Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa naunga mkono hoja yetu hii ya Wizara ya Ulinzi. Imesomwa na Mheshimiwa Waziri, yuko vizuri, yuko sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea Amiri Jeshi Mkuu, Mama yetu Mama Samia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nimshukuru sana kwa kazi anayoifanya. Amani ya nchi ina mambo mengi katika kuhakikisha amani inakuwepo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Moja katika kazi kubwa kabisa inayofanyika ni pamoja na Mama kutengeneza au kujenga au kuwa na mahusiano mazuri kabisa na nchi zote za Afrika ikiwemo nchi zilizotuzunguka. Hiyo yote ni sehemu moja katika kuona kwamba, Watanzania wanaishi kwa amani kufungua fursa za nchi, wakishirikiana na Jeshi letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili ni pia, nimshukuru Mkuu wetu wa Majeshi, CDF General Nkunda kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na timu yake nzima, Luteni General Salim Othman, ma-Meja Generals wote, ma-Brigadier Generals wote, ma-Kanali wote, ma-Meja wote kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya amani ya Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, amani ina mambo mengi na moja katika eneo ambalo wanatusababishia, ukiacha Mungu mwenyewe, amani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mungu mwenyewe ametupa zawadi kwamba, Tanzania ni moja katika nchi chache Afrika au duniani ambazo mpaka sasa hivi zina amani na tunaishi kwa raha. Kama ni wafanyabiashara, kama ni wafanyakazi, na namna yoyote ile tuko kwenye amani kubwa sana. Moja katika sababu kubwa kabisa ni Jeshi ambalo wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha amani inakuwepo katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taharuki niliwahi kusikia huko Kusini, kuna wakati ilitokea taharuki hapa na pale, kazi kubwa ilifanywa na Jeshi letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuna vijana kule wanakaa 24/7 wanakaa kwenye mapori mazito yale kuhakikisha wako tayari kujitoa muhanga, wako tayari kupoteza maisha yao kwa ajili ya amani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hapa tunapokaa tunaona Bunge hili, Bunge hili linakaa kwa sababu ya amani ya Jeshi hili la Jamhuri ya Muungano wakiongozwa na General Nkunda katika kuhakikisha kwamba, hata Kusini kule taharuki iliyokuwepo Kusini kule amani inakuwepo. Hata wananchi wa Mtwara amani ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna vijana wetu wako hata Msumbiji wanakwenda kutoa ushirikiano mkubwa sana kwenye Jeshi la Msumbiji ili kushirikiana na Jeshi ambalo liko hapa Tanzania kuhakikisha eneo lile ambalo liko Kusini kule linaendelea kuwa na amani. Amani katika nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kambi zile ambazo ziko Kusini, zote ni Watanzania vijana wako zaidi ya 1,500 ndani ya Msumbiji wakitoa ushirikiano, wakitoa mafunzo na Watanzania wanajeshi wanashirikiana pale kuona kwamba amani inakuwepo.

Mheshimiwa Spika, ninamuomba tu Mheshimiwa Waziri, operation kama hii ni gharama kubwa sana, Jeshi hili linafanya kazi kwa weledi, kwa uzoefu, kwa uzalendo, nikuombe tu kwamba kama kuna namna ambayo kuna mapungufu ya kulihudumia Jeshi hili kwenye aina hii ya operation peke yake huku Kusini, hebu jaribu kuona kwa sababu bado mwezi mmoja, hotuba yako na hotuba ya Kamati imeelezea kwamba, bado kuna fedha wanahitaji ili kukamilisha mambo yao waliyojipangia katika maendeleo yao. Bado sasa hivi ni kama mwezi mmoja mpaka kufikia Tarehe 30 mwezi wa Sita, kuna tatizo gani, kama ni Waziri wa Fedha yuko hapa, mkahakikishe kwa muda huu fedha ambazo zimebaki wakapewa, lakini specifically Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha hoja yako hapa itapendeza sana, sina mashaka na wewe kabisa Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi, lakini kama watakuwa na mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, kuboresha Jeshi la Tanzania kutoka tulikotoka tulipo hapa sasa hivi tukawa katika Jeshi bora Afrika na Tanzania. Kwa maana ya kwamba, kubadilisha mitambo, kubadilisha zana, kuwa na mawasiliano, Jeshi likawa la kisasa zaidi.

