Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuipongeza Serikali kwa usikivu wake wa kusikiliza kilio cha wananchi na kutoa agizo la kukubali kuagiza sukari. Huo ni uthibitisho kwamba hii ni Serikali tulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo napenda pia kuwashukuru Mawaziri. Kuna mjumbe mmoja alipokuwa anachangia alisema Mawaziri hawa wako reachable, kwa kweli na mimi nawapongeza kwamba ni kama simu ukipiga inakuwa reachable. Wakati mwingine hawa hata kama hujapiga wako reachable.
Nasema hivi kwa sababu nilifanya ziara katika Jimbo langu na Mheshimiwa Jafo, Naibu Waziri alipoona taarifa ya ziara ile na yeye akaenda kutembelea pale mahali ambapo mimi nilikwenda kutembelea ili kujionea mwenyewe zile changamoto. Kwa hiyo, hii ni uthibitisho wa usikivu pia wa Mawaziri hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo nianze kwanza kwa kusema kwamba tumesema tunapokusudia kujenga uchumi wa viwanda sekta binafsi ni injini ya kujenga uchumi huo. Mimi napenda kuongeza kwamba injini hii bila oil, ambapo kwangu mimi oil ni utumishi wa umma (public service) maana yake ni kwamba injini hii inaweza ika-knock. Kwa sababu hiyo basi, niiombe Serikali kupitia Wizara husika iwatazame watumishi wa umma walau kwa baadhi ya mambo kwa mfano fedha zao za likizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetokea kwenye utumishi wa umma ambapo ikiwa mwaka huu utakwenda likizo basi utalipwa fedha yako ya nauli mwaka unaofuata hulipwi, unalipwa alternatively. Sasa naomba wakati Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza makusanyo na kubana matumizi basi iwatazame watumishi wa umma katika suala hili. Pia iwatazame katika fedha zao za uhamisho kwa mfano walimu. Hata katika hii nauli unakuta mtu anakwenda likizo halafu anaambiwa fedha yako utakuja kulipwa ukirejea na inaweza kumchukua hata miaka mitatu, mwingine anakata tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie nauli kwa watumishi wa umma wanaokaa maeneo ya mijini. Mnafahamu kwa mfano Jiji la Dar es Salaam Serikali ina utaratibu wa kutoa mabasi lakini kuna maeneo mengine ya mikoani ambako watumishi wanatoka umbali mrefu kwenda kwenye maeneo ya kazi. Sasa kama sehemu ya kuwaongezea morale na kuwapunguzia ukali wa maisha, nashauri Serikali ilitazame jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusiana na Waraka huu wa Serikali, labda niusome. Kuna Waraka wa TAMISEMI Na.CFB/173/355/0 wa tarehe 06/06/2011 wenye kichwa cha habari kinachosema Majukumu ya Maafisa Biashara na namna bora ya utoaji taarifa. Mojawapo ya majukumu katika waraka huu ni kuhamasisha shughuli zilizo chini ya viwanda, biashara na masoko na uwekezaji pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali ili kuongeza kipato cha wananchi na kuongeza wigo wa kodi katika Serikali za Mitaa na Serikali Kuu.
Sasa ukienda katika halmashauri zetu ofisi za biashara si kitengo wala si idara isipokuwa ziko ndani ya Idara ya Fedha. Naziomba Wizara hizi mbili zijaribu kuangalia muundo wa Maafisa Biashara ili kusudi hata hizi shilingi milioni 50 ambazo tunatarajia zitatoka kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais basi zikawe na tija ili Maafisa Biashara wasibaki tu kuwa watu wa kukagua leseni bali wawe watu ambao wanaweza kusaidia wananchi katika kung’amua fursa mbalimbali za kijasiriamali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu nijielekeze katika Sekretarieti ya Ajira. Napenda kuipongeza kwa sababu kweli tuna changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira lakini jinsi ambavyo imejitengeneza kimtandao, jinsi ambavyo watu wana-apply online na maombi yao yanaendelea kutunzwa online ni jambo la kupongeza kwa sababu pia linapunguza malalamiko katika ajira ya utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niombe pengine ingeanza kwenda kwenye zones ili kuwapunguzia waombaji wa nafasi za kazi gharama zile za nauli na malazi kwa sababu mpaka sasa hivi pamoja na kuwa kuna nyakati inafanya interview kwenye maeneo ya nje ya Dar es Salaam lakini asilimia kubwa ni Dar es Salaam. Sasa uwezo utakapoongezeka basi tuanze walau na zone kwa ajili ya kuwasaidia watafuta ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, nijikite sasa kwenye Jimbo langu. Namshukuru tena Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea katika shule ya msingi Mchanganyiko Makalala. Shule hii ina watoto wenye mahitaji maalum. Kwa sababu shule hii iko katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga lakini ni kama shule ya kitaifa kwa sababu inachukua watoto kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu basi Serikali iitazame kwa macho mawili. Nampongeza Naibu Waziri na Wizara kwa ujumla kwa hatua ile ya kutembelea shule ile, naamini changamoto zile alizojionea zitamsaidia katika kuona umuhimu wa kuitazama shule hii kwa macho mawili katika uwiano wa walimu lakini pia miundombinu ambayo kwa kweli siyo rafiki sana kwa watoto wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala la elimu naiomba Wizara, Mheshimiwa Rais alipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam tarehe 13/02/2016 aliahidi kwamba ataupa Mkoa wa Dar es Salaam shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kukabiliana na ongezeko la wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza.
Niiombe Serikali hata sisi tunaotoka kwenye Halmashauri za Miji changamoto hii tumekutana nayo. Mafinga pale kuna ongezeko la watoto kwa asilimia 135. Serikali itutazame kwa sababu kwanza ni Halmashauri mpya bado haina makusanyo lakini pia iko mjini. Sasa sisemi kwamba na sisi tupewe shilingi bilioni mbili lakini tutazamwe kwa chochote kitakachoweza kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na suala la pampu. Pale tuna pampu ilipaswa iwe imefungwa toka mwezi wa kumi na moja lakini mpaka wakati huu yule aliyepewa kazi ya ku-supply amekuwa anapiga chenga. Kwangu naona hili ni jipu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa sababu wao ndiyo walitakiwa wanunue pampu na kutufungia sisi kwenye Halmashauri ya Mji. Ametuletea pampu haina TBS certification, haina manual, maana hata ukinunua simu Kariakoo ya shilingi 18,000 unapewa manual, lakini pampu hii hata manual haina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie katika suala la utawala bora. Wenzetu upande wa pili kule wanalialia Rais apunguze kasi ya kutumbua majipu. Mimi nasema tumuunge mkono Mheshimiwa Rais. Kuwa opposition sio kupinga kila kitu. Madawati kupinga, ujenzi wa maabara kupinga, hapana, kuna mambo tumuunge mkono Mheshimiwa Rais. Mimi naamini ninyi huko si majipu kwa hiyo mpunguze kulialia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, nimalizie kuzungumzia wastaafu ambao wanahudumiwa na LAPF wanalalamika kwamba wenzao wa central government tayari wameongezewa lakini wao bado. Kwa hiyo, niombe pia suala hilo litazamwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, niwahakikishie wana Mafinga kwamba nitaendelea kuwatumikia bila kuangalia rangi wala itikadi zao, ahsante sana.