Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Emmanuel Papian John

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. EMMANUEL J. PAPIAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Maana nimekaa muda mrefu naona wanaongea mara mbili mara tatu mimi nakosa nafasi, lakini nashukuru kwa kupata hiyo nafasi.
Kwanza niwapongeze wananchi wa Kiteto kwa kunichagua, wale wananchi wamenipa kura nyingi, wameniamini. Wananchi wa Kiteto nawashukuru sana na naendelea kuwaombea na naahidi kwamba nitawatumikia kama ambavyo wameniamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia upande wa kilimo kwa sababu kwanza ni bwana shamba, ni mkulima, ni mfugaji, nina uzoefu kwenye kilimo zaidi ya miaka 25. Kilimo cha nchi hii kimeshindikana, lakini nadhani kuna mahali ambapo yawezekana tumejichanganya, hebu tufikirie ni wapi tumekosea. Nchi hii sasa hivi tuna- import zaidi ya asilimia 60 ya mbegu za mahindi na mbegu za aina nyingine. Tunapolalamika, tumejiuliza kwamba sasahivi tumejiuliza habari ya pembejeo, lakini hata huyo msambazaji wa pembejeo atapata wapi hizo pembejeo. Nchi nzima hakuna mbegu asilimia 60, tunayo ardhi ya kutosha, tunao wataalamu, tunazo benki kwa nini watu wetu hawawezi ku-invest kwenye kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali haijachukua jukumu la kuwabinafsishia watu maeneo wakaweza kuendesha kilimo cha kuzalisha mbegu kiasi kwamba mbegu zikatosha na usumbufu ukapungua kwa wakulima wetu. Kuna Kanda ya Ziwa ukiangalia Kigoma, ukaangalia Kagera, ukaangalia ile kanda ya Kibondo nzima, mvua zinatosha, tungeweza kutenga maeneo, ule ukanda wote tukaweza kuzalisha mbegu, zikaweza kusaidia nchi yetu kwa maana ya kilimo, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Benki ya Kilimo imeanzishwa, ukiangalia mtaji wa Benki ya Kilimo, ukikopesha watu utakopesha watu ambao hawazidi 10, 20 hii benki na jinsi ambavyo tunawakulima na asilimia kubwa ya watu wetu ni wakulima na wafugaji hebu niambie kwa mtaji huu tunakwenda wapi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hamisheni pesa zilizoko kwenye ile Benki ya TIB, zipelekwe kwenye Benki ya Kilimo, kopeni pesa ingiza kwenye ule Mfuko, ruhusu wananchi wetu wakakope waweze kufanya kazi. Hata tutakapokwenda kutoza kodi, kuna kitu cha maana cha kutoza kwa sababu watu watakuwa wamezalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, benki nyingi za kibiashara zimeweza kukopesha wakulima na wakulima wengi wamefeli kwa sababu ya riba kuwa juu. Hata hivyo, jambo kubwa na shida kubwa hapa inaonekana ni kwa sababu hizi benki, Benki Kuu imekuwa inakopa, inaweka government guarantee na bado hazilipi zile benki na zile benki kwa sababu zinaogopa kufilisika haziwezi kushusha interest, mkulima na mfugaji wataponea wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Benki Kuu haiwezi ku-gurantee, iki-guarantee hailipi zile benki, hicho kilimo kitaenda wapi, watapunguza riba waende wapi na wanapesa za watu! Naomba kushauri, Benki ya Kilimo iimarishwe, mitaji ihamie huko, watu wakakope huko, wakachape kazi. Ukimaliza unawaandikisha VAT na TIN halafu wanalipa kodi kwa raha zao, wanaendelea kutambaa kwenye nchi yao kwa neema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto tunazalisha mahindi kwa maana ya kulisha central zone including Dar es Salaam, Morogoro, Arusha na Manyara. Awamu iliyopita, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alizungumza suala la kutujengea lami kutoka NARCO kwenda Kiteto ili mazao yaweze kutoka kwa salama. Mpaka leo hii barabara tumeimba, tumeomba, nimemwambia Ndugai, Ndugai amelia Bungeni, imeshindikana barabara, hebu niambieni hii barabara inajengwa lini niende kuwaambia wananchi. Maana Magari yanaanguka sasa hivi madaraja yemekwisha, magari yameanguka, chakula cha msaada kimeshindwa kwenda, watu watakufa njaa, barabara imekufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa mniambie leo, mimi sijui cha kuwaambia. Maana wananchi watakuja wenyewe hapa hapa maana Kiteto ni karibu hapo, wakiamua saa nne wako hapa, sasa mniambie niwaambie nini, hii barabara kwa nini haijengwi na sisi tunalisha watu? 90 percent ya mazao yanayokuja NFRA hapa yanatoka Kiteto, lakini Kiteto imegeuka vumbi, sisi hatuna benefit yoyote kwa sababu hata wananchi wetu hizi barabara wamezikosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu amani; Kiteto ni Darfur ndogo. Bunge lililopita wame-debate, mapigano ya wakulima na wafugaji watu wamekwisha. Nataka kuiuliza Serikali iniambie leo tunafanya nini ili kuhakikisha kwamba amani inatengemaa Kiteto, wakulima na wafugaji waweze kubaki salama?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Emmanuel hebu tulia kidogo. Tafadhali usiite Kiteto ni Darfur ndogo, wote tunajua nini kinaendelea Darfur, tafuta mfano mwingine tafadhali.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Haya nimefuta, lakini si zilipigwa na wewe unajua? (Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ukishafuta usiendelee tena na maneno mengine, futa uendelee kutoa hoja yako.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Haya nimefuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto watu wameumizana, lakini katika mambo ambayo yamesababisha ile Kiteto watu waumizane ni pamoja na viongozi, watendaji wa Serikali kushindwa kufanya kazi. Katikati ya mgogoro wa wakulima na wafugaji kuna watu wana-benefits ndani ya haya. Wanashindwa kufanya kazi za sehemu zao ili amani iweze kupatikana na kusema ukweli na kuusimamia. Hapa watendaji wa Serikali tuamini, tuseme waliteleza na walishindwa Serikali kuchukua hatua kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu NGOs. Kiteto kuna NGOs zinapenyeza penyeza zinakuja, wanazungumza, mara tunataka hifadhi ya nyuki, mara pingos, mara nini, kila siku wamo, wanazunguka, wanaita makundi machache, wanafanya vikao, wanalipana posho. Mmoja akiulizwa Mbunge wenu yuko wapi, wanasema, Mbunge tumechelewa kumpa taarifa kwa sababu ilikuwa ni haraka haraka. Mipango na haya mambo yanayopangwa ndani ya ile Wilaya, ndiyo matokeo ya kumaliza watu yanayoendelea sasa hivi.
