Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuchangia kwenye hotuba ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nawapongeza Mawaziri wote wawili kwa hotuba zao nzuri sana, zimesheheni mambo mengi, hata hivyo, pamoja na hotuba nzuri napenda kutoa maboresho kwenye maeneo machache yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni suala zima la utawala bora na uwajibikaji. Taarifa na hotuba inaeleza vizuri baadhi ya watumishi ambao wamekuwa wakifanya makosa na wakivuruga wanawajibishwa kwa kufuata taratibu za kinidhamu na hatimaye pia za kijinai. Wapo ambao pia wamepelekwa Mahakamani, wapo ambao wamefukuzwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na taarifa hii inaonesha tuko vizuri sana katika utaratibu huu, lakini kiuhalisia nikitoa mfano wa Halmashauri kama ya kwangu ya Kondoa Mjini wamekuwepo watu wengi sana ambao wamekuwa wakivuruga hasa Maafisa Ardhi, hata Mkurugenzi aliyekuwepo. Kinachotokea badala ya kuwajibishwa kutokana na makosa yaliyofanyika, wanahamishwa. Sasa unapomhamisha huyu mtu unahamisha tatizo siyo? Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Mawaziri, badala ya kufanya suala la kuwa-reshuffle hawa watumishi wanaovurunda, taratibu za kuwawajibisha kinidhamu na hatimaye kijinai zifanyike kwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na Maafisa Ardhi wengi sana wamekuwa wakituvuruga, anatoka Kondoa anapelekwa Rombo, anatoka Rombo anapelekwa sijui eneo lingine, wanaenda kuhamisha matatizo tu hayo. Pia wapo ambao kesi zimepelekwa Mahakamani, lakini wanatoka pale wanakwenda Makao Makuu TAMISEMI, wanasema sijui wamekaa benchi au vipi, sasa utaratibu huu haujengi nidhamu ya kuwafanya hawa watumishi wengine wawe waadilifu na wafanye kazi zao kadri ya miongozo na taratibu zinavyowataka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri huu utaratibu wa kutumbua majipu, huku kwenye Halmashauri zetu uende vizuri kabisa, watu kweli watumbuliwe maeneo yote, siyo mtu anavuruga halafu anahamishwa, hii haitatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, ipo hali ya baadhi ya watumishi kutokuwajibika, mfano, sasa hivi Halmashauri yangu ni zao la Halmashauri iliyokuwepo, wale wote ambao walionekana kwamba they are non- performance, wanahamishwa wanapelekwa kwenye Halmashauri mpya, kweli hakuna utaratibu tunaoweza kujiwekea kupima performance ili hawa ambao mwisho wa siku hawa-perform wawajibishwe? Nafikiri hilo ni suala muhimu sana la kuliangalia Waheshimiwa Mawaziri, ili watumishi wetu wanaokuwa Serikalini na kwenye hizi Halmashauri waweze kuwa wawajibikaji wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala zima la elimu, kwenye elimu naongelea suala la Walimu, nikianza na upungufu wa Walimu. Upungufu wa Walimu ni tatizo kubwa, najua utaratibu unafanywa ili Walimu wengine watoke vyuoni waweze kuingia kwenye mashule kufundisha, lakini wanapotoka upungufu ni mkubwa sana hapa katikati, shule zinateseka, wanafunzi wanaumia, wanashindwa kupata masomo yao kadri inavyostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale kwangu kwenye elimu ya Sekondari tuna upungufu wa Walimu zaidi ya 80. Jibu dogo tu la Kondoa Mjini upungufu zaidi ya Walimu 80, kwenye shule ya msingi kuna upungufu wa Walimu zaidi ya 60. Mpaka waje kutimia na mahitaji najua ni ya nchi nzima, utakuwa mtihani mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri kitu kimoja, wapo wale Walimu ambao in the interim kama mpango wa muda mfupi tu wakati tunasubiri uzalishaji wa wale Walimu wengine wapya. Wapo Walimu ambao walistaafu, haiwezekani tukawapa mikataba ya muda mfupi, wa- fill hii gap in the interim wakati tunasubiri hao wengine wanakuja, itusaidie