Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyenijalia kunipatia afya njema inayoniwezesha kuchangia katika hoja iliyokuwepo mezani. Napenda kukishukuru Chama cha Wananchi (CUF) kwa kuniona kuwa nina uwezo wa kulitumikia Taifa hili na kunipa nafasi ya Ubunge wa Viti Maalum na sasa hivi nipo katika Kambi ya Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumshukuru Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad kwa juhudi zake anazozifanya, Mwenyezi Mungu atamjalia na atampa haki yake iliyokuwepo mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kunipa afya njema na leo nitajaribu kuchangia katika hoja iliyokuwa mezani hasa katika upande wa uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuliingia katika uwekezaji kwa nguvu zote tukitegemea uwekezaji utatupa faraja kubwa na kuinua kipato cha nchi yetu. Tunazungumzia kipato cha 7.3%, lakini hiki ni kipato cha watu waliokuwa na uwezo wa hali ya juu. Ukienda kuangalia uhalisia huko vijijini watu ni maskini wa kupita kiasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia Tanzania tutaweza kukusanya mapato ya trilioni 14, hii ni pesa ndogo sana. Hizi pesa kuna wafanyabiashara sasa hivi wanazo, wameingia katika soko la dunia na kuonekana wao ni matajiri wakubwa, wana uwezo wa kuwa na trilioni 26, Serikali tukiwa na trilioni 14 kwa maana moja tumezongwa, tumekamatwa na wafanyabiashara wao ndio wataitawala nchi, hii Serikali itakuwa haina uwezo wa kuweza kujitambua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naingia katika uwekezaji, tumeingia katika uwekezaji lakini tulisema tulikuwa na malengo, goals, strategic, commitment, transparent, implementation, monitoring and evaluation, corruption, tumekwama wapi? Tafiti zote hizi zilifanywa na tukasema sasa hivi Tanzania uchumi wetu utakuwa mkubwa mpaka nchi nyingine kama Rwanda uchumi wao unakuwa kwa kasi sisi tupo nyuma pamoja na kuwa na resources zote ambazo tunazo. Tunataka tuseme kwamba tumekwama kwanza hatupo katika usimamizi uliokuwa bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, corruption imesimama kwa hali ya juu, baadhi ya viongozi wanaosaini mikataba wanaangalia matumbo yao, siyo kuangalia nchi inafanya nini. Usimamizi na ufuatiliaji wa miradi, Sekta ya Uwekezaji imeingia katika kila sekta kwa mfano, ukienda katika madini kuna uwekezaji bado hatujafanya vizuri; ukienda katika kilimo kuna uwekezaji, bado hatujafanya vizuri; ukienda katika viwanda na biashara kuna uwekezaji, bado hatujafanya vizuri; tumekwama wapi? Tusilizungumzie pato la asilimia 7, hakuna kitu hapo ni uchumi mdogo sana kwa Mtanzania na Watanzania tunakua, tunahitaji maendeleo, watoto wapate elimu na sisi wenyewe tuwe na maisha bora, lakini maisha bora kama hatujaweza kuangalia usimamizi huu tuliokuwa nao, tutakuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na suala la utalii, utalii unaingiza kipato cha nje (in forex), lakini leo utalii unaingiza asilimia 22.7, mianya ni mikubwa katika uwekezaji. Wawekezaji ambao wapo ndani ya utalii, ndani ya mbuga zetu hawataki kuchangia hata concession fee. Tunajiuliza usimamizi uko wapi? Kama wale watu wanapata nafasi yote, TANAPA inajenga barabara, Ngorongoro inajenga barabara na mazingira yote ya kuwapelekea maendeleo wale watu, lakini hakuna pesa wanazotoa. Matokeo yake tumekwama katika usimamizi, tungepata mapato makubwa kama tungekuwa tunasimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Selous ambayo ni mbuga kubwa ya kwanza duniani, lakini haina kipato. Wawekezaji kule ni ujangili kwa kwenda mbele na hata hao watu wanaokamatwa, leo tunaona watu wanakamatwa na meno ya tembo 30,000, lakini hatujapata taarifa yoyote humu ndani ya Bunge. Mtu anakamatwa na pembe 30,000 ina maana ameua tembo 15,000 amefanywa nini, usimamizi upo wapi, mapato ya Taifa yapo wapi, tunaiacha nchi inaangamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwa na wanyamapori na misitu hakuna mapato yatakayopatikana ndani ya utalii. Utalii watu wanakuja kuangalia mazingira yetu tuliyokuwa nayo, iwe wanyama, na misitu yetu. Leo misitu inakatwa kama hatumo humu ndani, kuna Mtendaji wa Kijiji, kuna DC, kuna Mkuu wa Mkoa na watendaji wengine wanafanya nini