Niombe Serikali iliangalie hili, Serikali ifungue macho ione lakini ichukue hatua za haraka na za makusudi kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni wanasiasa. Siasa zinazochezwa Kiteto zimekuwa ni za kihuni, sasa hivi tuko salama. Sasa niombe Serikali inisaidie, wale wanasiasa uchwara wanaokuja kutembeza siasa pale, tupige siasa wakati wa siasa, lakini wakati wa kazi, tuchape kazi badala ya kugombanisha wakulima na wafugaji. Wewe ukitafuta siasa, njoo wakati wa siasa tupige, tukimaliza tuhimize amani, tuhakikishe kwamba watu wote wana uwezo wa kufanya kazi, mkulima aende shambani, mfugaji aende shambani. Niombe Serikali inisaidie kupima ardhi ya Kiteto vizuri, iipime yote, mkulima ajue anaishia wapi na mfugaji ajue anaishia wapi, mwisho wa siku sisi tuijenge amani na Serikali isimame katikati kutekeleza hilo, huu muda wenyewe ni mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie afya, hospitali ya Kiteto, tumeomba pesa, tumeahidiwa, tumeambiwa, sasa tumechoka. Tunaomba jamani ile hospitali ikarabatiwe maana sasa hospitali itakuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko pale. Wodi ya wanaume iliyoko pale imechanganya na wale wagonjwa wa TB (Tuberculosis), wote wanachanganyika humo humo, sasa wale watu wataponea wapi? Aliyejeruhiwa ameanguka na pikipiki humo humo, aliye kwenye dozi ya TB yumo humo humo. Sasa tutajengewa lini hii wodi za wanaume zitenganishe hawa watu ili wananchi wasiweze kuambukizana magonjwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali inisaidie na Waziri wa afya, hakikisheni kwamba mnaweza kunitatulia huu mgogoro na ile hospitali ikarabatiwe maana sasa imefika mahali tunafanya repair tunazibaziba wenyewe, tunakwenda huko tunakarabati mahali, tunasogezasogeza ili lile jengo lisije likaangukia wagonjwa halafu tukaongeza wengine tena wodini, tukaongezea yale magonjwa wanayoumwa, halafu tunaongezea mengine tena ya jengo kuwaangukia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine tulilonalo Kiteto ni la maji. Kata za Dongo, Songambele, tumechimba visima, ile nchi ni kame. Hebu Serikali iangalie mfumo mpya wa kutusaidia, ile nchi ni kame, wamechimba visima havifiki. Visima vilivyochimbwa vikipatikana maji havifungwi mapampu ili watu waweze kupata maji. Niombe Serikali iweze kuliona hili kwamba kama inawezekana, tuchimbiwe mabwawa ya kutosha, watu watatumia maji na mifugo itatumia maji hayo hayo ili angalau tuweze kuokoa maisha ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ndani ya Mji wa Kibaya; ule mji Rais ametuahidi visima kumi, ametuahidi pesa, vile visima vimeshindikana. Sasa ule Mji wa Kibaya mnataka watu waende wapi, imeshindikana, watu hawapati maji na tumeahidiwa maji muda mrefu sana. Naomba Serikali iweze kuliona hili ule Mji wa Kibaya uweze kuokolewa maana watu wameongezeka, maji hatuna, tuna visima viwili, maji hayatoshi, watu wanabeba ndoo, akinamama wameota vipara. Na mimi niliwaahidi akinamama nikiwa Mbunge mtaota nywele mwanzo mwisho. Naomba Serikali ichukue jukumu la kuhakikisha kwamba hawa akinamama wanaota nywele kichwani. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha. Sasa atafuata Mheshimiwa Jamal Kassim Ali.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)