Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia siku ya leo katika Wizara yetu. Nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais ambaye ndiye Amir Jeshi Mkuu wa Taifa letu na mara kadhaa nimesema hapa Mheshimiwa Rais kama mwanadiplomasia namba moja amekuwa akiitendea haki nafasi yake kwa sababu tumeendelea kuwa Taifa ambalo linaaminika katika ulinzi wa amani duniani, katika ulinzi wa amani katika nchi mbalimbali za kiafrika. Hii ni kutokana na kazi nzuri ambazo Mheshimiwa Rais anazifanya kuendelea kutuheshimisha katika Jumuiya ya kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kama jina lake lilivyo Innocent yuko very innocent, msikivu na Kamati tunafanya nae kazi vizuri sana pamoja na Katibu Mkuu Faraji Mnyepe na viongozi wa Jeshi kwa maana Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda, pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi Luteni Jenerali Salum Haji Othuman ambae mara nyingi tumekuwa nae kwenye vikao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiona nchi imetulia kama alivyosema Mheshimiwa Ngasa, tunafanya shughuli zetu, tunashiriki kazi za Bunge, wakulima wanaenda mashambani, wananchi wangu Mafinga wanaenda kuchana mbao na kadhalika, maana yake wako watu hawalali usingizi. Kati ya watu ambao hawalali usingizi ni pamoja na wenzetu wa Jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huwa namwambia mtu, ukimwona Mwanajeshi vyovyote alivyo wewe mheshimu tu, awe na maji ya kunde kama mimi, kimo cha kati kama mimi vyovyote alivyo mheshimu tu, kwa sababu wanafanya kazi ya kutukuka ya kukesha. Sisi hatuwezi kujua tutakwenda huko masokoni, tutakwenda kunywa soda na kadhalika, tutakwenda kwenye ibada tutakwenda kufanya kila kitu lakini kuna watu ambao wanakesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hii kama alivyosema Mheshimiwa Fakharia, kazi ambayo imefanyika pale Ikulu ni mojawapo wa mfano kwamba, vyombo vyetu vikiaminiwa na kuwezeshwa vinaweza vikafanya maajabu makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe ushauri ambao nimetoa nadhani kama mara tatu mfululizo. Kama ambavyo umeona ile kazi ya Ikulu ya kuheshimisha, nenda Chita utaenda kuona maajabu, kwa wale ambao wamefika wanaweza kujionea jinsi ambavyo kilimo cha mpunga kinafanyika kwa weledi mkubwa sana. Ndiyo maana mara nyingi nashauri na nimesema hata mwaka jana, hii nchi yetu mimi nilisikitika na lazima niseme ukweli, Waziri wa Viwanda na Biashara anatoa vibali tuagize mchele tani 90,000 Tanzania, kuna vitu Hapana! Sasa, namna ya kusema hapana ni nini? Tuwekeze JKT, nilisema mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwezesheni JKT na kupitia SUMA JKT, wape target tu miaka miwili uone kama utaagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi hii, uone kama utatoa vibali vya kuagiza mchele kutoka nje. Tumefanya mambo mangapi kwa majaribio? Hebu tufumbe macho tukipe mkopo, tukiwezeshe, tuone maajabu.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Cosato Chumi, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Felista Njau.

TAARIFA

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nataka nimpe mchangiaji taarifa kwamba kwa ukosefu wa fedha JKT wana hekari 12,500 lakini mwaka huu imekuwa ni pori na miundombinu iko ardhini, kwa hiyo wamekosa fedha wangekuwa na fedha wangeweza kwenda mbele. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Cosato Chumi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili na huyu kama Mjumbe wa Kamati nadhani amenielewa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachotaka niseme ni nini? Kama Taifa kijiografia tunayo nafasi ya kunufaika na kuneemeka kutokana na geographical position, sasa miongoni mwa watu wanaoweza kutusaidia ni hivi vyombo, lakini hawawezi kutusaidia kama hatuviwezeshi ipasavyo. Ushauri wangu ni kwamba tuviwezeshe hivi vyombo na tuwape fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili na hili napenda kwa dhati ya moyo wangu nikushukuru wewe binafsi. Mimi na baadhi ya wenzangu tulienda JKT mwaka jana, hapa ndipo ambapo nataka nitoe ushauri na nisisitize. Kumekuwepo nafasi haba za vijana kwenda JKT wanaomaliza Kidato cha Sita, mara nyingi pengine kwa kukosa uelewa tunaona kama vile JKT imewanyima nafasi vijana, Hapana! Hawana vitendeakazi, hawana facilities. Kwa hiyo, nashauri Wizara ya Fedha tuwawezeshe JKT wajenge mahanga ya kutosha ili kusudi vijana wengi waende JKT.

Mheshimiwa Spika, zamani nilidhani JKT ni maguvu tu, lakini tulienda pale unakaa darasni wakati mwingine mpaka saa nne usiku, unafundishwa uzalendo, kuna vitu vingi. Kwa nafasi hii ninashauri na pengine ushauri huu unaweza usipokelewe vizuri sana, hata Watumishi wa Umma wanapoajiriwa kama ambavyo tunafanya semina elekezi, waende JKT hata mwezi mmoja. mimi nakwambia tutaona mabadiliko makubwa sana katika nchi yetu, kwa maana ya mindset, tabia, utendaji na uzalendo kwa ujumla. Simaanishi waliopo kwamba siyo wazalendo lakini itawaongezea uzalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia yapo mambo mawili. Jana tumejadili Wizara ya Uchukuzi hapa na tumesema mambo muhimu ambayo tunatakiwa tufanye katika kuboresha bandari yetu. Wenzetu hawa wakileta vifaa tayari wamekwisha jenga bonded warehouse, tunaomba na tunaishauri Serikali waruhusiwe wakishachukua vifaa vyao vya Jeshi wakavihifadhi kwenye bonded warehouse wakati taratibu zingine zinaendelea, tusivi – expose pale.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni la kisheria, tuniomba Serikali ilete sheria ili kusidi vile vifaa vya wenzetu visitozwe kodi. Kwa sababu kama alivyosema Mheshimiwa Zahor, ukisema tu ni military equipment mwingine anadhani ni vile vifaru tu hata buti ni kifaa cha Jeshi. Kwa hiyo, niombe sana kama naeleweka hii tuone haya mambo mawili. Moja, hili la kwanza nadhani ni administrative tu kwamba bonded warehouse zao wanazo zitumike kuhifadhia vifaa vyao na hilo la TRA.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni la wastaafu. Mimi napokea maombi kutoka Mafinga, sasa kidogo inanichanganya maana ni Mjumbe wa Kamati, nimepokea recently wakati tumeshamaliza Vikao vya Kamati, nikiwauliza wastaafu waliokuwa Wanajeshi kwanza wanaomba kwamba ile pensheni yao wanadhani kwa kuwa walistaafu wakiwa katika vyeo vya chini na wengine walilazimika kustaafu labda kutokana na maradhi kwa hiyo ile pesheni yao ni nyembamba kidogo. Kwa hiyo, wana ombi Serikali iwaangalie wastaafu pia kuwafikishia kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia niliona hapa timu ya JKT, imepanda Ligi Kuu, mimi ni mwanamichezo nampongeza sana Kocha Ndugu Malale Hamsini pia na JKT Queen ya wanawake Kocha Ali Ali kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana, naunga mkono hoja na Mungu akubariki sana. (Makofi)