Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa wachangiaji wa hotuba hii ya TAMISEMI. Kwanza kabisa, niwapongeze Mawaziri wote wawili katika Ofisi hii ya Rais (TAMISEMI) na nasema bado mapema kabisa naunga mkono hoja hii isipokuwa tu kuna sehemu nataka nitoe ushauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 16 tumeona kwamba sasa hivi Halmashauri zetu zote zinataka zitumie mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato, jambo jema sana. Pia tumesikia hotuba mbalimbali za Mheshimiwa Waziri Mkuu ambazo zinahitaji sana msaada wa kutoka katika Wizara hii. Tunajua Serikali ina nia nzuri sana na ndiyo maana inaanzisha maeneo mapya kama vile mikoa na wilaya. Hata tunaposema kwamba hotuba ya Waziri Mkuu inahitaji msaada mkubwa kutoka TAMISEMI, kwa mfano ile kusema kwamba tutafuta Halmashauri zile ambazo hazikusanyi mapato yanayotakiwa, naiomba Wizara ya TAMISEMI imsaidie Waziri Mkuu, kwanza ianze kufuta wafanyakazi wabovu kwenye hizi Halmashauri za Wilaya kabla ya kufuta Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukianza kufuta Halmashauri kabla ya kufuta wafanyakazi wabovu mtakuwa hamjatutendea haki. Wafanyakazi kwenye Halmashauri ni wabovu, wamechoka hasa ukichukua kwa mfano Halmshauri yangu ya Gairo, kuanzia Mkurugenzi, Afisa Mipango, Mweka Hazina wote hakuna kitu. Sasa kwa kweli utategemea Diwani au Mbunge atatoa ushauri gani wa kitaalam ili hiyo Halmashauri iwe na mapato? Cha msingi kwanza tuangalie hawa watendaji wetu, watendaji ni wabovu, lazima tukubaliane.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata nikisoma kwenye hiki kitabu cha Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kusema kwamba kuna Halmashauri zingine zina hati nzuri, zingine hati kidogo za mashaka, zingine hati chafu, ukiangalia ukweli Halmashauri zote zina hati chafu tu. Huo ndiyo ukweli. Ndugu yangu Mheshimiwa Simbachawene nakujua uhodari wako, naomba uziangalie kwa umakini sana Halmashauri, ndiyo kwenye mchwa, wanapewa pesa nyingi na Serikali na zote zinaishia huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tujaribu kuziangalia hizi Halmashauri mpya kwa jicho la huruma, tumeanzisha Halmashauri nyingi sana. Nitoe mfano wa Halmashauri yangu ya Gairo toka ianzishwe mpaka sasa hivi haina hata gari. Wakati tuko Halmashauri mama ya Wilaya ya Kilosa tunagawana pale, tumepewa magari sita na mpaka sasa hivi linalotembea ni moja tu na lenyewe ukipanda kilometa saba unasukuma kilometa saba. Kwa hiyo, Mkurugenzi hana gari, kituo cha afya hakina ambulance, hebu mtufikirie, mtuonee huruma hizi Halmashauri mpya, tupeni vitendea kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika ukurasa wa 32 wa hotuba ya Mheshimiwa Simbachawene amezungumzia kuhusu habari ya Hospitali za Wilaya, hapa nchini Hospitali za Wilaya ziko 84 tu, wilaya 97 zinatumia hospitali za taasisi za umma au za dini. Kwa mfano, kama pale Gairo, Wilaya ya Gairo inategemewa na wilaya nyingi za pembeni kwa mfano Kiteto, Kilindi, Kongwa na Mvomero wote wanategemea sana pale Gairo lakini Gairo pana kituo cha afya na toka tuanzishiwe wilaya ile hatujapata fungu la aina yoyote la kujenga Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Gairo tuna kituo cha afya ambacho kinatoa huduma za hospitali pamoja na operesheni pamoja na vitu vingine lakini hatuna ambulance na Gairo ni kama Tumbi pale maana ni katikati ya Morogoro na Dodoma. Sasa mnataka mpaka kiongozi aje avunjike miguu pale ndiyo muone umuhimu wa Gairo kwamba panatakiwa ambulance? Tunaomba tupate ambulance na tupewe fungu la kijenga Hospitali ya Wilaya ya Gairo. Tumeshaomba sasa hivi ni zaidi ya miaka miwili, huu wa tatu, hatujapata. Tunaomba sana mtufikirie kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye upande wa barabara, sasa hivi kila Mbunge anataka barabara yake ihame kutoka TAMISEMI ipandishwe hadhi iende TANROADS. Ilitakiwa TAMISEMI mjiulize ni kwa nini Wabunge hawataki barabara zao ziwe TAMISEMI au ziwe chini ya Halmashauri? Utakuta kilometa tano inayotengenezwa na TANROADS na kilometa tano inayotengenezwa na Halmashauri ni vitu viwili tofauti na ndiyo maana Wabunge wote hawataki barabara sasa hivi ziwe chini ya Halmashauri. Kuna maombi zaidi ya 3,400 ya kupandisha daraja barabara ili ziwe chini ya Barabara za Mikoa kwa sababu huku kwenye Halmshauri ndiyo kwenye mchwa wa kula pesa zote za barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata mgao wa pesa ukiangalia utakuta Wilaya kama ya Gairo na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri anaifahamu vizuri sana Wilaya ya Gairo, anafahamu kuanzia Gairo mpaka Nongwe, anaijua vizuri sana milima yake ile ilivyo inazidi hata milima ya Lushoto. Mwaka jana tumeomba shilingi bilioni 1.5 tunakwenda kuwekewa shilingi milioni 400 na katika hizo mpaka sasa hivi imefika shilingi milioni 22. Sasa hata huyo mama aliyeko hapa TAMISEMI, anayeangalia hizi barabara za Wilaya sijui mmemuweka tu akae, hatembei au hajui mazingira ya hizi wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nashauri itengenezwe agency ambayo itakuwa ina mamlaka ya kuzisimamia barabara za TAMISEMI na kuangalia ubora wake ili Wabunge tusiwe tunaomba barabara nyingi ziwe chini ya TANROADS. Pawe na kitu ambacho kinasimamia ufanisi wa barabara vinginevyo tunakuwa tunaacha watu wanakula hela tu. Utakuta barabara ya TANROADS ina shilingi milioni 200, ya Halmashauri ina shilingi milioni 300 lakini ya TANROADS ina kiwango cha juu na hao hao Ma-engineer bado wapo, usimamizi mbovu, lazima kitengenezwe chombo ambacho kitasimamia hizi barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye bajeti hii, nikisoma katika hiki kitabu, Ofisi ya TAMISEMI, fedha za 2016/2017, ukienda kwenye kilimo hapa utakuta Wilaya ya Ilala imetengewa shilingi milioni 100, Wilaya ya Kinondoni shilingi milioni 148, Wilaya ya Temeke shilingi milioni 113, halafu ukija hapa Wilaya ya Gairo shilingi milioni 15, ina maana Temeke wanalima sana kuliko Gairo? Kinondoni, Ilala wanalima sana kuliko Gairo, haiwezekani! Angalia, ukisoma humu utakuta miji mikuu imewekewa hela nyingi sana za kilimo kuliko zile wilaya. Sasa nafikiri haya mambo tujaribu kuyaangalia hayako sawasawa kabisa. Hivi hapa kuna sehemu inalima viazi kuliko Gairo katika nchi hii, kuna sehemu inalima mahindi mazuri kuliko Gairo, acha mahindi ya wapi sijui huko hayakoboleki hayo. Kwa hiyo, naomba hili liangaliwe kwa umakini zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.