kuhakikisha misitu inaimarishwa? Tembo atajificha wapi, faru atajificha wapi na simba atajificha wapi misitu yote inaangamia, mkaa kwa kwenda mbele, njia za panya zinaachwa, lakini viongozi wanahusika. Tunataka Serikali itupe tamko je, hali hii ya kuhakikisha utalii unakufa itaisha lini? Tunaona katika TV sasa hivi mpaka kobe, kasa wanatoka wanakwenda nje, sura pana wamekuja kuleta fujo ndani ya nchi hii, lakini tunawafanya nini sura pana? Hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji katika viwanda, wamechukua viwanda vyote wawekezaji vikiwemo Viwanda vya Korosho, Viwanda vya Mafuta, Viwanda vya Ngozi, lakini sijasikia viwanda vile kwa miaka 20 vikifanya kazi na Serikali ipo humu ndani, Mawaziri wapo humu ndani, watendaji wapo wanasimamia nini. Nenda Nachingwea kile kiwanda, ni ghala la kuweka mbao na majangili kuweka mapembe ndani ya vile viwanda, nani anafuatilia hivyo vitu? Nenda viwanda vya Mtama vya Korosho havifanyi kazi, Mtwara havifanyi kazi, Mbagala havifanyi kazi, halafu tunasema tunataka tupate uchumi endelevu, tutaupataje huo uchumi kama hakuna usimamizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe makini katika kusimamia, tufuatilie, tuachane na corruption. Corruption imekuwa ni donda ndugu ndani ya nchi hii. Hatujitambui, tumeachia uchumi tunaosema tuna uchumi, lakini uchumi huu ni kwa wageni, siyo Mtanzania halisia, nenda vijijini hakuna uchumi huo tunaozungumza hapa. Tusidanganye watu, tujipange katika uchumi ambao utamgusa mwananchi kijijini, siyo uchumi unawagusa watu waliopo Dar es Salaam na maghorofa. Maghorofa yale siyo ya Watanzania yale maghorofa ni ya wawekezaji ambao wanakwepa ushuru, wanakwepa kulipa kodi halafu tunajumuisha kuonekana Tanzania kuna uchumi wakati hakuna uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kuzungumzia suala la ajira na uwekezaji. Kwa vile hatusimamii humu ndani tumewahi kuuliza kwa Waziri, leo tunaona Wachina wanauza karanga Kariakoo, katika majumba ma-godown Wahindi wamejaa mle, wanatoka India kuja kufanya kazi za vibarua, je, Mtanzania atapata wapi ajira? Hakuna ajira kwa Watanzania, Watanzania hawana ajira, ina maana uchumi wa Tanzania unahamishwa kupelekwa kwa wageni. Tumejipanga kwa hilo, tunajiuliza maswali kama hayo kwa kujua, je, kama sisi Watanzania wazalendo tunajiangalia vipi. Tumeuhamisha uchumi tunaupeleka kwa wageni, lakini tumekaa hapa tunasema tunapanga mipango mipango, kila baada ya miaka mitano mipango, tunarudi nyuma katika enzi ya ujima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja katika upande wa kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo, lakini jiulize kila mwaka Tanzania kuna njaa. Hivi kweli kilimo kwanza kimemsaidia Mtanzania? Hakijamsaidia Mtanzania. Leo unampelekea Mtanzania kilo tano za mahindi, ana watoto, wajukuu, familia kubwa je, kilo tano alizopelekewa zitamsaidia nini Mtanzania yule?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika mahali unajiuliza, mvua kama hivi sasa hivi ya kutosha ipo Serikali imetoa juhudi gani kuwapelekea wananchi pembejeo, Serikali imetumia juhudi gani kuwapelekea wananchi mbegu iwe za mahindi, ufuta au karanga, hakuna, lakini utasikia mwakani tunaomba msaada wa chakula. Hii inatokana na sababu kwamba, hamjazisimamia sekta ya kilimo, mnawafanya wananchi wanahangaika na hata pale anapoweza kulima, akapata mazao yake, hakuna soko kwa mkulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima ni kundi ambalo wamekuwa watu wa kutangatanga wakitafuta soko; inapofika wakati wa mazao, wanakuja wababaishaji kuja kuchukua mazao yao kwa bei ya kutupa. Mazao yale wanayapeleka nchi za kigeni kuwa kama raw material, nchi haifaidiki hata na mazao yetu. Tanzania hata mchele tunapeleka nje, tunaletewa michele mibovu, Tanzania tunatoa mbegu za alizeti, lakini tunaletewa mafuta mabovu kutoka Ulaya kwa nini. Ndiyo maana sasa hivi Tanzania tuna kasi kubwa ya kansa, tunakula mafuta mabovu, lakini je, viwanda vyetu vinafanya nini, tulikuwa na viwanda vya kusindika mbegu na kupata mafuta Mwanza…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lulida muda wako umekwisha.
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Ahsante sana. (Makofi)