Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba au kuchangia makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Rais na nianze na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwanza, nakubaliana na makadirio ya matumizi ya Wizara hii, naunga mkono kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwanza kabisa niwape pongezi kwa kazi kubwa wanayofanya, wanafanya kazi kubwa ambayo ni ngumu, Mheshimiwa Waziri Simbachawene naona kwa kweli anapambana, anastahili sifa ya pekee, nimpe hongera kwa kazi kubwa anayoifanya. Mheshimiwa Waziri naomba aendelee kupambana asiwe discouraged na maneno ya watu, aendelee kufanya kazi kwa ufanisi, Watanzania wanasubiri huduma yake kwa hali na mali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kutoa baadhi ya ushauri kutokana na changamoto zinazokabili Wizara hii kwamba shule zetu za msingi kwa kweli tunahitaji bajeti kubwa ya kutosha kwa maana ya kujenga majengo na hasa vyoo. Nimesoma ripoti ya Waziri, ratio ya vyoo kwa kweli inakatisha tamaa. Unakuta tundu moja la choo watoto wanaotumia ni wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama kwa muktadha wa afya kwa kweli sisi katika mkoa wetu na hasa Wilaya yetu ya Maswa tulipata tishio la kipindupindu kwani kuna baadhi ya shule kwa kweli zilistahili kufungwa. Nafikiri ungewekwa mkakati mzuri hata kama madarasa bado hatujajipanga vizuri na bado tunahangaika na madawati lakini tuhakikishe kwamba pawe na mazingira mazuri ya kupata huduma ya vyoo. Kwa kweli hali ya vyoo ni mbaya na inatishia afya za watoto wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hukohuko katika shule za msingi tunaomba basi Walimu waendelee kuboreshewa mafao yao, Walimu wana hali ngumu. Wilaya ya Maswa Walimu hawana nyumba za kutosha na wanaishi kwenye mazingira magumu. Ndiyo sisi kama Halmshauri tunafanya kazi kupambana kujenga na tunajaribu kuwaelimisha wananchi, lakini Wizara iweze kuongeza nguvu kuhakikisha kwamba Walimu wanaishi at least kwenye nyumba ambazo zinatia moyo. Ukienda katika vijiji vya Wilaya yangu ya Maswa ukienda Masanwa, Budekwa na maeneo mengine kwa kweli kuna hali ngumu sana ya nyumba za Walimu. Hivyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri atazame kwa kina ni namna gani anaweza akatusaidia.Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kutoa ushauri kwenye Halmashauri pengine Halmashauri yangu ya Maswa na Halmashauri zingine. Katika ujenzi wa maabara ukienda Wilaya zingine kwa kweli watu wamefanikiwa wamejenga maabara na wameweka vifaa. Mimi katika Wilaya yangu ya Maswa tuna mahitaji ya maabara 128, lakini tuna maabara nane tu ambazo zimekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri ukatafutwa uwezekano au utaratibu Halmashauri zikaweza kukopa benki fedha nyingi kuhakikisha miradi ya maabara inakamilika. Nina maana Serikali iziwezeshe Halmashauri ziweze kukopesheka. Ukipiga hesabu ya harakaharaka kwa mfano mimi nishapauwa maabara karibu 90 zinahitaji kukamilishwa na kuwekewa vifaa, inahitajika shilingi bilioni 3.5 ili kuweza kukamilisha. Halmashauri inakusanya fedha ndogo sana, ukienda kuwachangisha wananchi kwa kweli wananchi wangu hawana kipato kikubwa, kuchangisha kiasi hicho itachukua miaka, watoto wa Maswa hawataingia maabara kujifunza kisa wazazi wao hawana fedha, kisa wazazi wao ni walalahoi.
