Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuleta haya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2016/2017. Wamejitahidi sana kuweza kuoanisha na nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango na timu yake kwa kiujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika huu Mpango naomba nichangie maeneo machache kwa sababu ya muda. Jambo la kwanza ambalo ningependa nishauri, ili tuweze kuwa na maendeleo katika huu mwaka mmoja, tuendelee kupunguza urasimu uliopo katika maeneo mbalimbali, ambayo ndiyo yanaongeza kipato cha Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ambayo imeshaanza kufanyika bandarini, TRA na kwenye border zetu kama Tunduma, Kyela, Namanga kote huko tuendelee kufanyia kazi. Pia Mamlaka husika kama ya mazingira na yenyewe pia iendelee kuangalia muda ambao wana-process vibali mpaka mtu anapata kuweza kufanya shughuli ambayo ameiomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie eneo lingine ambalo ni suala zima la uchumi. Ili uchumi uweze kukua kuna vigezo mbalimbali, lakini kuna michango ambayo inachangia kukua kwa uchumi na vipato vyetu. Tumeangalia kipato kimekuwa mpaka kimefikia shilingi 1,700,000/=, ni hatua nzuri ya kuonesha kwamba uchumi umekuwa, lakini kuna sekta hambazo hazikufanya vizuri katika kipindi kilichopita na hasa upande wa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kufikia 3.4%, na lengo lilikuwa ni 6% na upande wa kilimo ndio eneo ambalo limeajiri zaidi ya watu 70%. Sasa tunaomba kwenye huu Mpango wa mwaka mmoja 2016/2017 na katika bajeti, Serikali iangalie matatizo yaliyojiri, tukafikia 3.4%, badala ya 6% na iweze kurekebisha na hasa ni katika fursa mbalimbali na pembejeo ambazo wakulima hawapati ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika Mpango huu tumezungumzia kuboresha fursa upande wa viwanda, lakini hatujagusa upande wa viwanda vidogo vidogo. Sehemu kubwa ambayo naiona bado elimu ya ujasiriamali kwa watu wetu haijafika ipasavyo na wafanyakazi wa Halmashauri hasa Maafisa Biashara, wanatakiwa waifanye kazi hiyo ili watu wetu wajue na wapate hizo fursa za kufungua biashara ndogo ndogo na hizi ziendane kutokana na maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, katika kuongeza mapato, ni Taasisi za Serikali, zamani tuliona Jeshi la Magereza likiwa ni mojawapo likijishughulisha na uzalishaji, mazao ya biashara na mazao ya chakula. Hata hivyo, sehemu nyingi sana sasa hivi za Magereza hayazalishi, sasa tatizo liko wapi? Liangaliwe na wenyewe waingie katika kuchangia kwenye pato, tunawagharamia sana Magereza lakini uingizaji ni mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mapato na kukuza uchumi na swali leo limeulizwa na Mheshimiwa Risala ni utalii, mbuga ya Katavi, Ruaha, Udzungwa, Mikumi ni sehemu ambazo haziangaliwi na kupewa kipaumbele. Matatizo ambayo yameoneshwa tunaomba Serikali kupitia Wizara zake, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa pamoja ziangalie kwenye bajeti hii ya mwaka 2016/2017, kuboresha miundombinu ambayo inakwenda kwenye hizi mbuga ili tuweze kuongeza kipato, pamoja na kuzitangaza. Kwa hiyo, tunaingia gharama lakini Serikali itaingiza fedha kwa kupitia watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingine napenda niizungumzie tena, ni kuhusu mashirika ya umma. Tumekuwa na mashirika ya umma ambayo yanaendelea kuitia hasara Serikali, hayajiendeshi kibiashara. Namuunga mkono Mbunge wa Kigoma Mjini, Mheshimiwa Zitto, suala la Air Tanzania liangaliwe, retrenchment ifanyike, watu waingie kwenye mikataba ya ajira mipya, wapunguzwe wafanyakazi na tuweze kwenda kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na yote tunayozungumza hapa, lazima turejee kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, tuone kitu gani ambacho kimeandikwa na tuangalie utekelezaji. Katika ilani ya Chama cha Mapinduzi tumeahidi kutengeneza reli katika kiwango cha Kimataifa, standard gauge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, katika haya mapendekezo gharama za upembuzi yakinifu, reli mpya kuanzia Mpanda kwenda Kalema na kukarabati kuanzia Kaliua mpaka Mpanda, iingie na iwemo na reli ya kuanzia Uvinza kwenda Burundi na yenyewe iingie iwemo katika upembuzi yakinifu kwa mwaka huu 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini iwe hivyo? Kwa sababu tayari nchi ya Burundi ina uhitaji wa haraka na wenzetu wa Kongo na wenyewe kwa habari ambazo sina hakika wameshaanza kutengeneza reli ya kuja Ziwa Tanganyika ili mizigo ipitie Kalema. Sasa sisi kwa upande watu tuanze kazi haraka iwezekanavyo na tunamwomba Mheshimiwa Waziri iingie katika bajeti hii, huu upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika ripoti ya miaka mitano iliyopita ya maendeleo, tulisema tutajenga reli kilometa 2,707. Mwaka huu wa mwisho tulisema tutajenga kilometa 197, lakini tumeweza kujenga kilometa 150. Tuangalie ni wapi tulikwama, tatizo ni fedha au tatizo ni utawala? Tunaomba reli yetu ya kati iwekewe kipaumbele, iweze kutengenezwa katika kiwango cha Kimataifa na ili tuweze kuingiza mapato kutokana na mizigo ya ndani pamoja na mizigo ya nchi jirani. Hilo nalo liingie katika huu mwaka 2016/2017 na lionyeshwe kwa kutajwa kilometa zitakazotengenezwa na maeneo wapi mpaka wapi na isiwe tu nadharia inayotaja idadi bila kujua na maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie kwenye suala zima la elimu. Tumeelezwa kwamba kutokana na mafunzo ya kiujumla kusomesha watu, lakini kuna Kanda nyingine hakuna Vyuo Vikuu. Tanzania ukanda wa Mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa ukanda ule pia hakuna Vyuo Vikuu. Sasa katika kugawa rasilimali kijografia na yenyewe tuangalie tuweze kupata Chuo Kikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile niongezee katika suala zima la miundombinu. Tumeeleza fursa Tanzania ni nyingi na lazima kuwe na viwezeshi, kiwezeshi kimojawapo pia ni kuboresha miundombinu ili wawekezaji waweze kufika. Hata hivyo, katika sehemu nyingi barabara hatuna na hasa Mkoa wa Katavi. Tuna fursa nyingi, tuna madini, gesi, mafuta, lakini barabara hakuna. Barabara ya kuunganisha kutoka Uvinza kuja Mpanda tunaomba ianze na iingie kwenye bajeti hii na pia tuweze kupewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii na naunga mkono na naomba yote niliyopendekeza yafanyiwe kazi. (Makofi)