Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kukushukuru sana wewe Kiongozi wetu wa Muhimili huu kwa kazi kubwa ya kulitumikia Taifa kwa njia ya Muhimili wako unayoifanya. Pia, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu kabisa ambayo inagusa maslahi mapana ya amani, ulinzi, usalama na maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongrza sana Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni wazi toka Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingia madarakani chini ya uongozi wake, mipaka ya Taifa letu iko salama, ndani na nje Taifa letu liko salama, pale ambapo pamejitokeza mambo ambayo yangeweza kufanya instability ya amani ya Taifa letu Rais wetu kupitia Vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama wameendelea kusimama imara, Taifa letu liko salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri wetu wa Ulinzi, Kaka yangu Mheshimiwa Innocent Bashungwa, kwa unyenyekevu wake na uzalendo wake mkubwa uliompelekea Rais kumwamini na kumpa kuongoza Wizara hii muhimu sana katika Taifa letu. Hongera sana Mheshimiwa Bashungwa, endelea kuwa mnyenyekevu namna hiyo, uendelee kuwatumikia Watanzania kwa maslahi ya Taifa letu na kwa maslahi ya welfare ya watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba nitoe ushauri ufuatao kwa Taifa langu na kwa Wizara yangu hii muhimu ninayoipenda sana. Kwanza kabisa, takwimu zinaonesha mwaka 2016 vijana waliohitimu Kidato cha Sita walikuwa 65,000. Takwimu za mwaka jana zinaonesha vijana waliohitimu Kidato cha Sita walikuwa takribani 95,000. Ninaomba nitoe wito kwamba pawepo na mwingiliano wa Wizara zifuatazo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Kilimo, Wizara inayoshughulikia Mambo ya Vijana ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na Wizara ya Mifugo.

Mheshimiwa Spika, ninachokisema hiki ni kwamba amezungumza Kaka yangu Mheshimiwa Cosato Chumi, vijana wanaohitimu JKT, tunazungumza habari ya kujenga ajira za vijana, hili jambo ni rahisi sana, fedha ambazo Serikali inazitenga katika Wizara ya Kilimo, pakiwepo na mikakati kati ya Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo pamoja na Wizara hii iliyoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia mambo ya vijana, tunaweza tukafanya mkakati rahisi sana.

Mheshimiwa Spika, fedha za kilimo za kimkakati kwa vijana ambazo sasa hivi, kwa mfano Wizara ya Kilimo walikuwa wanakimbizana kwenda kule kwenye maeneo yetu kutafuta vijana ni jambo jema, nataka nikwambie kwa nidhamu ambayo Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania inalijenga kwa vijana wa Kitanzania, vijana wale huwa wanachukuliwa wanajenga component ya uzalendo wa nchi nzima. Wanachukuliwa kutoka Jimboni kwangu, wanachukuliwa Mtwara, Mwanza na maeneo yote ya nchi na wengi wao wanatoka vijijini, kuna ugumu gani vijana hawa JKT wakatafutiwa mashamba ya kuzalisha, wakaingizwa kwenye kilimo? Fedha zinazotokana na bajeti tunapeleka kwenye kilimo, tatizo la ajira tunalolizungumza litatafutiwa solution ya kudumu tutakuwa tumelitibu tatizo la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa wito na ninawaomba Wizara, nina imani Rais ameteua vijana mahiri tunawaamini, Kaka yangu Mheshimiwa Katambi tunajua uwezo wako, Kaka yangu Mheshimiwa Mavunde Kijana mwenzangu tunajua uzalendo na uwezo wako, Mheshimiwa Bashungwa tunajua uzalendo na uwezo wako. Fanyeni coordination ya vijana wa JKT haya mabilioni Mama Samia aliyoyatoa mama yetu aandike record ya ku-recruit vijana wengi katika kuwapa ajira wanaotokana na Sekta ya Kilimo kupitia JKT. