Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana kwa nafasi hii. Ninashukuru sana nami niungane na wenzangu kuwapongeza sana Wizara ya Ulinzi lakini pia nimshukuru na kumpongeza sana Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuiongoza Nchi yetu vizuri na mpaka sasa tunaona amani na salama tunayo na tunaendelea kujenga uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru pia wewe kwa kunipa nafasi hii zaidi nichangie tu kidogo kwenye eneo moja, Kwanza niwape confidence ya Serikali kwenye eneo hili, imezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge vizuri sana hapa kuhusiana na hoja mbalimbali wote ni nia njema ya kutaka kuboresha vyombo vyetu hivi vya ulinzi na usalama na hasa Jeshi letu hili.

Mheshimiwa Spika, Vyombo vya Ulinzi na Usalama vinatambulika kwenye Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 147 (1) na (2) lakini pia ni jambo ambalo liko kwenye orodha ya Muungano katika orodha namba tatu na sambamba na hilo vyombo hivi vya ulinzi na usalama Amiri wake Mkuu kwa mujibu wa Ibara ya 148 ya Katiba ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si mwingine ni Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatambua Serikali upande wa umuhimu kubwa wa Jeshi hili la kwetu hapa la ulinzi na usalama, kwa kutambua umuhimu huo kwa sababu jeshi hili limefanya kazi kubwa ya kulinda mipaka ndani na nje ya nchi lakini pia kulinda viongozi wetu, kulinda uchumi wetu ili isitokee wakati wowote hali ambayo itapelekea kupoteza usalama wa Nchi na hivyo kurudi nyuma katika uchumi na hata kupoteza maisha au usalama wa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika suala hilo niweze kueleza tu kwenye maeneo ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge. Kwanza limezungumzwa hapa suala la kuhusiana na kodi. Niwape tu uhakika na kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba michango yote ambayo wameizungumza hasa kwenye maeneo ya kodi kwenye vifaa vya Jeshi lakini pia maslahi megine ya vyombo vyetu hivi vya ulinzi na usalama si yote ambayo tunaweza tukayazungumza hadharani hapa, kwa sababu Bunge lako Tukufu hili linaenda public, lakini kuna mambo niwahakikishie na kuwapa confidence Waheshimiwa Wabunge kwamba kama Serikali tumeyachukua tunaheshimu sana na kupokea mchango wao kwa moyo mkunjufu ili tuweze kufikisha na viongozi hawa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana husika atakutana na Waziri wa Fedha lakini pia wataongozwa na viongozi na timu nzima, kwa ajili ya kuyaangalia pia masuala haya ya kikodi yamekaaje na kuweza kuyaweka sawa sawa ili kuimarisha Jeshi letu ambalo lina heshima kubwa sana ndani na nje ya Nchi.

Mheshimiwa Spika, mnakumbuka kwenye peace keeping mission mara nyingi Tanzania tumekuwa tukipata record nzuri sana ya kufanya vizuri katika kazi za Kimataifa ambazo zimekuwa zikitokea katika Ukanda wa Afrika hata katika ngazi ya Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunatambua kwenye eneo lingine la masuala ya wastaafu ambao ni Wanajeshi, wanapopumzika sasa tunatambua wanakuwa wamechangia na wamefanya kazi kwa kweli kubwa kwa kuweka mchango wao kwa masuala ya kiusalama lakini pia ujenzi wa Taifa katika suala la uchumi. Mimi pia katika eneo hili nieleze na kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwa sababu Mawaziri wenye dhamana husika hapa pengine hawapo lakini kwa hatua hii kwa sababu sisi tuko hapa kuwakilisha hili, tunalichukua nalo na tutaenda kufanya kazi ya kufanya mapitio upya ya wastaafu wetu wa vyombo vya ulinzi na usalama ambao bado wana changamoto za kuhusiana na kupata mafao yao au kupewa stahiki zao ili kuweza kuhakikisha kwamba basi tunaona na kuheshimu mchango wao katika kipindi chote ambacho wamefanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika maeneo mengine ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na suala la fursa za ajira kwa ajili ya vijana wetu na namna ya kuweza kuunganisha na kutengeneza teamwork pamoja na Jeshi hili kwa maana ya Wizara ya Ulinzi. Hili nalo tunalichukua kwa ajili ya kulifanyia kazi na hivi yote ni kwa sababu ya maslahi mapana ya Taifa letu lakini nizidi kuhakikishia Watanzania wote wanaonisikiliza lakini pia Bunge lako Tukufu. Sisi Serikali tuko imara tukiongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu katika vyombo vya ulinzi na usalama wakati wote, tutasikiliza kwa unyenyekevu na tutaenda kutoa huduma inayostahiki kwa mujibu wa mambo yale ambayo yatakuwa yamepangwa ili kuweza kuhakikisha mipango na mikakati inawekwa sawa sawa ili kuweza kuhakikisha Taifa letu linakuwa salama pia tunaendelea kuulinda uchumi wetu wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatutakuwa na uchumi wala hatutakuwa na shughuli kama usalama utakuwa hatarini, kwa hiyo usalama ni kipaumbele namba moja cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa muda wako, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)