Mheshimiwa Spika, specifically kwenye operation hii nimuombe Mheshimiwa Waziri kama kuna uwezekano waongezewe fedha angalao hata kama bilioni 150, specifically naongelea kwa ajili ya operation hii ya Kusini mwa Tanzania. Sasa utakapokuja kuhitimisha hapa Mheshimiwa Waziri, kama utakuwa na namna ambayo utaiweza sisi Wabunge tuko hapa na tuko tayari kukuunga mkono. Kama utakuwa na mipango mizuri tutakuunga mkono wala hatuna shida na wala sina mashaka kabisa na wewe pamoja na Serikali ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ameongea hapa kwa maana sasa wamekubaliana kwamba tutaingia partnership na private sector katika kuliendeleza Jeshi. Niliwahi kuongea na niliwahi kushiriki Bunge hili wakati ule, mwaka juzi kwenye bajeti na nikasema Jeshi letu la Tanzania wana uwezo mkubwa mno wa kutengeneza silaha ndogondogo, wana uwezo mkubwa mno wa kutengeneza hata risasi, wana uwezo mkubwa mno wa kutengeneza hata magari, lakini pale ambapo kutakuwa na mpango mzuri wa kushirikiana na sekta binafsi, iwe nje ya nchi iwe ndani ya nchi, uwezo huo upo. Hawa wenzetu wamewezaje?

Mheshimiwa Spika, kuna nchi hapa jirani wanajipambanua hivi, lakini sisi ndiyo tuliowafundisha, tuliowaweka pale na tuliwasababisha wakakaa vizuri. Leo wanakuwa na mipango mizuri kuliko hapa, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri awe na mipango hiyo. Na uwezo mkubwa kabisa, Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapo wasomi wazuri, Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wana uwezo mkubwa sana, wamo ma- engineer wazuri sana, ni suala tu la kukaa, kuwa na mipango, tunafanyaje, unahitaji fedha, kama kuna private sector inakuja, lete Bungeni tupitishe waende wakatengeneze hayo mambo ambayo watakuwa wamejipangia. Tukianza kutengeneza silaha, tukawa na risasi, tukawa na mambo yote hayo, hata magari, hata zana, hatuwezi kushindwa, lakini tukawa na mpango wa muda mrefu tunakuwa tunajihakikishia kabisa kwamba, tunaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi kama Egypt leo wanatengeneza silaha nyingi tu, wanatengeneza risasi nyingi tu, tunashindwaje sisi? Tanzania ina historia kubwa ya kuleta uhuru Kusini mwa Afrika, tunashindwaje sisi? Leo hapa nchi jirani hapa tuna mawasiliani mazuri. Jeshi la Tanzania lina historia nzuri sana Afrika, Jeshi la Tanzania lina historia nzuri sana kuleta uhuru nchi zote za Kusini mwa Afrika, tunashindwaje kufanya hivyo, ni suala la mipango tu.

Mheshimiwa Spika, mimi sina mashaka na uongozi wa Jeshi wako vizuri sana, tukiamua kwa pamoja, mkiamua kama Wizara kwa pamoja tutoke kwenye Jeshi lililopo sasa hivi standard hii tuihuishe ipande kabisa liwe Jeshi la kisasa, wawe na mitambo ya kisasa, wawe na mawasiliano ya kisasa, yaani liwe Jeshi la kidijitali kutoka kwenye Jeshi la analogia ambalo tunalo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, ukishakuwa na mipango ya kati, mipango ya muda mrefu, Jeshi hili litakuwa Jeshi moja zuri sana. Bahati nzuri sana heshima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nchi za Afrika ni kubwa mno. Suala la kuwa na amani mimi sina matatizo kwa sababu amani ipo, lakini unapokuwa na jeshi zuri ni back up ya kuwa na amani ndani ya nchi na hata nchi jirani wanajua kabisa Tanzania pale Jeshi ni zuri hakuna sababu ya kuleta fyokofyoko, tukileta fyokofyoko tunafyatuliwa. Kwa hiyo, suala la kuwa na Jeshi imara ni moja ya back up kubwa sana kusababisha amani ndani ya nchi, Ukiachana na Mama Samia anavyohangaika kutengeneza diplomasia nchi za Afrika na duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuboresha maslahi ya wanajeshi na hasa hawa ambao wanaingia kwenye operations za moja kwa moja, kuwepo na mipango mahsusi kabisa hawa ambao wanakwenda kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya nchi yetu, hawa ambao wanakaa kule kwa ajili ya nchi yetu, hawa hebu tuone maslahi yao yamekaaje kwa maana ya maslahi yao, kwa maana ya zana za kisasa…

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga hoja mkono, ahsante sana. (Makofi)