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili nakuambia likifanyika jambo la kulia kwa sababu hamna ajira litakuwa historia na jambo hili nalizungumza ni mara ya tisa mchango huu nautoa katika Bunge hili lako Tukufu, ninawaomba Mawaziri wangu tekelezeni jambo hili litapata baraka na mtafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, pamoja na kumpongeza Kaka yangu Jacob Mkunda, Jenerali wetu na Kiongozi wetu wa Majeshi yetu, ninatoa wito kuwa dunia inabadilika, sayansi na teknolojia inabadilika, ninaamni kabisa Jeshi letu ni Jeshi lenye nidhamu limefanya ukombozi wa mataifa ya Kusini, limefanya ukombozi wa kulinda mataifa mengi dunia, natoa wito ni wakati sasa ya kuli - modernize Jeshi letu liwe na vifaa vya kisasa, adui akitaka kuweka mguu kwenye nchi yetu wakati wowote tunao uwezo wa kukabiliana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa wito, Rais wetu sasa hivi anatekeleza miradi ya kimkakati, tunajenga mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyeyere, tunajenga mradi wa SGR tunataka kwenda kwenye uchumi wa bahari, tunahitaji bahari yetu iwe salama, tunahitaji miundombinu tunayojenga iwe salama. Kwa maana hiyo, ninatoa wito tununue vifaa vya kisasa vya kijeshi tuwe na ma – artillery ya kisasa tuwe na anti-aircraft ya kisasa ili kusudi tuwe na uhakika. Taifa letu lina ulinzi na usalama wakati wote na Mungu aendelee kuwapigania wazalendo wetu wanaotoa maisha yao kwa ajili ya kulinda Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ninalotaka kulisemea ni wakati muafaka sasa Jeshi letu la Wananchi lipewe fursa ya kujenga chuo cha kisasa, Chuo Kikuu cha kisasa kitakachoweza kutoa mafunzo ya teknolojia ya kisasa Jeshini. Itakayoweza kutoa mafunzo kwa wanajeshi wetu kuji-equip na teknolojia za kisasa kwa sababu dunia imebadilika. Mambo ya kutumia mavifaru yale ya mwaka 1961 yameshapitwa na wakati, dunia sasa hivi imekwenda mbele. Ninatoa wito Jeshi letu litengewe bajeti kwa siku zinazokuja, wajengewe chuo cha kisasa kitakachoweza kutoa mafunzo ya kiutalaam ya Wanajeshi wetu ambao baadhi yao ndiyo watakwenda kui-feed Nyumbu, hao baadhi yao watakwenda ku- feed vyuo vyetu vya kisasa ambavyo Jeshi letu linavimiliki kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho siyo kwa umuhimu lakini ni la mwisho, nilikua naomba nitoe ushauri. Naomba hili ya vijana nililolizungumza wa JKT katika miradi niliyoitaja tuwekeane malengo. Tuseme kwa mfano, mwaka huu umemaliza vijana 95,000 katika sekondari zetu za high school, tunaweza tukasema mwaka huu tunaweka project ya miaka kumi, mwaka huu wa kwanza tutaanza na asilimia 33, mwaka unaokuja asilimia 40 na kuendelea, nataka nikuambie Mawaziri hawa wazalendo vijana wenzangu watakuwa wamesaidia Taifa hili kuweka record kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niwapongeze sana Jeshi la Wananchi wa Tanzania, nimeona leo Mabregedia Jenerali wanawake, nimeona leo wanawake wakitajwa humu kwenye Jeshi lao lakini kubwa zaidi nimefarijika sana na mimi nataka niwaambie nasi humu Bungeni tunae Brigedia Tulia. Huko nje mnaupiga mwingi na sisi humu ndani yuko Brigedia Tulia anaendelea kufanya kazi ya kizalendo na hivi karibuni Taifa na watu wake tunamuombea Brigedia huyu akaongoze chombo kikubwa duniani akawe Rais wa Bunge la Dunia, ama namna gani jamani Wabunge? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niwaombe Jeshi la Wananchi wa Tanzania hawa Makamanda tumewaona wamekuja hapa, tumeona wamechukua mikanda ya medeni kwenye kupigana, wapo akina Simbu wamechukua medani kwenye riadha. Jeshi Kamanda Mkunda nakuomba unanisikiliza Kaka yangu pamoja Waziri hembu nendeni mkawa - promote hawa vijana. Tunataka tuwaone kwa kazi kubwa wanayoifanya vijana hawa waje Bungeni wamechafuka nyota, wanaleta sifa na heshima kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru, Mungu Ibariki Tanzania, Mungu libariki Jeshi la Wanachi wa Tanzania, Mungu mbariki Amiri Jeshi, Rais Mama yetu Daktari Samia Suluhu Hassan, amani ya Taifa letu iendelee kutawala. Ahsanteni kwa kunisikiliza. (Makofi)