Halmshauri zetu zinakopesheka kwa riba ndogo na ikiwezekana tupewe muda mrefu. Mimi nilijaribu kwenda CRDB kuwaomba kwamba Halmashauri yetu ikope, tukapiga mahesabu ya shilingi bilioni 3.5 inahitaji tulipe zaidi ya milioni 80 kwa mwezi na hawataki kwa muda mrefu wanataka ndani ya miaka mitatu tuwe tumelipa lile deni.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba Halmashauri zikopeshwe na zipewe muda mrefu wa kulipa ili kusudi tuweze kupata fedha nyingi kwa wakati mmoja, tutafute wakandarasi wanaoweza kujenga zile maabara, watoto wetu wakaingia kujifunza ili sisi wazazi na Halmashauri tukaendelea kulipa deni. Naomba sana utaratibu huu ufanyike ili kusudi Halmashauri nyingi ziweze kupata maabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha upande wa shule vilevile kwamba maabara zinajengwa, ndiyo, maeneo mengine wameshajenga lakini suala la madawati nalo linashughulikiwa. Napenda kutoa pongezi kwa suala hili na naomba nguvu ya kutengeneza madawati inayotumika iendelee. Nashukuru kwa Wilaya ya Maswa sasa hivi madawati tunapata na nashukuru kuna fedha imerudi, Naibu Spika umerudisha fedha kwamba Wabunge tutapatiwa madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami naungana na wenzangu kusema kwamba madawati yale tunayaomba yaje kwa wakati tuyapeleke na sisi Wabunge tushiriki kuhakikisha madawati yale tunayapeleka maeneo husika, kwa sababu ni fedha zinazotokana na Bunge basi tunaomba wakati madawati yanapelekwa, basi sisi twende tukayakabidhi tuoneshe kwamba yale madawati yaliochangiwa ni sehemu ya fedha zinazotokana na Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la wazabuni. Kuna maeneo mengine nafikiri Wizara ilitoa ahadi kwamba itahakikisha wazabuni wanalipwa madeni yao. Imefika wakati sasa waje Wilaya yangu ya Maswa wahakiki madeni hayo na kuhakikisha wazabuni wale wanalipwa madeni yao. Wilaya ya Maswa tumepata fedha kidogo, shilingi milioni 18 tu tunasema haitoshi, kuna shule ya Maswa Girls, Binza Day, kuna wazabuni wanadai madeni makubwa Serikali haijalipa. Nafikiri Mheshimiwa Waziri ataiangalia Wilaya ya Maswa ili waweze kulipa madeni hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuungana na wadau wengine kwenye masuala ya utawala bora, naomba nichangie kidogo. Kwenye utawala bora tumeona jinsi watumishi hewa walivyokuwepo, natoa pongezi kwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha watumishi hewa wanaondoka katika nchi hii. Tunaomba juhudi ziendelee kufanyika, tuendelee kuhakikisha kwamba wale ambao walishiriki kuhakikisha kwamba kuna wafanyakazi hewa wanachukuliwa hatua ili liwe fundisho haya mambo yasiendelee kujirudia tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile napenda kutoa ushauri kwa Serikali kwamba ili kuondokana na watumishi hewa kuna maoni yametolewa hapa kwamba tuwe na system ambayo ni nyepesi ya kuweza ku-identify nani amefariki, nani kaacha kazi na nani kaajiriwa ili pawe na system ambayo inaweza ika-respond haraka. Pia ikiwezekana pawe na intergrated systems ambazo zina-connect data zote kwa watu wote nchini kwa mfano, Kitambulisho cha Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna dada mmoja alizungumza kwa upande wa pili alisema tuwe na intergrated system kwa maana ya kujua mtu aliyefariki, mtu ambaye ameajiriwa, pawe na system nyepesi kuweza kujua ni nani hewa, nani ambaye si hewa ili kusaidia Taifa lisiweze kuingia kwenye hasara kubwa ya kulipa mishahara mikubwa kwa watumishi hewa na kuondokana na hasara kubwa ambayo tulikuwa tunaipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumalizia kwa kusema kwamba nampongeza Mheshimiwa John Pombe Magufuli na Baraza lake la Mawaziri tumekwenda kwenye bajeti ambayo inaonekana ni ndogo lakini ni attainable. Ni bajeti ambayo tunaweza kukusanya fedha na tunaweza kuzitumia kwa jinsi bajeti ilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatoa pongezi kwa sababu siku za nyuma, bajeti zilikuwa zinaonekana ni kubwa lakini utekelezaji wake ulikuwa hauzidi asilimia 50, utekelezaji wake ulikuwa ni asilimia 30 mpaka 40, unakuwa na bajeti kubwa ambayo haitekelezeki. Tunapenda kutoa pongezi kwa wakati huu hata kama inaonekana bajeti ni ndogo lakini ni ya ukweli, tuendelee kupambana na tufanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuunga mkono hoja na nakushukuru sana.