kidogo kupunguza makali ya upungufu wa Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niliweke hilo kama changamoto na mapendekezo ya kuboresha hawa Walimu ambao tunazungumzia wanadai mafao, wanadai malimbikizo ya mishahara, hebu tuwatumie wale wanaweza wakatusaidia kwa muda mfupi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa hapo, katika suala la Walimu, najua hili litamgusa zaidi Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako, pia nataka niliweke hapa kwenu, Walimu na nilizungumza kwamba mkazo wangu upo sana kwenye elimu. Walimu watokane na best performance, siyo Walimu watokane na yale madaraja ya mwisho ndiyo wanaenda kuwa Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kufanya ni kuboresha maslahi yao pia kuwa-remunerate vizuri, kuwa- compensate vizuri na kwa kuwa ajira yao itakuwa inaonekana ina uhakika zaidi na iko vizuri wanafunzi wengi watataka kwenda kufanya hii kazi ya Ualimu. Tutakuwa tumewa-motivate, tumewa-inspire, matokeo yake kazi ya Ualimu itaonekana ni kazi yenye heshima, siyo kazi tu ya wale wanaofeli. Wanalipwa vizuri, wanatengenezewa mazingira mazuri ya kazi, matokeo yake inawa-motivate na kuwa-inspire watoto wetu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Profesa Ndalichako katika marekebisho yetu tunayoyafanya, moja ya vitu vya kuhakikisha vinarekebishwa ni kuona kwamba Walimu wanatokana na best performance.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa hapo elimu, naomba sana hili najua linaenda zaidi kwa Profesa Ndalichako Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi tena, tubadilishe huu utaratibu wa madaraja, tunasema ufaulu ni asilimia kubwa, tunaamini kwamba mpaka division IV ni ufaulu!
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tusijidanganye, tunajipa picha kwamba watu wetu wanafaulu, kumbe tunakwenda kupeleka katika soko la ajira watu ambao hawako competent. Turudishe ufaulu division one mpaka three, ndiyo iwe maximum ya ufaulu na watu watajitahidi, watu watapambana, na Walimu watapambana kuhakikisha kwamba vijana wetu wanafaulu katika madaraja hayo.
Mheshimiwa Nabu Spika, tunajiridhisha tu kwamba ufaulu mwaka huu asilimia 69 kumbe kuna division four kule ndani, division four ni ufaulu? Haiwezekani tunataka tutoe Taifa la watu ambao wanajiweza. Taifa la watu ambao wako competent, tukitoka hapa tunashindanishwa na watu wa Mataifa mengine, tuweze ku-survive. Naomba sana hilo tulizingatie na kama inawezekana , tuanze kulibadilisha sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu nataka kuliongelea kidogo ni maji. Katika Jimbo langu la Kondoa kuna upungufu mkubwa sana na tatizo kubwa sana la maji Mjini pamoja na Vijijini. Pamoja na upungufu wa maji huu na miradi inayokwenda michache, bado usimamiaji wa miradi ambayo ilikwenda kule mwanzo siyo mzuri kiasi kwamba miradi inakufa, visima vinashindwa kuendeshwa vizuri, wale watu hawapati elimu ya kutosha, Kamati za Maji hazijielewi, matokeo yake hata ile miradi michache iliyokwenda inakufa na tatizo linazidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba Waziri wa TAMISEMI suala hili tuliangalie, tuhakikishe maelekezo mazuri yanakwenda kwenye Halmashauri zetu, watu wasimamiwe wapate maelekezo mazuri, Kamati ziundwe, ziwe zinakuwa monitored, matokeo yake miradi iweze ku-survive. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua bajeti yenyewe ni ndogo, hiyo miradi michache itakayokwenda kule lazima tuilee na iwe endelevu, bila usimamizi mzuri, tunawaelewa watu wetu vijijini, itakuwa changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimependa nizungumze hayo matatu tu katika hotuba hizi mbili. Nakushukuru sana na naunga mkono hoja.