu walishangaa, wakasema kama Shirika la Nyumbu linaweza likatengeneza magari ya Zimamoto yenye ubora wa kimataifa namna hii, kwa nini mnaendelea ku-import? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo hili hata Kamati ya NUU wameliona, tunaendelea kushirikiana kuangalia namna bora tutakavyoshirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani kufanya import substitution ya magari ya Zimamoto taratibu kwa kadiri ya uwezo wa uzalishaji ndani ya Shirika la Nyumbu utakavyoruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile hata Shirika la Mzinga tunasema mazao ya msingi, lakini tukija huku kwenye Kamati wanaelewa mazao ya msingi ni yapi? Tunaendelea kuangalia mashirika mengine kwenye nchi rafiki ambazo tunashirikiana nazo kwenye masuala ya kiulinzi kuliwezesha Shirika la Mzinga kuweza kuzalisha mazao ya msingi zaidi yanayozalishwa hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, vile vile, tunaandaa sheria ambayo tutaileta Bungeni hapa ya Defense Industry. Sheria ambayo itakuwa facilitative kwa mashirika yetu ya kiulinzi, sambamba na kuyajengea ustawi wa kufanya vizuri zaidi na kwa kuingia partnership na mashirika mengine ya kiulinzi kwenye nchi ambazo ni rafiki, tunashirikiana nazo kiulinzi. Pia sheria hii itaangalia namna ya ku-facilitate uwekezaji wa sekta binafsi katika sekta ya ulinzi. Ndiyo maana kwenye hotuba yangu nilisema, Wizara pamoja na kuandaa sheria hii, pia tumeanza kubainisha maeneo ambayo tutaweka exclusive zone kwa ajili ya uwekezaji wa sekta ya ulinzi sambamba na hii sheria ambayo tutaileta mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Sera ya Ulinzi, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, kwenye hili naomba mtupe muda ili tulifanyie uchambuzi zaidi. Ukiangalia historia ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, wakati nchi yetu inapata uhuru, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilikuwa ni Wizara moja pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje. Walikuwa wanatumia sera moja na kulikuwa kuna sababu za msingi. Kwa hiyo, ni vizuri tukafanya uchambuzi, tukashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje kuangalia wazee hawa walipokaa na kutengeneza hii sera ambayo ni pacha, inatoa guidance kwenye masuala ya kiulinzi kwa sababu tunapolinda mipaka ya nchi ni mipaka ya nchi yetu dhidi ya nchi jirani. Kwa hiyo, suala hili ni lazima liwe na mtazamo wa ndani kulinda mipaka, lakini pia liwe na sura ya mambo ya nje.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, jambo hili kwa msukumo wa Bunge hili kupitia Kamati ya NUU, ilitufanya twende deep zaidi kuangalia na tukagundua kwamba hili jambo inabidi twende taratibu tufanye uchambuzi na tushirikiane kwa kina na Wizara ya Mambo ya Nje ili tuweze kuwa na sera ambayo itaweza kukidhi yale ambayo tunatarajia sera iweze kusaidia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, suala la ajira upande wa JKT nimeshalisema na kama tukifanya kama mlivyotushauri, itakuwa ni sehemu ya mkakati wa kutengeneza ajira milioni nane ambazo tumeziahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, vile vile katika michango ya Waheshimiwa Wabunge, mlisema nitakaposimama hapa nielezee tutajenga makambi mangapi ili kuwezesha vijana wanaomaliza Form Six kwa mujibu wa sheria kuweza kwenda JKT wote, lakini vile vile hata vijana ambao wanajitolea kuweza kupeleka idadi kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, takwimu za JKT zinaonesha miundombinu ambayo tunayo kwa ajili ya kupokea vijana wanaomaliza Form Six bado tunapokea wachache kuliko miundombinu inavyoweza ku-support. Kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuhamasisha vijana ambao wanatakiwa kwenda JKT wanapomaliza Form Six kwa mujibu wa sheria watii matakwa ya kisheria hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha tunapokea takribani 22,000 na wakati tuna uwezo wa kupokea 26,000. Kwa hiyo, kuna gap ya 4,000 lakini mtaani mtazamo ni tofauti. Upande wa vijana ambao ni kwa mujibu wa sheria, utakuta wanasema walitaka kwenda, lakini miundombinu haitoshi. Hii changamoto ya kutotosha kwa miundombinu ni kwa upande wa vijana ambao wanajitolea. Hilo nikiri changamoto ipo na tutakaa na Wizara ya Fedha na Mipango kuangalia namna ambavyo tunaweza tukasaidiwa ili kuweza kuongeza miundombinu kuweza ku-accommodate vijana wengi zaidi ambao wanajitolea waweze kupata fursa ya kupata mafunzo ya JKT. Kwa hiyo, hili tunalichukua ili tukalifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, mawazo yalikuwa ni constructive. Waheshimiwa Wabunge mmetupa ushauri mzuri, tumechukua yote na itoshe kusema kwamba tutaenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwashukuru sana Waheshimiwa Naibu Mawaziri kwa ushirikiano ambao wamenipa katika kuwasilisha hotuba hii. Vile vile nimhakikishie Mheshimiwa Mathayo, mtani wangu, tutaenda Musoma tuangalie maeneo haya ambayo ameyataja na tushirikiane kama nilivyosema, lazima tuangalie pande zote mbili. Majeshi yetu yanahitaji maeneo ya kufanyia mazoezi na kujiandaa kivita. Kwa mtazamo wa macho ya kiraia, unaweza ukaona eneo la jeshi ni kubwa, lakini kwa mtazamo wa kitaaluma ya kijeshi ni eneo dogo na majeshi yetu hayawezi kwenda nchi ya nje eti waazime eneo kwa ajili ya kufanya mazoezi. Hiyo itakuwa siyo jeshi. Kwa hiyo, mazoezi lazima wafanyie humu humu ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kushirikiana, tutatue migogoro ya ardhi baina ya wananchi wetu na majeshi, lakini pia mtusaidie kutoa elimu kwa wananchi wetu, tuheshimu maeneo ya jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimalizie. Kulikuwa na maombi maalum ya Waheshimiwa Wabunge wawili; Mheshimiwa Mathayo kwamba twende site, nitakuja.

Pia kaka yangu Mheshimiwa Rashid Abdalla Rashid, nitakuja Pemba tukaangalie maeneo ambayo umeyataja tutembelee ile skuli ambayo umesema tuitembelee. Nitumie nafasi hii kuwapongeza vijana kwa kazi nzuri wanayoifanya ya ku-perform vizuri na kupata heshima ya performance nzuri ya skuli hii. Basi nitakapokuja tutaangalia hizo changamoto za migogoro uliyoitaja ili tutafute namna bora ya kutatua changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru tena kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, naafiki.